• Ni pamoja na kuwaunganisha na matumizi ya nishati safi za kupikia.
  • Nishati mbadala endapo anaishi eneo lisilo na umeme.
  • Nishati hizo zitaokoa afya ya wazazi wako na mazingira.

Dar es Salaam. Ni msimu wa mwisho wa mwaka, kipindi ambacho wengi hukitumia kama muda wa kuwasalimu ndugu zao waishio mbali.

Wengine huenda kuhesabiwa huku wengine wakitumia msimu wa sikukuu kama muda wa kupeleka wajukuu kuwasalimia babu na bibi zao.

Hata hivyo, unapoenda huko, haipendezi kwenda mikono mitupu. Inapendeza kwenda kuonana na ndugu zako walau ukiwa na kitu mkononi. Zawadi

Unadhani Waswahili walikosea waliposemaa, “mkono mtupu, haulambwi”? Usilitilie maanani hilo. 

Haya ni mapendekezo ambayo tovuti ya masuala ya mapishi na nishati safi na salama ya Jiko Point (www.jikopoint.co.tz) inakupatia kama zawadi zinazoweza kuwafaa unapoenda kuwasalimia katika msimu huu wa sikukuu. 

Ukimpatie zawadi ya jiko la gesi, hatohangaika kuchochea kuni au kuwasha mkaa. Picha| iStock.


Mtungi wa gesi na jiko lake

Mafanikio yako yanatakiwa kuakisi maisha ya wazazi wako kuwa bora. Huenda ni muda wa kumpumzisha mama na majukumu ya kuwasha mkaa na kuchochea kuni kwa kumnunulia mtungi wa gesi na jiko lake kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

Mbali na kuwapatia wazazi tabasamu usoni, utakuwa unaokoa afya ya mama yako na kumuondolea usumbufu wa kusugua masufuria yaliyojaa masizi.

Kwa kuanzia Sh250,000 unaweza kukamilisha ndoto ya mama yako kuachana na kuni au mkaa kwa kununua mtungi mkubwa na jiko la mezani. Unaweza pia kununua jiko kubwa kulingana na bajeti yako.

Kuwaunganishia mama umeme nyumbani

Siyo wote wamefikiwa na umeme. Wapo ambao bado gridi ya taifa haijawafikia hivyo kibatari, mishumaa na tochi bado ni sehemu za maisha yao.

Kuelekea msimu wa sikukuu, unaweza kuchagua kuwaunganishia wazazi umeme wa nishati mbadala ukiwemo wa sola au biogesi.

Kwa maisha ya vijijini, zipo kazi mbalimbali ambazo zinaweza kufaa katika ufuaji wa biogesi hasa endapo wazazi wanajihusisha na kilimo.

Kwa ambao biogesi inaweza isiwe sawa kwao, unaweza kuwafungia  umeme wa sola kwa ajili ya matumizi ya kuwashia taa na hata kupata burudani ya televisheni na redio.

Mbali na kumjali wazazi, utakuwa umechangia katika kupunguza matumizi ya nishati zinazotoa moshi (koloboi na mishumaa).

Wakati mwingine, mama anachohitaji ni kuona familia yake tu. Picha| VideoHive.


Muda wako

Kuna wakati mwingine wazazi hawahitaji makubwa. Wanachohitaji ni kuwaona watoto wao wakiwa wamejumuika na wakitabasamu pamoja.

Katika msimu huu wa sikukuu, Nukta Habari inakushauri hata kama hauna pesa, unaweza kujiandaa kwa nauli ya kukufikisha nyumbani na kukurudisha.

Amini ya kuwa wazazi watakupokea na mikono miwili huku wakitabasamu kufahamu kuwa mtoto wao anaendelea vyema. 

Unasubiri nini? Anza kujipanga sasa