Dar es Salaam. Mwaka umeanza vizuri kwa binti Consolata Prosper baada ya kutangazwa kuwa mwanafunzi bora wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021 kutoka Shule ya Sekondari ya St Francis Girls iliyopo mkoani Mbeya. 

Katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa leo Januari 15, 2022 na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Prosper ndiyo mwanafunzi aliyefaulu vizuri zaidi kati ya wanafunzi 483,820 waliofanya mtihani huo mwishoni mwa mwaka jana. 

Binti huyo mwenye miaka 16  ameuambia mtandao huu kuwa moja ya silaha zilizomwezesha kuwa bora zaidi ni maombi. 

Wakati matokeo hayo yanatangazwa binti huyo alikuwa akisikiliza nyimbo za injili huko  nyumbani kwao Salasala jijini Dar es Salaam. 

“Sikutarajia. Nilikuwa na uhakika kuwa sitofeli lakini sikutarajia kama nitaogoza pia,” Consolata ameiambia Nukta Habari baada ya kuulizwa amepokeaje matokeo hayo. 

Mwaka umeanza vizuri kwa binti Consolata Prosper baada ya kutangazwa kuwa mwanafunzi bora wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021 kutoka Shule ya Sekondari ya St Francis Girls iliyopo mkoani Mbeya.  Picha| Beatrice Halii.


Binti huyo amesema wakati akifanya mtihani, somo pekee lililomsumbua kidogo ni somo la Fizikia lakini mengine hayakuwa tatizo sana kiasi cha kumpa ujasiri kuwa angetoboa. 

Ndoto ya binti huyu ni kuwa dakari na ameahidi “kuendelea kufanya juhudi na kujitahidi katika masomo” siku zijazo. 

Familia nzima ya binti huyu imelipuka kwa furaha. Mama yake anasema ni “Mungu tu”. 

“Nina furaha sana. Ni Mungu tu amejibu maombi,” amesema Beatrice Halii, mama yake Consolata huku sauti yake ikibainisha furaha ya wazi. 

Mama Consolata amesema kikubwa walichofanya kwa binti yao ni “kumsapoti” kwa kumpatia mahitaji yote ya kielimu na jambo kubwa lilikuwa kumuombea wakati wote kwa Mungu ili afanikiwe zaidi.

“Tulikua tunamuombea tu kwani Consolata anapenda kusoma. Ni binti ambaye hakumbushwi kusoma wala kufanya kazi zake. Tulimpatia muda, zana za kujisomea na msaada wote aliouhitaji,” amesema mama wa Consolata.


St Francis “full shangwe”

Katika matokeo ya wanafunzi bora wanafunzi saba kati ya 10 wametoka Shule ya St Francis Girls wakiongozwa na Consolata.

Mtaaluma Msaidizi wa shule hiyo, Reginald Chiwanga ameiambia Nukta Habari kuwa siri za ushindi wa shule hiyo ni maombi na kufuata miongozo ilyotolewa na Necta kwa kuwa mitihani inajibiwa kwa uelewa.

Kingine ni mazingira mazuri ya kujifunzia, juhudi za watoto pamoja na ushirikiano wa uongozi wa shule.

“Kwetu Mungu ndiyo kipaumbele. Kila kitu sisi huwa tunaanza na sala,” amesema mwalimu Chiwanga