Mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu Mzumbe, Nicas Lubangu (22) mkazi wa Mzumbe mkoani Morogoro amefariki dunia baada ya kuangukiwa na jiwe kichwani lililoporomoka kutoka kwenye maporomoko ya Mlima wa Uluguru walipokuwa wakifanya Utalii katika maeneo hayo na wenzake.


Kwa mujibu wa Kamishna Mwandamizi wa polisi, Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim tukio hilo lilitokea Aprili 26, majira ya saa 6 mchana katika maeneo ya maporomoko ya Mlima wa Uluguru kwenye kijiji cha Lagure, kata ya Mlimani Manispaa na Wilaya ya Morogoro.


Amesema marehemu huyo ambaye alikuwa Mwanachuo wa Shahada ya pili ya Biashara katika Chuo cha Mzumbe akiwa na wenzake 12 walikwenda kutembelea maeneo ya maporomoko kwa ajili ya utalii ambapo akiwa anapiga picha jiwe liliporomoka kutoka mlimani na kumpiga kichwani sehemu ya sikio upande wa kushoto na kumsababishia jeraha.


Kamanda Musilim amesema kutokana na jeraha hilo wanachuo wenzake walimchukua na kumkimbiza hospitali kwa matibabu lakini wakiwa njiani alifariki dunia na kwamba mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi kwa ajili ya mazishi.


Hata hivyo, amewaasa watu wanaopenda kufanya utalii katika maporomoko hayo  kuchukua tahadhari.