TAFSIRI NA UKALIMANI,

ATHARI ZA TAFSIRI KATIKA TAALUMA YA UKALIMANI

Na,

Hashim Juma.

                                                  hashimjuma255@gmail.com

     Ikisiri

Tafsiri na ukalimani hizi ni taaluma zinazojishughulisha na uhawilishaji wa mawazo/maarifa kutoka lugha moja (lugha chanzi/chasili) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa) (Mpemba, 2013). Licha ya mfanano huo Mpemba (2013) anasisitiza kwamba hizi ni taaluma ambazo zinamawanda tofauti. Kati ya taaluma hizi mbili taaluma ya ukalimani inaelezwa kuwa ni taaluma ambayo imekuwapo tangu hata kabla ya ugunduzi wa maandishi (taz: Pochhacker, 2004 na 2009). Licha ya taaluma ya ukalimani kuwa kongwe kuliko tafsiri, taaluma ya tafsiri imeiathiri kwa kiwango kikubwa taaluma ya ukalimani. Makala haya yamekusudia kueleza athari hizo na sababu zake. Makala haya yataanza kwa kueleza fasili ya taaluma hizi, kisha katika kiini cha makala haya tumeeleza athari za tafsiri katika taaluma ya ukalimani na sababu zake na mwisho ni hitimisho.

Utangulizi

Katika sehemu hii tumetarajia kueleza maana ya tafsiri kwa mujibu ya wataalamu anuwai. Catford (1965) na Newmark (1988) wanaeleza kuwa tafsiri ni kama mchakato wa uhamishaji wa ujumbe kutoka lugha chanzi na kuumba ujumbe unaolingana na huo katika lugha lengwa. Mtazamo wa wataalamu hawa umejikita hasa katika kutimiza kuwepo kwa ulinganifu wa maana na ujumbe uliopo kwenye matini chanzi na ule wa matini lengwa. Hii inamaanisha mfasiri anapokabiliwa na shughuli ya kutafsiri hana budi kutafuta visawe linganifu ambavyo ni sawa na vile vya matini chanzi na maana ya ujumbe.

Mtazamo huu, kwa kweli ni mgumu kutekelezwa na mfasiri kwani lugha hutofautiana na usawiri ulimwengu kwa namna tofauti na lugha nyingine. Aidha, kwa kutumia mtazamo huu si rahisi kuwepo kwa tafsiri za kiutamaduni kwa kuwa mara nyingi visawe vya kiutamaduni fulani huwa vya pekee na si rahisi kuvikuta katika utamaduni mwingine. Tazama mfano 1 kwa ufafanuzi zaidi

Summer-Kiangazi (lakini joto la kiangazi ni kali zaidi ya lile la summer)

Autumn-vuli winter-kipupwe lakini baridi ya winter ni kali zaidi ya ile ya kipupwe.

Chanzo: Mwansoko na wenzake (2015)

Licha ya Kiswahili kubainisha misimu minne yaani kiangazi, vuli, masika na kipupwe. Na Kiingereza kubainisha minne ambayo ni summer, autumn, winter na spring lakini misimu hii haiwezi kushabihiana. Kadhalika si rahisi kupata visawe vya dhana ya masika na spring. Hii ni kwa sababu Kiswahili huzungumzwa kwenye nchi joto (ya kitropiki) ilhali kiingereza huzungumzwa kwenye nchi ya baridi na msimu mfupi sana wa joto la wastani. Kwa msingi huo ni vigumu kupata visawe linganifu baina ya lugha chanzi na lugha lengwa.

Aidha, Bassnet (2013) anaeleza kuwa tafsiri ni ubadilishaji wa ujumbe ilio katika lugha moja na kuweka ujumbe unaolingana katika lugha nyingine, ujumbe huo unaweza kuwa katika maandishi au mazungumzo. Kuhusu utata wa kulingana kwa ujumbe katika lugha chanzi na lengwa kumeshajadiliwa, hapa tunaona mtaalamu huyu anaongeza sifa ya ujumbe unaoweza kutafsiriwa kwamba unaweza kuwa katika maandishi au mazungumzo. Kwa muda mrefu suala la ujumbe unaotafsiriwa kwamba sharti uwe katika mandishi limeshikiliwa kwa muda mrefu (taz: Mwansoko na wenzake 2015). Kwa hiyo, kwa kuongeza suala la mazungumzo fasili hii imepiga hatua licha ya hivyo,bado fasili nyingi hazielezi ubainifu wa tafsiri.

Kwa hiyo makala haya yanachukulia kuwa tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo, taarifa au mawazo yaliyoko kwenye maandishi au yaliyorekodiwa na kwenda kwenye lugha nyingine bila kubanwa na upapo kwa papo. Fasili hii inamaana kuwa zoezi la kutafsiri halibanwi na kufanyika papo kwa papo. Zoezi hili hufanyika kwa muda mrefu na hujumuisha hatua kadhaa ambazo si rahisi kuzifanya papo kwa papo. Kwa mfano hatua ya kwanza ni (i) maandalizi (ii)uchambuzi (iii) uhawilishaji (iv) usawidi wa rasimu ya kwanza ya tafsiri (v) udurusu wa rasimu ya kwanza ya tafsiri (vi) kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu wa pili (ili kurekebisha zaidi matini ya tafsiri na usawidi wa rasimu ya mwisho ya tafsiri) (Taz: Mwansoko na wenzake, 2015)

Kwa upande wa ukalimani, wataalamu mbalimbali wametoa mitizamo yao kama ifuatavyo; Kade (1968) kama anavyonukuliwa na Pochhacker (2004 na 2009) anaeleza ukalimani ni namna ya tafsiri ambapo ufafanuzi wa kwanza na wa mwisho wa lugha nyingine hutolewa kwa kuzingatia uhawilishaji wa mara moja wa usemi wa lugha chanzi. Fasili hii ya Pochhacker (2004 na 2009) ni nzuri kwa kuwa inadokeza kipengele cha upapo kwa papo ambacho ni kama mojawapo ya nduni bainifu ya taaluma hii ya ukalimani. Zoezi la kukalimani si sawa na tafsiri kwani tafsiri hupitia hatua kadhaa (taz: Mwansoko na wenzake 2015) lakini kwa upande wa ukalimani zoezi la uhawilishaji hufanyika papo kwa papo. 

Pamoja na jambo la msingi linalodokezwa na fasili hii kuchukulia taaluma ya ukalimani kama aina ya tafsiri kuna kanganya kwani historia inaonesha ukalimani ni mkongwe zaidi ukilinganisha na tafsiri (taz: Beker na Saldanha 2000) Sasa inakuaje tena aina ya tafsiri, hili swali linaibua upungufu katika fasili hii. Vilevile, fasili haiweki wazi ujumbe unaohawilisha ama upo katika ishara, mazungumzo au maandishi, jambo ambalo pia ni la msingi katika fasili ya ukalimani.

Baada ya kueleza usuli kuhusu taaluma hizi, hebu sasa tutazame athari za tafsiri katika taaaluma ya ukalimani. Maana ya athari katika makala haya tumechukulia kuwa ni mawanda ya ukalimani ambayo yamekuwa yanachukuliwa kama mawanda ya tafsiri.

Athari za Tafsiri katika Taaluma ya Ukalimani

Sehemu hii imeeleza athari za tafsiri katika taaluma ya ukalimani. Zifuatazo ni athari za tafsiri katika ukalimani

2.1 Ukalimani kama Aina ya Tafsiri

Licha ya kwamba taaluma ya ukalimani ni taaluma kongwe, kuna wataalamu wanaona kwamba ukalimani ni aina mojawapo ya tafsiri. Kwa hali halisi, walau ingekuwa inachukuliwa kwamba tafsiri ni aina mojawapo kwa kuwa taaluma ya ukalimani ni kongwe. Wataalamu wanaona ni aina ya tafsiri. Kade (1968) kama anavyonukuliwa na Pochhacker (2004 na 2009) anaongeza kuwa ukalimani ni namna ya tafsiri ambapo ufafanuzi wa kwanza na wa mwisho kwa lugha nyingine hutolewa kwa kuzingatia uwasilishaji wa mara moja wa usemi wa lugha chanzi. Pochhacker (keshatajwa) anafafanua zaidi kwamba anatumia neno tafsiri linaloanza na herufi kubwa kwa maana pana, na anaeleza kwamba fasili yake inadokeza kipengele cha upapo kwa papo.

Ukitazama fasili ya Kade (1968) na Pochhacker (2004 na 2009) yanaeleza mambo yote yanayohusu ukalimani. Mathalani sifa ya upapo kwa papo na uwasilishaji wa mara moja wa usemi wa lugha chanzi. Sifa hizi ni tofauti kabisa na zile za tafsiri mfano tafsiri haina uwasilishaji wa papo kwa papo wa ujumbe kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa kwani hupitia mchakato au hatua mbalimbali kwa mfano, (i) maandalizi (mfasiri huisoma matini chanzi mara kadhaa ili kuelewa ujumbe wake, kubaini mtindo wa matini na kuziwekea alama maalumu sehemu za matini zenye utata  au zisizoeleweka vizuri (Mwansoko na wenzake, 2015). 

Mambo hayo yanadhihirisha kwamba tafsiri matini chanzi huwasilishwa mara kadhaa tofauti na ukalimani. Vilevile, sifa ya upapo kwa papo haipo kwenye tafsiri kwani baada ya uhawilishaji wa mawazo au ujumbe haufanywi papo hapo hupitia hatua zingine. Kwa msingi huu basi, hapakuwa na haja yoyote ya kuichukulia ukalimani kama aina au namna ya tafsiri, hii inaonesha ni athari za taaluma ya tafsiri kwenye taaluma ya ukalimani ambapo mawanda ya ukalimani yanaonekana kuwa ndani ya tafsiri jambo ambalo si sawa. 

2.2 Shughuli ya Kukalimani kuiita shughuli ya Kutafsiri

                   Athari ya inaanzia kwenye kukanganya kwa istilahi yenyewe ya tafsiri na ukalimani. Aidha,          Schafner (2004) anaeleza kwamba kukanganya kwa istilahi ya ukalimani na tafsiri kunaashiria kwamba licha ya kuwa taaluma hizi ni sehemu za maisha ya kawaida ya binadamu watu wengi bado hawajui umahususi wa shughuli ya mfasiri na mkalimani. Katika makala haya tunachukulia kwamba hii ni athari ya tafsiri kwenye taaluma ya ukalimani kwa kuwa si rahisi kukuta kwamba watu wamemuita mtafsiri mkalimani ila si ajabu kukuta mkalimani anaitwa Mtafsiri. Athari hii ilionekana katika vyombo vya habari kadhaa na mitandao ya kijamii mara baada ya mkalimani, aliyekuwa anakalimani hotoba ya Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini katika shughuli ya kuuga mwili wa Hayati Dkt Magufuli pale Dodoma. Hebu Tazama mfano ufuatao

Mkalimani (mtafsiri) Aliyetafsiri uongo huyu hapa. Chanzo: Sun set video

Mfahamu mkalimani aliyetrendi kwa kutafsiri tofauti, aanika ukweli wa kilichotokea uwanjani Dodoma. Chanzo: Dozen selection

Mazito yamkuta mkalimani aliyetafsiri uongo kwenye msiba wa Magufuli Dodoma. Chanzo: Drama Tv

Ukichunguza vichwa vya habari hivyo ambayo vinapatikana katika mtandao wa Youtube utaona jinsi kulivyo na athari ya tafsiri kiasi cha watu kudhani shughuli ya kubadilisha ujumbe ulioko katika lugha fulani kwenda lugha nyingine ni tafsiri. Mfano katika (a) hapo juu mwandishi anachukulia kwamba jina lake jingine ni mtafsiri jambo ambalo linatatizana na, katika mfano (b) mwandishi anachukulia kuwa mkalimani hufanya kazi ya kutafsiri. Aidha, katika mfano (c) tunaona kwamba mkalimani anachukuliwa kama ni mtu anayefanya kazi ya kutafsiri, ukweli ni kwamba shughuli ya ukalimani na kutafsiri ni shughuli mbili tofauti licha ya kwamba zinahusiana. (taz: Nolan, 2005). Baada ya kueleza athari za tafsiri kwenye taaluma ya ukalimani, katika sehemu inayofuata tumeeleza sababu zake kwa nini athari hizo zinatokea katika taaluma ya ukalimani

Chanzo cha Athari za Tafsiri katika Taaluma ya Ukalimani

Athari za tafsiri katika taaluma ya ukalimani hazielekei kutokea bahati mbaya bali zina chanzo chake. Sehemu hii imejadili chanzo hicho ni kipi hasa

Mosi, Tafsiri ni maarufu kuliko ukalimani. Taaluma ya tafsiri ni taaluma inayojulikana ukilinganisha na taaluma ya ukalimani. Kwa msingi huu unafanya taaluma hii kuathiri taaluma ya ukalimani. Kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam toka (2012) ni mwanafunzi mmoja tu ambaye ni Mwituka (2012) aliyeandika tasnifu yake kuhusu ukalimani ilhali kwa upande wa tasnifu za tafsiri zipo nyingi zilizofanywa katika uga wa tafsiri mathalani Jilala (2014) na Ngesu (2021) hao ni baadhi tu. Kadhalika, majalida ya Kiswahili, Mulika na Kioo cha Lugha, jalida la Kiswahili ni mwandishi mmoja hasa aliyejikita kuandika kuhusu ukalimani ambaye ni Mpemba ilhali kwa upande wa tafsiri wapo waandishi kadhaa walioandika kuhusu tafsiri mfano Malangwa na Jilala. Kutokana na kujulikana huku ndiko kunafanya taaluma ya tafsiri kuathiri taaluma ya ukalimani kwani makala, tasnifu zinazohusu ukalimani ni chache ukilinganisha na kwenye upande wa tafsiri. 

                         Pili, kutojua umahususi wa taaluma ya tafsiri na ukalimani. Hili linashadadiwa na Schafner (2004) anapoeleza kuwa kukanganywa kwa istilahi za ukalimani na tafsiri kunaashiria kuwa licha ya ukalimani na tafsiri kuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya binadamu watu bado hawajui umahususi wa shughuli ya mkalimani na mfasiri. kwa maelezo haya inaelekea kwamba watu wengi pia wanajua kuna taaluma ya ukalimani na tafsiri lakini hawajui hasa mawanda ya taaluma hizi ni yepi. Mathalani mfano uliotolewa katika (2.2). Hivyo basi, inaonekana kwamba watu wengi hawafahamu mipaka ya taaluma hizi mbili na kupelekea taaluma ya tafsiri kutwishwa mzigo mkubwa kwani ukalimani huonekana kama aina ya tafsiri ambapo kwenye makala hii ndiyo tumeita athari za tafsiri kwenye ukalimani. Aidha, kuhusu mipaka ya taaluma hizi (Taz: Nolan, 2004: Mpemba, 2013).

                  4.0 Hitimisho 

Makala haya yanejadili athari za tafsiri katika taaluma ya ukalimani. Athari zilizojadiliwa ni kuchukulia taaluma ya ukalimani kama aina ya tafsiri na shughuli ya kukalimani kuiita shughuli ya kutafsiri. Kadhalika katika makala haya yamejadili chanzo cha athari hizo. Chanzo kilichojadiliwa ni; umaarufu wa tafsiri ukilinganisha na ukalimani na kutojua umahususi wa taaluma hizi mbili yaani tafsiri na ukalimani, ambapo inaonekana tafsiri ndiyo inapewa mawanda mapana zaidi inapotokea hivyo ambapo tumeita athari za tafsiri katika taaluma ya ukalimani. Aidha, tumependekeza taaluma zote hizi zitiliwe maanani katika taasisi mbalimbali kwani zina uzito sawa kutokana na mwingiliano wa tamaduni zenye lugha tofauti unaozidi kuongezeka kila uchao.


                                                     

                                                                MAREJELEO 

Beker, M na Saldanha, G. (2008) Routledge Encylopidia of Translation Studies. New York. Routledge.

Bassnet,S (2013) Translating Studies. London Routledge: Methuen& Co Ltd.

Catford, J.C. (1965) A Linguistic Theory of Transalation (Language and Language Learning). London: Oxford University Press.

Jilala, H. (2014) “Athari za Kiutamaduni katika Kutafsiri: Mifano kutoka Matini za Kitalii katika makumbusho za Tanzania”. Tasnifu ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo .Kikuu cha Dar es Salaam.

Mpemba, T. (2013) “Hali ya Taaaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho” katika jalida la Kiswahili. Juzuu no 76: 111-139.

Mwansoko, H.J.M. Mekacha, R.D.K. Masoko, D.L.W. Mtesigwa, P.C.K. (2013) Kitangulizi 

                  cha Tafsiri Nadharia na Mbinu. Dar es salam: TUKI.

Mwituka, D.P. (2012) “Matatizo ya Kiutendaji Ukalimani wa Mikutano”. Tasnifu ya Umahiiri      (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

NewMark, P. (1988) A Text of Translation. New York: Prentice Hall.

Nida, E.A. (1964) Toward a science of Transalation with Special Reference to Principle Involve in Bible Translating-Leiden: Brill.

Nida, E.A. na Taber, C.R. (1969) The Theory of Practice of Translation. Leiden: Published for the United Bible Societies.

Ngesu, S.N.M (2021) “Tafsiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni Nchini Uganda”. Tasnifu ya Uzamivu (haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nolan, J. (2005) Interpretation: Technique and Exercise. Toronto. Multilingual Matters Ltd.

Pochhacker, F. (2004) Introducing Interpreting Studies. New York: Routledge.

Pochhacker, F. (2009) “Interpreting as Mediation” Katika Valero-Garces. Carmen na Martin Crossing Borders in Community Interpreting: Definitions and Dilemmas Amsterdam: John Benjamin Publishing Company.

Schaffner, C. (2004) “Researching Translation and Interpreting” Katika Translation Research and Interpreting Research: Traditions, Gaps and Synergies. Toronto: Multilingual Matters Ltd, Kur 1-9.