Umuhimu wa Kiswahili katika Taifa
Mwalimu J. K. Nyerere ametuasa tusiwe wabinafsi katika masuala yahusuyo taifa. Suala la ubinafsi amelipiga vita tangu alipoasisi taifa hili na kutuagiza tuondokane na unafsi kama alivyoandika katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe.’ Kitabu hiki kilichapishwa mwezi Juni 1962. Kwa maana hiyo, alitupa fursa ya kuielimisha jamii bila uchoyo na husuda.
Katika eneo la lugha, tunayo mambo mengi tunayoweza kujifunza kwa faida yetu binafsi, kwa taifa letu na kwa ulimwengu mzima kwa jumla. Hapa yafaa nitoe ufafanuzi kidogo. Katika miezi ya hivi karibuni liko jambo lililotokea huko Uingereza ambalo ni mfano wa kuigwa.
Wabunge wa Bunge la Uingereza ambao ni wapenzi wa lugha yao ya taifa hawakuridhishwa na hadhi ya lugha yao inavyotumika kitaifa na kimataifa. Wameishauri Serikali yao iimarishe ufundishaji wa lugha ya Kiingereza katika shule zote na hasa vyuo vya lugha. Pia waliishauri serikali kufundisha Kiingereza kwa umakini mkubwa katika shule na vyuo. Pia walishauri kuwa shule na vyuo vya lugha viongezewe fedha katika bajeti kila mwaka ili kupatiwa fedha mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2011/2012. Pamoja na kutilia mkazo mafunzo ya lugha yao, wamesisitiza pia lugha za kigeni zisomeshwe kwa watu wa kada mbalimbali hasa wanadiplomasia.
Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge imeshauri kuwa kupandishwa vyeo kwa maofisa kutokane na ujuzi na weledi wa Kiingereza pamoja na lugha moja ya kimataifa. Wamekubali bajeti kwa mafunzo ya lugha iongezeke kutoka $ 3 milioni kwa mwaka 2011/12 hadi $ 3.9 milioni kwa mwaka 2013/14. Vilevile idadi ya wanafunzi kwa mwaka iongezwe na kuwa 1000.
Lugha kubwa za nchi za nje kama lugha ya Mandarin, Kiarabu, Kihispania na Kireno zisomeshwe shuleni. Lugha ya Mandarin ni lugha rasmi na lugha ya taifa la Wachina. Lugha ya Kihispania hutumika katika nchi za Argentina, Chile, Uruguay, n.k. Kireno hutumika katika nchi za Brazil, Cuba, Venezuela, n.k Kireno. Nchi za Argentina, Chile, Uruguay, n.k. hutumia Kihispania. Lugha hizi mbili hutumika katika nchi za Amerika ya Kusini. Lugha ya Kiarabu nayo inatiliwa mkazo kama lugha muhimu na sababu kubwa ni za kiuchumi na kisiasa.
Je, Waingereza wamegundua nini walipoamua kufungua tena chuo chao cha lugha walichofunga mwaka 2007? Bila shaka wamegundua kuwa nafasi ya lugha ni kubwa duniani hasa katika mazingira ya utandawazi kama masuala ya diplomasia, biashara, siasa na uchumi. Uamuzi wa kujifunza lugha ya Kiarabu, Kimandarin, Kihispania na Kireno ni kuwawezesha Waingereza kujua kwa undani masuala mengi yanayowahusu Wachina, nchi za Amerika ya Kusini na Waarabu katika biashara. Kwa upande wa Kiarabu ni dhahiri kuwa ni suala la mafuta.
Katika bara la Afrika, ziko lugha tofauti ambazo zinatufanya tusielewane kutokana na sababu za kihistoria. Nchi za Afrika zinatumia lugha zenye asili ya kikoloni kama Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kiingereza. Hizi ndizo lugha zinazotumika katika vikao vya Umoja wa nchi za Afrika (AU)
Lugha ya Kiafrika iliyokubaliwa kutumika katika shughuli za kikazi za AU ni Kiswahili. Tanzania ilipewa jukumu la kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili kifikie hadhi ya Kimataifa. Agizo hili lilitolewa mwaka 1988 huko Addis Ababa, Ethiopia.Tumefikia wapi tangu mwaka 1988 Tanzania ilipoteuliwa katika kikao kilichofanyika huko Mauritus cha Mawaziri wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) na kuridhiwa na Wakuu nchi na serikali mwaka huo huo? Ilitakiwa uandaliwe utaratibu wa mafunzo ya ukalimani na tafsiri kwa ajili ya kuwaandaa wataalamu kwa kazi katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika.
Mafunzo yaliandaliwa kwa kuwapeleka wataalamu wazalendo waliozifahamu lugha za Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili. Wataalamu hawa walipelekwa Chuo Kikuu cha Paris kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baada ya kufaulu walirejea nyumbani llakini hawakuelekezwa kujiandaa kwenda Addis Ababa. Mpaka leo mpango wa kwapeleka Watanzania Addis Ababa haukutekelezwa kikamilifu.
Kwa suala la ukuzaji wa Kiswahili ndani ya nchi, mipango imekwama ya kukuza Kiswahili kutokana na kutokuwepo kwa sera ya lugha iliyo wazi. Kila waziri mwenye dhamana ya kusimamia lugha anapoteuliwa huwa hana mawazo ya kutupeleka mbele katika kukifanya Kiswahili kiwe ni lugha imara ya kitaifa.
Hapa nchini kiko kituo cha kufundisha lugha za kigeni huko Zanzibar linachojulikana kama Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI). Kina kila sababu ya kuitwa kituo cha lugha kwani kinafundisha lugha za kigeni kama Kiarabu, Kiingereza , Kijerumani na Kifaransa katika ngazi ya Diploma kikiwaandaa wataalamu wa ngazi ya kati. Pia kinafundisha Kiswahili kwa wageni wanaokuja hapa nchini ama kufanya kazi au kujifunza Kiswahili ili baadaye wakafundishe katika nchi zao.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itambue kuwapo kwa kituo hiki na kipatiwe fedha za kutosha. Yanatakiwa maboresho ya hali ya juu ili kukiwezesha kituo hiki kikidhi vigezo vya kimataifa. Kwa mfano wanatakiwa wahadhiri wenye digrii za uzamili na uzamivu katika lugha nilizotaja hapo juu pamoja na vifaa vya kufundishia kama vitabu, video na kanda zake na vilevile maabara kisasa za lugha kwa ajili ya kufundishia fonetiki, fonolojia na sintaksia.
Kituo hiki kitawavutia wanafunzi wengi kutoka nje na taifa litapata fursa nzuri ya kujiongezea kipato pamoja na kuwaandaa Watanzania ujipatia ajira nchi za nje.
Aidha matangazo ya kutosha kwa vyuo vyetu vinavyo funza kiswahili kama Udsm/Tataki yanapaswa kupewa kipaumbele
Mwandishi Wa makala haya ni mtaalamu Wa lugha , sanaa pamoja na kiswahili na tehama
info.masshele@gmail.com
Aidha matangazo ya kutosha kwa vyuo vyetu vinavyo funza kiswahili kama Udsm/Tataki yanapaswa kupewa kipaumbele
Mwandishi Wa makala haya ni mtaalamu Wa lugha , sanaa pamoja na kiswahili na tehama
info.masshele@gmail.com
Comments
Post a Comment