LUGHA NA SIASA

LUGHA YA KISWAHILI MHIMILI MKUU KATIKA SIASA
 
   

WAKATI lugha yoyote ile inakuwa na umuhimu mkubwa, hasa kama kiunganishi cha watawala na watawaliwa, mfumo wa elimu uliopo hugeukiwa kuwa njia kuu ya usambazaji wake.
Nchini Tanganyika (kabla ya kuwa Tanzania) chini ya utawala wa Wajerumani, mojawapo ya majukumu ya kimsingi ambayo Kiswahili kiliyatelekeza yalikuwa ni kuziunganisha jamii za Kiafrika na Wajerumani; ambao walikuwa wageni. Unganisho la pili ambalo Kiswahili kilitekeleza ni lile la utabaka kwani Wajerumani, kama wakoloni wengine katika mataifa ya Afrika, walikuwa wakionekana kama “wa tabaka la juu.”


Wajerumani walikuwa wamekichagua Kiswahili kama lugha ya kiutawala, ambapo walifaulu kuwafunza watawala wengi kutoka pande zote mbili-Waafrika na Wajerumani kuendesha utawala wao.
Mfumo wa kiutawala uliowekwa ulioana pakubwa na sera ya lugha iliyokuwepo, ambayo kimsingi ilikuwa ikilenga kuhakikisha kuwa walifaulu kutumia Kiswahili kama nguzo kuu ya kufanikisha lengo lao la udhibiti wa kisiasa nchini humo.
Wadadisi wa kihistoria wanakubaliana kwa pamoja kuwa juhudi za kisiasa za Wajerumani kuimarisha Kiswahili wakati wa ukoloni zimechangia sana katika chocheo la nafasi kubwa ambayo lugha hiyo inapewa nchini Tanzania hadi sasa.

Utabaka
Kuu linalorejelewa ni sisitizo la uondoaji wa utabaka kati ya Waafrika na Wajerumani, ambalo lilikifanya Kiswahili kukubaliwa kama lugha ya matabaka yote-watawala na hata watawaliwa.
Katika robo ya kwanza ya karne ya 20, kulikuwa na nia sawa ya matumizi ya Kiswahili nchini Kenya na Uganda kati ya watawala na watawaliwa. Kama nchini Tanzania, Kiswahili pia kilipewa umuhimu mkubwa katika sera za elimu za mataifa hayo mawili.
Hata hivyo, Kiswahili hakikupewa vipindi vingi vya masomo, kama yalivyopewa masomo mengine. Katika baadhi ya shule, lugha hii ilitumiwa na “tabaka la chini”-wengi wakiwa Waafrika waliokuwa wameajiriwa au walikuwa wakisomea katika shule hizo.
Katika nchi hizo mbili, watawala kutoka Uingereza walihitajika kujifunza Kiswahili. Kulingana na Kipengele 19 cha Kanuni za Uajiri za Agosti 1, 1903, maafisa wote wa Uingereza walihitajika kujifunza lugha hiyo “ili kuwawezesha kutaasisisha” utawala wa kikoloni katika nchi hizo mbili.
Maafisa walioteuliwa baada ya tarehe hiyo nchini Uganda walihitajika kuwa na ufahamu kidogo wa Kiswahili. Walipewa mwaka mmoja kujifunza lugha hiyo pindi tu baada ya kufika nchini humo. Msingi wao wa kupandishwa madaraka ulitegemea kiwango cha ufahamu wa Kiswahili ambacho walikuwa nacho. Manufaa mengine ambayo maafisa hao walikuwa wakipata kutokana na ufahamu wa Kiswahili ni kuwa walilipwa mishahara ya juu kuliko wenzao ambao bado hawakuwa wakikifahamu.
Utawala wa Uingereza ulitathmini ufahamu wao kupitia mitihani maalum, ambayo walipewa, ambapo wale waliopita walikuwa wakipandishwa madaraka.
Kwa kuzingatia umuhimu wa Kiswahili katika uunganishaji wa kisiasa wa Afrika Mashariki, mamlaka za Uingereza zilibadilisha lugha ya kiutawala nchini Uganda kutoka Luganda hadi Kiswahili mnamo 1914.
Lililofuata ni kuwa Kiswahili kilikumbatiwa na kuwa mojawapo ya lugha muhimu zaidi nchini humo, hadi wakati wa utawala dhalimu wa Idi Amin Dada katika miaka ya 1970, ambapo raia wa taifa hilo walianaza kubadili dhana zao kuhusu Kiswahili, baada ya kuonekana kama ndicho kilitumiwa na wanajeshi na polisi kuendesha ukatili dhidi ya raia.

Kutafuta uungwaji mkono
Kufikia wakati wa uhuru nchini Kenya, viongozi wengi tayari walikuwa wamekumbatia Kiswahili kama lugha yao ya matumizi ya kimsingi. Kichocheo cha matumizi hayo kilitokana na nia yao ya kutaka kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa kutoka kwa wananchi.
Hata hivyo, lugha hii ilipata upinzani katika miaka kumi ya kwanza baada ya uhuru, licha ya umuhimu wake mkubwa kama kiunganishi cha kisiasa.
Wakati mswada ulipowasilishwa Bungeni mnamo 1969, ukipendekeza lugha hiyo kufanywa kuwa rasmi nchini, wapinzani wake waliioanisha na Uislamu pamoja na Uarabu.
Kwa mfano, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu mwenye nguvu wakati huo Bw Charles Njonjo alisema kuwa: “Usuli wa Kiswahili ni Uarabuni. Ni lugha iliyotoka Uarabuni. Si lugha yetu, na si mojawapo ya lugha za Kiafrika zilizokubalika.”
Licha ya hayo, Kiswahili kimepiga hatua na kuwa kiunganishi kikuu cha kisiasa katika kanda nzima ya Afrika Mashariki.

Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?