Baada ya miaka mingi ya kupungua, ugonjwa wa kipindupindu sasa unarejea kwa kishindo ukilenga nchi zilizo hatarini zaidi duniani.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na lile la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) yanasema nchi nyingi zaidi hivi sasa zinakabiliwa na milipuko, huku idadi ya wagonjwa ikiripotiwa ikiwa ni kubwa kuliko miaka 10 iliyopita.

“Janga la kipindupindu linaua maskini zaidi mbele ya macho yetu,” amesema Jérôme Pfaffmann Zambruni, Mkuu wa kitengo cha UNICEF kinachohusika na Dharura ya Afya Umma. 

Takwimu za WHO zinaeleza kuwa hadi Mei mwaka jana, nchi 15 ziliripoti kuwa na wagonjwa wa kipindupindu, lakini hadi katikati ya mwezi huu wa Mei, tayari kuna nchi 24 zinazoripoti kuwa na ugonjwa huo idadi inaweza kuongezeka zaidi.

“Licha ya maendeleo yaliyopatikana miongo iliyopita katika mbinu za kudhibiti kipindupindu bado tuko hatarini kurudi nyuma,” amesema Henry Gray, Meneja wa WHO akihusika na hatua dhidi ya kipindupindu duniani. 

WHO inakadiria kuwa watu bilioni moja katika nchi 43 wako hatarini kupata kipindupindu huku watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wakiwa hatarini zaidi. 

Yana Duka ni mmoja wa waathirika 35 wa cholera katika kituo cha afya cha muda mfupi kambini Muna nchini Nigeria. Alipoteza mimba yake baada ya kuwa mgonjwa. Picha | UNFPA/Anne Wittenberg

Afrika hali si shwari

Huko Malawi na Nigeria, idadi ya vifo kutokana na kipindupindu ni kubwa ikifikia asilimia tatu mwaka huu, juu ya kiwango kinachokubalika cha asilimia moja. 

Ukanda wa Kusini-mashariki kwa Afrika ndio umeathiriwa zaidi ambako maambukizi yanasambaa Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, wameeleza wataalam hao wa UN.

Mwenendo huu umekuja baada ya uharibifu uliofanywa na kimbunga Freddy Februari na Machi mwaka huu na kuacha watu 800,000 nchini Malawi na Msumbiji bila makazi yao huku huduma za afya zikiwa zimevurugika. 

Jamii hizi ziko hatarini kupata kipindupindu, ugonjwa unaozuilika ambao inashamiri kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa na mafuriko. 


Vipi kuhusu chanjo?

Ijapokuwa chanjo dhidi ya kipindupindu tayari inapatikana na inatumika, bado kiwango chake hakijakidhi mahitaji yanayoongezeka kila uchao. 

Kwa mujibu wa WHO, ombi la dozi milioni 18 za chanjo ya kipindupindu limekuwa likiwasilishwa kila mwaka lakini zinazopatikana ni chanzo milioni 8 pekee. 

“Ongezeko la uzalishaji wa chanjo si suala la usiku mmoja, lakini hatutakuwa na dozi za kutosha iwapo mwelekeo wa sasa wa maambukizi utaendelea. 

“Chanjo ni mbinu lakini sio jawabu kamilifu. Uwekezaji wa muda mrefu kwenye huduma za maji safi na kujisafi ndio kipaumbele.” ” amesema Gray.




Nini kifanyike?

Ili kukabili kitisho cha kipindupindu, WHO imezindua mpango wa kimkakati wa miezi 12  wa kujenga uwezo wa kujiandaa, kuchukua hatua na tayari  ukiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 160 (Sh376.9 bilioni), sambamba na wito kwa hatua uliotolewa na UNICEF ukihitaji dola milioni 480 sawa na Sh1.13 trilioni.

Mpango huo wa pamoja wa UNICEF na WHO utahusisha nchi 40 zilizo kwenye janga la kipindupindu.

 Hatua zitakazohusika ni uratibu, usimamizi wa maambukizi na kuzuia maambukizi pamoja na chanjo, matibabu, huduma za maji safi na salama na kujisafi

Soma zaidi nukta africa