Editors Choice

3/recent/post-list

Necta yafuta orodha ya 10 bora kidato cha nne Tanzania


  •  

Dar es Salaam. Wazazi na viongozi wa shule waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuona iwapo watoto wao wameingia katika orodha ya dhahabu ya 10 bora katika mitihani ya taifa sasa watasubiri sana jambo hilo baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutangaza kufuta rasmi utaratibu huo likisema “hauna tija”.

Uamuzi wa Necta kufuta utaratibu huo uliokuwa ukishindanisha wanafunzi, shule, wilaya na mikoa kupitia orodha ya 10 bora huenda ukapeleka maumivu kwa baadhi ya viongozi waliokuwa wanatumia takwimu hizo kuvuta zaidi wanafunzi au kuonyesha ubora wa utendaji kazi wao.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta Athuman Amas amewaambia wanahabari sasa baraza hilo limeuondoa utaratibu huo ambao hata wanahabari waliokuwa ndani ya chumba cha mikutano walikuwa wakisubiri kwa hamu kujua nani ni nani.

“Tumeondoa utaratibu wa kutangaza shule 10 bora au watahiniwa 10 bora kwa sababu hauna tija, tunawafananisha watu ambao wamefanya mtihani sawa lakini mazingira tofauti,” amesema Amas huku baadhi ya wanahabari wakionekana kukubaliana na uamuzi huo.

Kwa miongo kadhaa sasa Necta imekuwa ikishindanisha shule 10 bora kitaifa na wanafunzi 10 bora huku yule wa kwanza maarufu kama “Tanzania One” (TO) akipewa heshima zaidi.

Baadhi ya shule hizo hasa binafsi na za mashirika ya dini zimekuwa zikitumia orodha hiyo kwenye matangazo ya biashara kuvutia wazazi kupeleka watoto kwenye taasisi zao huku baadhi zikihusisha mchujo mkali.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amas akiwasilisha matokeo ya kidato cha nne na mtihani wa maarifa (QT) mwaka 2022 kwa wanahabari jijini Dar es Salaam Januari 29, 2023.

"Unamtaja huyo mtu kwamba ameongoza katika kundi ambalo pamoja na kuwa wamefanya mtihani mmoja lakini hawakusoma katika mazingira yanayofanana, wakati mwingine niseme tu kutangaza shule ya kwanza, inawezekana kama mheshimiwa mwandishi ulikuwa na shule, huenda tulikuwa tunakufanyia matangazo, huenda nasema," amesema Amas huku wanahabari wakiangua kicheko.


Mara baada ya kutangazwa uamuzi huo, baadhi ya wadau wa elimu wamefurahia uamuzi huo wa Necta huku wengine wakishauri kuwa ili orodha hiyo iwe ina maana Serikali inapaswa kuboresha mazingira ya kijifunzia katika shule zote.  

Post a Comment

0 Comments