Uhakiki wa Fonimu na Miundo ya Silabi za Kiswahili 10 Uhakiki wa Fonimu na Miundo ya Silabi za Kiswahili Benard Odoyo Okal Ikisiri Fonimu ni kipashio kidogo cha sauti ya lugha chenye uwezo wa kubainisha maana na hudhihirika kama irabu au konsonanti. Kama ilivyo katika lugha nyinginezo ulimwenguni, Kiswahili vilevile kina fonimu za kategoria mbili yaani irabu na konsonanti. Hata hivyo, idadi ya fonimu konsonanti za Kiswahili inaelekea kuainishwa tofautitofauti kwa mujibu wa wanaisimu mbalimbali wa Kiswahili. Mathalani, wanaisimu wengine wanadokeza idadi ya fonimu konsonanti kuwa 24, 25, 26, 29, 32 au 33. Kwa upande mwingine, miundo ya silabi za Kiswahili pia hudokezwa kuwa tofauti kama vile 4, 5, 6, 7 na 8. Idadi tofauti ya fonimu konsonanti za Kiswahili pamoja na idadi tofauti ya miundo ya silabi za Kiswahili huelekea kuwakanganya wasomaji wa lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, makala hii inalenga kuhakiki fonimu na miundo mbalimbali ya silabi za Kiswahili. Ili kufanikisha uhakiki huu...