Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato nne mwaka 2021 na kuzitaja shule 10 zilizofanya vizuri huku Shule ya Sekondari ya Kemebos ya mkoani Kagera ikishika nafasi ya kwanza kitaifa.

Kemebos imepanda kutoka nafasi ya nne iliyoshika katika matokeo ya mwaka juzi na kuishusha Shule ya Sekondari ya St Francis ya mkoani Mbeya hadi katika nafasi ya pili.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa  leo (Januari 15, 2022) na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amezitaja shule nyingine nane  zilizofanya vizuri zaidi katika matokeo hayo kuwa ni Waja Boys ya mkoani Geita iliyoshika nafasi ya tatu.

Shule ya Sekondari Bright Future Girls ya Dar es Salaam imepenya katika nafasi ya nne,  Bethel Girls (Iringa) katika nafasi ya tano na Maua Seminary mkoani Kilimanjaro ikishikilia nafasi ya sita.


Feza Boys ya jijini Dar es Salaam yenyewe imepigana vikali na kujitwaliwa Nafasi ya saba, Precious Blood (Arusha) katika nafasi ya nane na Feza Girls ya Dar es Salaam imefakiniwa kushika nafasi ya tisa katika orodha hiyo ya dhahabu.

Shule ya Sekondari ya Mzumbe ya mkoani Morogoro imefunga 10 bora kitaifa ikiwa ndiyo shule pekee ya Serikali iliyofanikiwa kuingia katika orodha hiyo. Katika matokeo ya mwaka 2020, Mzumbe ilishika nafasi ya 20

Uchambuzi zaidi wa matokeo hayo unaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanikiwa kuingiza shule tatu huku mikoa iliyobaki ikiingiza shule moja moja