MKAZI wa Kitanzini Iringa, Atka Kivenule (25) aliyekuwa na ujauzito wa miezi miwili, amebakwa na kuuawa kwa kukabwa koo katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia Jumapili nyumbani kwake mjini Iringa. 

-

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini majukumu mengine ya kikazi hayakumwezesha kuzungumza na wanahabari hadi habari hii inakwenda mitamboni. 

-

Mmoja wa maofisa wa polisi Iringa ambaye si msemaji wa jeshi hilo, alimtaja kijana mfanyabiashara wa viatu vya mtumba, Mohamed Njali maarufu kama Muddy amekamatwa akihusishwa na tukio hilo. 

-

Muddy anayeishi nyumba ya pili kutoka nyumba ya marehemu, alikamatwa akiwa na simu ya marehemu, suti ya mume wa marehemu na pasi anavyodaiwa kuvichukua baada ya kutekeleza unyama huo. 

-

Mume wa marehemu, Adeline Michael Kileo alisema tukio hilo lilitekelezwa wakati yeye akiwa baa ya jirani na nyumbani kwao Kitanzini mjini Iringa akitazama pambano la ndondi la Twaha Kassim ‘Kiduku’ na bondia kutoka Misri lililofanyika mwishoni mwa wiki Mtwara.

-

Kileo alisema mkewe aliyekuwa na ujauzito wa miezi miwili, alifanyiwa unyama huo baada ya mtuhumiwa huyo kuvamia nyumbani kwake yeye akiwa hajarudi. Alisema wakati akifanya uvamizi huo, mkewe alikuwa chumbani na mtoto wao mdogo wa kike mwenye umri wa miaka mitano aliyejificha huku akishuhudia mama yake akibakwa. 

-

“Mtoto alijificha wakati mtuhumiwa huyo akivunja mlango na alishuhudia mama yake akipigwa kabla ya kufanyiwa unyama mwingine na baadae kupoteza maisha,” alieleza Kileo.