*FUMANIZI* (SEHEMU YA II)

*©Mwafrika Merinyo*

Hulka yake ilimwepusha ugomvi na mapigano kati yake na Rama. Tena hakumjua yule jamaa kwa jina wala kwa wasifu, seuze kipimo cha nguvu zake. Kidudumtu wake alimwambia tu kwamba kuna mtu, tena mtu mzima mwenziye, aliyekuwa anatia mkono katika sahani yake ya ugali na kusokota matonge makubwa kumzidi. Mwanzoni hakutaka kuamini. Kidudumtu akakoleza moto na kumwambia aje siku ya Jumanne kufumania, kwani mwizi wake alikuwa na tabia ya kuja kuchonga na kula nanasi siku za jumanne. Jambo hili kwanza lilimfadhaisha. Kisha likamtia hasira. Akaweka nia na kuingia mjini Uswazini siku ya Jumatatu kwa jahazi la jioni kutoka Chanjali. Akalala kwa jamaa yake na siku ya Jumanne akazuga mitaa ya mbali mpaka pale alipoletewa taarifa kuwa tayari nyegere analipua mashuzi mzingani na keshaanza kubugia asali.

Himid akatoka huko atokako kwa hasira na wahaka kwenda kumfumania mkewe Fatima. Baada ya kushindwa kupambana na mgoni wake, sasa alijikuta pia anaishiwa nguvu ya kupambana na Fatima.

“Ndio, umenikosea sana!” Sauti ya Fatima ilimgutusha Himid. Himid alijiuliza kama masikio yake yalimwongopea au alisikia sawa alichosema Fatima. Fatima mwenyewe hakujua neno lile lilimtokaje. Yawezekana ulikuwa mwitikio wa akili-silika ikimtuma kujinasua mtegoni. Au labda ndio akili ilichomoa hisia kutoka hifadhi yake bila utambuzi.

“Mume wangu,” aliendelea Fatima kutumia fursa iliyoachwa na ukimya wa Himid, bado akijishangaa maneno yalikotoka. “Wakumbuka nilikuomba uniongezee walau pesa kidogo nikanunue bati la kupaua kibanda changu kule shamba, ukanikatalia ilhali pesa ulikuwa nazo. Mmeuza nyumba ya familia, ukaja hapa na silingi milioni tatu kibindoni, usiniachie hata mia! Unafurahia kuniacha katika chumba kimoja cha kupanga! Katika hali hiyo nitakosaje kwenda kuomba msaada?” Fatima alijua kwamba kajitoa ufahamu ili ajiokoe, kwa mbinu ya kumpiga dafrau ya akili mumewe.

“Kwa hiyo kutoa uchi wako kwa huyo mwanaume ndiyo kuniadhibu mimi au?” Aliuliza kwa uchungu Himid. “Kwa hiyo amekupa pesa huyo afriti mwenzio?”

“Ndiyo!” Fatima akajibu kwa ujasiri uliomshangaza hata yeye mwenyewe. “Kaniahidi shilingi laki moja na elfu hamsini.”

“Ziko wapi hizo pesa?” Japo alishangazwa na maneno ya mkewe alitaka kujua ukweli wa jambo lile. Lakini nia yake hasa azichukue hizo pesa kumwadhibu Fatima, chambilecho Waswahili akose mtoto na maji ya moto.

“Sasa si umeharibu kila kitu?” Kasema Fatima. “Kabla hajapata haja yake wala kunikabidhi pesa, wewe umeingia na kutukatiza. Kaondoka na pesa zake!”

“Mwongo na mzandiki Fatima!” Akahamaki Himid. “Mlishamaliza mambo yenu!”

“Wallahi mume wangu, wala hakufanikiwa kuniingilia!”

“Nina habari kuwa ni bwana wako wa siku nyingi!”

“Aka!” Akaruka Fatima. “Kweli nimeshamkaribisha hapa lakini alikuwa akinitongoza tu, hatuja-” Himid akaipiga kwa kishindo meza ndogo iliyokuwa karibu yake kwa hasira na kumkatisha Fatima kauli yake.

“Hee, tayari muvi ishaanza!” Kidudumtu aliwaweka sawa wenzake kule uani kwa kusikia mbamizo ule wa meza.

“Kaniwekee maji ya kuoga.” Aliamrisha Himid baada ya kupiga kimya cha takriban dakika nne.

Fatima akanyanyuka, akachukua maji katika ndoo ya plastiki, kopo la kukogea kutoka uvunguni pa kitanda likiwa na dodoki, akatoka navyo nje. Alielekea maliwatoni kumwandalia mumewe. Ndani maliwatoni akaamua kufuta chembe yoyote ya ushahidi. Aliteka maji na kopo, akajisafisha vema kuhakikisha anafuta ushahidi kwa kiasi ilivyowezekana, akasafisha sakafu ya maliwatoni na kurudi ndani kuchukua maji mengine.

Wanawake waliokaa uani walimpapasa mwili mzima kwa macho yao ya kichimvi, wakijiuliza maswali kimoyomoyo bila kupata majibu.

“He, mwenzenu keshamroga huyu bwana!” Kidudumtu akaanzisha wimbo kwa sauti ya chinichini baada ya Fatima kuzama chumbani kwake.

“Lo! Yaillahi toba, tuokoe na majanga!” Mwenzake akabwagiza.

Fatima akawakatisha wimbo wao aliporudi na maji ya mumewe ya kuoga kutoka ndani, akaiweka ndoo maliwatoni na kurudi tena ndani.

“Maji tayari mume wangu” Alimwarifu mumewe, bado hofu imemjaa.

“Twende tukaoge wote mke wangu.” Alisema Himid, keshavua nguo zake na kukwida msuri tayari kwenda maliwatoni. Wawili hao wakafuatana kwenda kuoga. Walipowapita washabiki wa mambo pale uani, Kidudumtu na wapambe wake wakatumbua macho kama majuha, wasijue nini mwisho wa senema ile isiyoeleweka.

Maliwatoni, bwana na bibi wakakogeshana. Himid akafanya ukaguzi wake aliodhamiria, kwani kutaka kuoga na mkewe muda ule alikuwa na lengo maalum. Nia yake ampime mgonjwa joto kabla homa haijashuka. Baada ya kufanya kipimo akajiambia kuwa yawezekana japo chui kaingia zizini, yaelekea hakupata nafasi ya kumrarua mbuzi. Fatima akamtazama mumewe usoni, akatabasamu kama ishara ya kumsuta sambamba na kumwondolea wasiwasi.

“Hukuniamini sio?” Fatima akamuuliza Himid, akizidisha tabasamu lake la ushindi.

“Mhmm!” Himid aliishia kuguna, akitahayari na kujisikia aibu.

Usiku wa siku ile walilala kitandani kwa mtindo wa ‘kuviziana’. Bwana Himid, kama kawaida yake kwa miaka miwili sasa, akijidai kushughulika na mkewe kama ilivyo ada ya mume. Kuna nyakati huko nyuma kitendo chake hiki kilimkera Bi Fatima, lakini kwa kuihifadhi heshima ya mumewe akaamua kukivumilia. Himid alitumia vidole vyake kushughulika, mara avitie mate, mara hivi, akigunaguna na kuongea maneno yasiyokuwa na maana, maneno ya kujibaraguza. Na kilichomkera zaidi Fatima ni ukweli kwamba Himid alijua kuwa anaamsha waliolala ilhali hapana shughuli aliyoweza kuwapa.

-ITAENDELEA-