Wanafunzi 56,132 Heslb wapata mkopo wa elimu ya juu awamu ya kwanza


  • “Niwaombe wale ambao hawataona  majina yao katika awamu hii ya kwanza waendelee kuwa wavumilivu na kuwa na subira kwani kuna ‘batch’ awamu nyingine ambazo zitakuja,” ameongeza  MariaIdadi hiyo ni wale waliokidhi vigezo vilivyoainishwa na Heslb.
  • Sh159.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi hao.


Dar es Salaam. Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (Heslb) imetangaza orodha ya kwanza ya majina ya  wanafunzi 56,132 wa mwaka wa kwanza waliopata mkopo wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2023/2024.

Mikopo hiyo yenye thamani ya Sh159.7 bilioni itawawezesha wanafunzi hao kugharamia ada za masomo pamoja na fedha za kujikimu katika awamu ya kwanza ya masomo inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.

Fedha hizo zilizotumika ni asilimia 21.8  ya Sh731 bilioni zilizoidhinishwa na Serikali ya awamu ya sita kunufaisha wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa ya kupata mkopo huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo Abdul Razaq Badru aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 20, 2023  amesema kuwa wanafunzi hao ni wale waliokidhi vigezo walivyoviweka wakati wa kuomba mikopo hiyo.

“Orodha hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo kimoja,” amesema Badru.


Kati ya idadi ya wanufaika hao, wa kiume ni 32,264 sawa na asilimia 57 na wa kike ni 23,868 ambao ni sawa na asilimia 43.

Kwa mujibu wa Badru,uwiano wa kijinsia katika wanufaika wa mikopo katika awamu hii umeimarika kulinganisha na awamu zilizopita.

“Huko tulipotoka wanufaika wakiume walikuwa wengi zaidi tunaongelea asilimia 80 asilimia 90 lakini siku za hivi karibuni uwiano unaendelea kuimarika,” ameongeza Badru.

Wanafunzi tumieni fedha vizuri

Rais wa Shirikisho la wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania (Tahliso), Maria John amewataka wanafunzi waliopata mikopo hiyo kuitumia vizuri ili iwawezeshe kufanya vizuri katika masomo yao.

“Niwaombe hao wanufaika watakaopata fedha hizo wazitumie katika malengo mahususi, kwamba  wamepewa katika kutimiza malengo ya elimu na si vinginevyo,” amesema Maria

Aidha, kiongozi huyo amewataka wanafunzi ambao hawataona majina yao katika awamu hii ya kwanza kuwa wavumilivu na kusubiri awamu nyingine zitakazotoka hivi karibuni.

Credit Nukta