*FUMANIZI* (Hadithi fupi)

*©Mwafrika Merinyo*


Himid aligonga mlango mara ya kwanza. Akagonga mara ya pili. Mara ya tatu akalazimika kusindikiza na mwito: “Hodi!” Mwili ulimtetema kwa fukuto la hisia mchanganyiko. Hasira, uchungu, wivu, maumivu, wahaka. Alijua kilichokuwa kinaendelea ndani, kwani kaja kwa taarifa za kidudumtu na bila kumpa taarifa mkewe Fatima. Kaletwa na wahka, kabebwa na roho ya kisasi japo hakujipanga atakavyolipiza, kasukumwa na mshawasha wa kuadhibu bila kujua aina ya adhabu wala utekelezaji wake utakavyokuwa. 

Ndani, Fatima na Rama walikuwa ngomani. Walikuwa wamekolea mchezoni, kila mmoja akikwea mlima kutoka upande wake, wamekaribia kukutana kileleni. Kitanda kilikuwa kinaonewa, la kinaadhibiwa. Pumzi zao zilikuwa zikipishana mithili ya fuo za msana chuma. Palikuwa hapatoshi. Na katika patashika ile ya “Njoo basi! Nipishe nipite miye kwanza! Utaniua! . . .” ndipo hodi tatu  zilipogongwa kwa mfululizo mlangoni. Ilikuwa adhuhuri, jua limeuacha tu utosi. Alisema nani kuwa bundi halii mchana?

Hodi ya kwanza iliwagutusha. Wakazigusa breki za magari yao yaliyokuwa yakiserereka kilimani. Hodi ya pili ikawakata pumzi, fuo za mfua chuma zikakosa ridhimu. Hodi ya tatu iliyoambatana na kugongwa mlango ikawakata pumzi ghafla na kwa sekunde kadhaa, pumzi iliyojaa kifuani mwa Fatima ikashindwa kutoka na Rama aliyekuwa ametoa pumzi akashindwa kuvuta ingine kifuani. Fadhaa! Mshituko! Fatima akawa wa kwanza kukusanya fahamu.

“Yallah!” ikamtoka Fatima kwa ukelele wa kunong’ona. Ajabu kumkumbuka Mola wake katika dhahama ya aina ile! “Mume wangu huyo!” Alipiga kelele ya mnong’ono, akajizoazoa na kujishusha pale alipokuwa ameketi akiendesha farasi.

“Sasa?” Rama hakujua kama anajiuliza au anamuuliza Fatima. Mhamaniko ulizikumba fahamu zao. Fatima akaruka na kujikalisha kitandani. Alifuta kijasho chembamba kilichokuwa kikimtoka mwilini akitumia moja ya kanga zake zilizokuwa zimevurumshwa ovyoovyo pale kitandani, haraka akajifunga  moja kifuani na kukamilisha ya kiunoni huku akijiinua kusimama wima. Alipepesuka, kisha akasimama sawasawa katikati ya chumba. Macho yalimtoka pima, yakipepesa huku na kule chumbani kama aangaliaye pa kumficha Rama, akagundua jambo hilo haliwezekani. Saa ile Rama alishakuwa tembo ndani ya kasha la kiberiti!

Rama hakujua alichodhamiria Fatima. Yeye alikuwa na yake. Kabla Fatima hajakamilisha kujifunga kanga, Rama alishavaa nguo yake ya ndani, akaruka kutoka kitandani na kupandisha suruali kiunoni, akafunga zipu na kishikizo cha suruali bila kuwaza, vidole vikijiendesha kimazoea. Shati lilitiwa mwilini kwa sekunde saba tu na vifungo vikafungika kwa kasi ya umeme. Fatima alishatandika kitanda kama aliyeendeshwa kwa rimoti ya umeme. Akasogea mlangoni, anatetemeka mwili, miguu ikigongana magotini. ‘Abee’ na ‘nakuja’ zilizojaa kitetemo zilikuwa zikimtoka mfululizo kuitikia ‘hodi’ na ‘fungua’ za Himid.

Fatima alisimama nyuma ya mlango na kumwashiria Rama asogee kando ya mlango kule unakofungukia. Rama, kwa utii kama kuruta aamrishwaye na afande wake, akanyanyua begi lake na kwenda kusimama pale alipoelekezwa.

'Ko' ya ufunguo mara mbili, Fatima akaufungua mlango wazi na kwa ghafla. Fatima hakupima anachokifanya, wala Rama hakutarajia vile. Midume miwili ikajikuta ikitazamana, mmoja kwa mshangao, mwingine kwa hofu. Rama, kama aliyeendeshwa na rimoti, akiwa amejawa hofu ya hayawani aliyenaswa mtegoni, akapiga hatua kumwelekea Himid ili atoke nje ya chumba. Himid, kwa kupigwa na butwaa, akajikuta anarudi nyuma hatua moja; nusu akitaka amwone sawasawa mbaya wake, nusu akifadhaika moyoni na kuvurugwa akilini kwa kushindwa kuamua afanye nini kwa sekunde ile.

Kwa sekunde ya sekunde Himid alimtia machoni na kumpima harakaharaka mbaya wake: ana umri huenda sawa na wake, kama kuzidiana labda yeye Himid kamzidi kwa tarehe chache; ana wajihi wenye mvuto wa kiume, sharafa zilizochongwa vema na kuipa midomo minene kidogo nafasi ya kutulia chini ya sharubu zilizokatwa mkato mkali wa kitanashati. Alikuwa na mwili kumzidi Himid, musuli uliojaa kwenye shati jepesi la kunguru ya kahawia nyepesi na suruali ya jeans ya buluu iliyokoza. Himid alijihisi mwepesi katika makabiliano yale. Akapungukiwa nguvu, akasahau alikoiacha mikono yake, wala asikumbuke kuwa katika hali kama hii mikono ilikuwa na jukumu gani!

“Salaam aleykum!” Ikamtoka Rama kwa ujasiri ambao hata yeye hakujua ulikotokea, huku akipiga hatua ya pili na kujitoa mzima mzima kutoka chumbani, kama kulitoroka eneo la ushahidi. Kitendo cha Rama kilikuwa na kishindo kuliko kumbo ya mwili kwa Himid.

“Wal-kum s’lam!” alijibu kwa kubabaika Himid, begi lake la safari mkononi, asijue afanyeje kwa wakati ule. Himid, katika muda ule wa kupishana na mbaya wake, akagundua kuwa hawakuzidiana kimo. Rama akapiga hatua ya tatu na kumpita Himid aliposimama kama mlingoti, akaelekea mlango wa nje huku ameshika begi lake kama afisa aliyetoka kukamilisha mazungumzo ya kibiashara; potelea mbali hata kama hakukamilisha biashara iliyomleta. Alishusha pumzi, akapiga hatua kuelekea kituo cha basi kuanza safari ya kurudi kwake.

Uani pa nyumba palizuka mabishano miongoni mwa wanawake waliokuwa wameshajiandaa kuona mtanange. Kidudumtu ndiye aliyeongoza mzozo ule.

“Heee, katoka!?”

“Mwenzangu, tumekosa muvi!” Kabwagiza mwingine.

“Kha! Mwenye mali kamwogopa mwizi wake, au?” Huyu hakutaka kuachwa katika ushabiki ule.

“Ngojeni, picha halijaisha bado!” Walipeana moyo kusubiria hukumu ya mwenye mali kwa mali yake.

Himid alitatanika, asijue amfuate yule mgeni dukizi au aingie chumbani; akamwacha mkewe kwa sekunde kadhaa nae akihangaika na moyowe, mchecheto ukiupakata na kuupetapeta moyo uliokosa utulivu. Fatima akapata fursa ya dakika kujifunga vema kanga zake mwilini. Baada ya dakika moja ya mbabaiko, Himid alivuta hatua akaingia chumbani. Fatima akaurudisha mlango na kubaki amesimama mlangoni bila kuushindika kabisa mlango kama ilivyokuwa ada yake kumkaribisha mumewe. Pumzi zilikuwa zikimwenda mbio bado, asijue hatima ya mambo yale ingekuwaje. Alidhihirisha hofu na mbabaiko usoni. Alishindwa kuudhibiti mtetemo uliomvaa maungoni, vidole vya mikono vikimcheza, midomo ikicheza kama asemaye yasiyosikika, akiyapiga macho pande zote za dira bila kuangalia pahali mahsusi.

Himid alikuwa akikagua chumba kana kwamba mwizi alikuwa ametoka kuiba pale, naye akitaka kuona kilichoibwa. Machoye yalipiga kitandani, uvunguuni, dirishani, kutani, alimradi hajui akikaguacho.

“Mume wangu nisameheee!” aliangua kilio cha mtetemo Fatima. Hakujua yalikotoka machozi. Labda fedheha, au hofu, au kuhisi ukali wa kipigo alichotarajia kutoka kwa mumewe, kwani mkono wa Himid ulikuwa mwepesi pale anapoudhiwa na mwanamke. Himid alikaa kwenye kiti cha pekee kilichokuwa mle ndani, akihisi kuishiwa nguvu. Siku zingine ajapo alizoea kukaa kitandani, akihisi mahaba ya Fatima kutokana na maandalizi yake; lakini leo alihisi kitanda kimechafuka, akaona haramu kukikalia.

“Nimekukosea nini mke wangu?” Aliuliza Himid, akimkatiza Fatima kilio chake. Uso wake ulidhihiri mseto wa unyonge, huzuni, fedheha na hasira. Himid alishapitia mtihani mgumu na mbaya tangia alipopata tetesi za mkewe Fatima kumsaliti katika ndoa yao. Haidhuru kwamba alikuwa mkewe wa tatu, yeye akiishi na wakeze wawili huko Chanjali; lakini wivu wake ulimuuma kama kidonda, utadhani Fatima ndiye mke pekee.

Fatima alikiendea kitanda, akajipwetesha kwa unyonge, akikwepesha macho yake kukutana na ya Himid. Aliifumbata mikono yake na kuiweka katikati ya magoti, akainamisha kichwa kuepuka kumtazama mumewe. Alikuwa akijiuliza kimoyomoyo kwanini Himid hajamvaa na kumjeruhi hadi wakati ule.

“Mke wangu nakuuliza, nimekukosea nini?” alirudia Himid, sasa sauti yake ikipanda kama aliyekumbuka kuwa alipaswa kukasirika. Sasa hasira ilipanda, ikaja juu ya hisia za unyonge na fedheha. Ghafla alijiwa na mshangao. Kwanini hakupambana na yule mwanaume? Akajishangaa. Lakini akatanabahi kwamba katika maisha yake, na hata katika kazi yake jeshini, hakuwahi kupigana ngumi au hata kushikana mashati na mwanaume mwenzie. Hakuwa na hulka ya ugomvi, mara nyingi alipogombana na mtu alijiepusha na kupigana kwa kuhofia kupigwa na kutolewa ngeu, hata kama angelikuwa mshindi. Kisha taswira na jumbo la mgoni wake ikamjia, akatambua kuwa kumshambulia isingalikuwa busara. . . . japokuwa alibakiwa na hisia ya aibu kwamba chini ya uaskari wake na ukakamavu kazini, alikuwa nyanya, mlaini wa moyo.

-ITAENDELEA-