LUGHA NA SIASA
LUGHA YA KISWAHILI MHIMILI MKUU KATIKA SIASA WAKATI lugha yoyote ile inakuwa na umuhimu mkubwa, hasa kama kiunganishi cha watawala na watawaliwa, mfumo wa elimu uliopo hugeukiwa kuwa njia kuu ya usambazaji wake. Nchini Tanganyika (kabla ya kuwa Tanzania) chini ya utawala wa Wajerumani, mojawapo ya majukumu ya kimsingi ambayo Kiswahili kiliyatelekeza yalikuwa ni kuziunganisha jamii za Kiafrika na Wajerumani; ambao walikuwa wageni. Unganisho la pili ambalo Kiswahili kilitekeleza ni lile la utabaka kwani Wajerumani, kama wakoloni wengine katika mataifa ya Afrika, walikuwa wakionekana kama “wa tabaka la juu.” Wajerumani walikuwa wamekichagua Kiswahili kama lugha ya kiutawala, ambapo walifaulu kuwafunza watawala wengi kutoka pande zote mbili-Waafrika na Wajerumani kuendesha utawala wao. Mfumo wa kiutawala uliowekwa ulioana pakubwa na sera ya lugha iliyokuwepo, ambayo kimsingi ilikuwa ikilenga kuhakikisha kuwa walifaulu kutumia Kiswahili kama nguzo kuu ya kufani...