Google yashtakiwa kwa kusababisha kifo
Kampuni ya Google imeshtakiwa na Familia ya Philip Paxson ambaye kwa kufuatia ramani za Google aliendesha gari kwenye daraja lililoanguka na kupoteza maisha.
Paxson alizama Septemba mwaka jana baada ya gari yake aina Jeep Gladiator kutumbukia katika daraja huko North Carolina,nchini Marekani.
Alikuwa akirudi nyumbani kutoka kwenye sherehe ya kumbukizi ya miaka 9 ya kuzaliwa kwa binti yake.
Eneo alilokuwa akipita lilikuwa geni kwake ndipo ramani za Google zilipomuelekeza kuvuka daraja ambalo lilikuwa limeporomoka.
Familia hiyo inaituhumu Google kwa uzembe, na kudai kuwa kwa takribani miaka mitano Kampuni hiyo ilikuwa ikipewa taarifa na watu kadhaa kuwa daraja hilo limeanguka na waliitaka irekebishe taarifa za ruti.
Hata hivyo Kampuni hiyo haikurekebisha taarifa za ruti hiyo kwenye mfumo wa ramani.
Kesi hiyo pia imezitaja kampuni kadhaa binafsi zilizokuwa na jukumu la kusimamia daraja na eneo hilo.
Polisi walioukuta mwili wa mwanaume huyo kwenye gari yake iliyokuwa imepinduka na kuzama kiasi walisema hakukuwa na vizingiti au alama yoyote ya kutahadharisha watu kutopita kwenye eneo hilo
Comments
Post a Comment