Takriban wahamiaji 59, wakiwemo watoto 12, wamefariki dunia na makumi ya wengine wanahofiwa kutoweka baada ya boti yao kuzama kwenye bahari ya kusini mwa Italia.

Boti hiyo ilizama ilipokuwa ikijaribu kutia nanga karibu na mji wa pwani wa Crotone katika eneo la Calabria.

Walionusurika walisema angalau watu 150 walikuwa ndani.

Wengi wao walikuwa wakikimbia hali ngumu, rais wa Italia alisema.

Waziri wa Mambo ya Ndani Matteo Piantedosi, ambaye alitembelea eneo la tukio, alisema hadi watu 30 bado hawajulikani walipo.

Mtoto anayedhaniwa kuwa na umri wa miezi michache tu alikuwa miongoni mwa waliofariki, kulingana na shirika la habari la Ansa la Italia.

Miili iliopolewa kutoka ufukweni katika eneo la mapumziko lililo karibu la bahari.

Walinzi wa pwani walisema watu 80 wamepatikana wakiwa hai, “ikiwa ni pamoja na wengine ambao walifanikiwa kufika ufukweni baada ya kuzama”.

Idadi kamili ya watu waliokuwa kwenye boti hiyo ilipovunjika haijabainika – waokoaji waliliambia shirika la habari la AFP kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba “zaidi ya watu 200”, ambayo itamaanisha zaidi ya watu 60 hawajulikani waliko.

Boti hiyo iliyosafiri kutoka Uturuki siku kadhaa zilizopita, ilikuwa imebeba abiria kutoka Afghanistan, Pakistan, Somalia na Iran.

Idadi kubwa ya watu wanaokimbia migogoro au umaskini huvuka kutoka Afrika hadi Italia kila mwaka.