Baraza la mitihani Tanzania NECTA  limetangaza matokeo ya kuhitimu Darasa la saba hivi leo. Bofya hapa kuona matokeo ya shule zote >>>HAPA>>
Orodha hiyo inaongozwa na Shule ya Msingi Graiyaki ya mkoani Mara.

Mkoa wa Kagera waingiza shule tatu.
Kanda ya ziwa yaongoza kuingiza shule nyingi.

Dar es Salaam. Wakati matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa leo yakipokelewa kwa hisia tofauti, Shule ya Msingi Graiyaki ya mkoani Mara ndiyo imeongoza kitaifa katika matokeo hayo huku Mkoa wa Kagera ukiongoza kuingiza shule nyingi katika orodha ya shule 10 bora kitaifa. 
Matokeo hayo ya mtihani huo uliofanyika Septemba mwaka huu yametangazwa leo Oktoba 30, 2021 na Baraza la Mtihani Tanzania (Necta) ambapo ufaulu wa ujumla umeongezeka kwa asilimia 6.6 ndani ya mwaka mmoja.
Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 74,130 ikilinganishwa na mwaka jana.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo ameitaja Graiyaki ambayo ilikuwa na watahiniwa 50 kushika nafasi ya kwanza kitaifa ikifuatiwa na St Peter Claver ya mkoani Kagera katika nafasi ya pili.
Nafasi ya tatu imeenda kwa Shule ya Msingi Rocken Hill ya mkoani Sinyanga, Kemebos ya Kagera imeshika nafsi ya nne huku Bishop Caeser ya Kagera pia ikishika nafasi ya tano.
Shule ya Msingi Kwema Modern iliyokuwa na watahiniwa 44 ya Shinyanga iko nafasi ya sita, St Magret (Arusha) nafasi ya saba, Waja Springs (Geita) iko katika nafasi ya nane na Kadama ya Geita imeshika nafasi ya tisa.
10 bora hiyo imefungwa na Shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic ya mkoani Pwani.
Kwa matokeo hayo, mkoa wa Kagera ndiyo umeingiza shule nyingi (3) ukifuatiwa na Shinyanga na Geita ambayo imeingiza shule mbili kila moja huku mikoa iliyobaki ikiingiza shule moja moja. Pia orodha hiyo imetawaliwa na shule kutoka Kanda ya Ziwa ambapo nane za kanda hiyo zimeingia.
Licha ya ushindani kuwa mkali kuwania orodha hiyo ya dhahabu, Graiyaki imefanikiwa kuvunja rekodi yake ya mwaka 2019 baada ya kuishusha Shule ya Msingi God’s Bridge ya mkoani Mbeya ambayo mwaka jana ilishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Shule hiyo ya God’s Bridge haipo kabisa katika 10 bora ya mwaka huu wala Mbeya haijafanikiwa kuingiza shule hata moja katika orodha hiyo.
Shule hiyo imeshika nafasi ya 756 kati ya 11909 katika kundi lake la shule zisizozidi wanafunzi 50
Katika hatua nyingine, Shule ya Msingi Twiboki ya mkoani Mara ambayo mwaka huu imefanikiwa kutoa wanafunzi watano bora kitaifa, imetupwa nje katika orodha ya 10 bora ambayo katika matokeo ya mwaka jana ilishika nafasi ya tatu

.