SIMBA SC inatakiwa kutoa dola 100,000 (sawa na Sh 232,385,000 za Kitanzania) ili kufanikisha usajili wa winga wa zamani wa TP Mazembe, Isaac Tshibangu ambaye kwa sasa anakipiga Bandırmaspor ya Uturuki.

Winga huyo ni kati ya wachezaji waliokuwepo katika mipango ya kusajiliwa na Simba katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa Desemba 16, 2022.

Simba imepanga kukifanyia maboresho kikosi chao katika baadhi ya maeneo ikiwemo winga baada ya kumkosa mchezaji mzuri wa kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, winga huyo anasajiliwa kuja kuchukua nafasi ya Mnigeria, Nelson Okwa.

Bosi huyo alisema kuwa, winga huyo Mkongomani yupo katika mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kukamilisha dili lake la kutua Simba baada ya kuona ugumu wa kumrudisha Luis Miqquisone raia wa Msumbuji.

Aliongeza kuwa, winga huyo kwa sasa sokoni thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni 200, hivyo Simba itatakiwa itoe kitita hicho kufanikisha usajili wake.

“Wapo wachezaji kadhaa tuliokuwa nao katika mazungumzo ambayo muda wowote yatakamilika na kuwasajili kabla ya dirisha kufungwa.

“Uongozi umepanga kumsajili winga mwenye kiwango bora atakayekuja kuingia moja kwa moja katka kikosi cha kwanza cha Mgunda (Juma).

“Kati ya hao yupo Tshibangu ambaye ni kati ya viungo bora hivi sasa, hivyo kama mazungumzo yatakwenda vizuri, basi tutamsajili kwa atakayekuja kuchukua nafasi ya Luis ambaye tumeshindwa kufikia muafaka mzuri,” alisema bosi huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alizungumzia usajili huo na kusema: “Tumepanga kumaliza usajili wa dirisha dogo haraka sana kabla haujafungwa.

“Tumepanga kufanya usajili mkubwa na wa kisasa wenye faida katika timu yetu, hivyo wapo baadhi ya wachezaji tuliokuwa nao katika mazungumzo kama yakienda sawa, basi tutawatangaza.”