Dar es Salaam. Mwanadada Sarafina akiwa ameshirikishwa na msanii Baddest 47 wameimba kuwa “Single” kuna raha yake na utafurahia. 
Kufurahia huko ni pamoja na kulala usingizi bila hofu ya kusahau kutuma meseji ya “usiku mwema”.
Hata hivyo, kwa wengi kuwa singo ni kipindi cha mpito kwani utawadia muda ambao Adam atakutana na Hawa wake. Ombi ni kuwa, nyoka asiwafikie tena.
Lakini kwa kipindi ambacho hauna mawazo ya mahusiano, yapo mambo ya msingi ambayo unaweza kuyafanya ili Adamu au Hawa wako akiwasili, akukute upo tayari.
Wekeza katika kitu cha kukupatia kipato
Sijasema uache kutoka mtoko na marafiki zako kwenda kule mnakoendaga kujirusha. Ninachojaribu kusema ni kuwa, ni muhimu kuwa na kiasi. Usitumie fedha zako zote kwa kula bata na badala yake, anza kuwekeza.
Kuna mifuko ya uwekezaji kadha wa kadha ambayo unaweza kuwa unaweka fedha zako huko ili zijizolee faida baada ya muda fulani.
Pia unaweza kufungua akaunti ya benki ambayo hautoibugdhi na kuwa unaweka fedha zako huko kwa ajili ya malengo ya badaye.
Siyo poa siku unataka kuoa masela tukuchangie kila kitu, walau kuwa na hata cha kuanzia.
Ukiwa singo ndio muda wa kujitafuta. Picha Zoosk.

Jijenge kitaaluma
Ukiwa kwenye mahusiano, huenda ukapata vizingiti (distractions) ikiwemo ‘stress’ za hapa na pale ambazo zinaweza kukurudisha nyuma kitaaluma usipokuwa makini.
Mfano kuachwa na mtu umpendaye sana wakati kesho una wasilisho (presentation) ni lazima kutazingua wasilisho lako. Lakini ukiwa singo, vikwazo kama kuachwa, kutokujibiwa meseji kwa wakati au kukosa mawasiliano havikuhusu. Hivyo unamuda mwingi wa kujenga taaluma yako na ubongo. 
Utumie muda huo ili ukimpata mwenzi wako uwe na msingi tayari.
Jifunze kutoka kwa wanandoa
Posti za mitandao ya kijamii zinaweza kukufanya ukanunue pete ya uchumba leo leo umvishe binti wa watu au useme ndiyo kwa jamaa ambaye amekuwa hakauki kwenye “inbox zako”.
Hata hivyo, huenda picha na video hizo ni matukio mafupi ndani ya siku nzima wanayoipitia wapendanao wengi.
Tovuti ya Shirika la Lifehack ambalo inaandika juu ya masuala ya mahusiano, imeandika kuwa, kutumia muda wako, kwa mfano kipindi cha wikiendi ukiwA na wanandoa wa rika lako kutakufundisha mambo kadha wa kadha ambayo unatakiwa kujiandaa nayo endapo utaamua kuingia kwenye mahusiano. 
Usiishie kwenye familia moja, jifunze kwa famiLia mbali mbali.
Pia unaweza kusafiri, kutumia muda na rafiki zako na kufurahia maisha. Picha| Pexels.

Kama una uwezo, ishi mwenyewe
Hii inaweza kutegemeana na hali yako ya kipato. Kwa ambao wanauwezo wa kupanga, kujenga nyumba kwa ajili ya makazi, ni kitu kizuri pia kufanya ukiwa haupo kwenye mahusiano.
Tovuti ya masuala ya mtindo maisha ya Project Hot Mess imeandIka kuwa, kuishi mwenyewe kutakusaidia kukomaa kimaisha ikiwemo kujitunza.
Pale unapotakiwa kufanya kila kitu mwenyewe, itakusaidia kujifunza kujitegemea.
Sio lazima iwe kwenye jumba la kifahari,  inaweza kuwa hata kwenye chumba kimoja au chumba na sebule. Anza maisha yako.
Pia unaweza kutumia muda huo kusafiri, kuimarisha mahusiano yako na familia na kujitambua unahitaji mwenza wa kukukamilisha kwenye kipi.
Kuwa singo haimaanishi kila siku ulale baa. Inamaanisha umepata muda wa kujitafakari na kujitambua.

Tukutane wiki ijayo katika kolamu zangu za mtindo maisha.