Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania

 Arnold B. G. Msigwa

 Ikisiri 

Uthabiti wa taasisi yoyote ya elimu ya juu hasa katika ngazi ya Chuo Kikuu unatokana na uimara wa programu zitolewazo katika taasisi husika na ubora wa wahitimu katika ngazi husika. Kuimarika kwa programu kama za Umahiri na Uzamivu ni sifa mojawapo ya taasisi ya elimu ya juu. Kuimarika huko hakutawezekana kama eneo la istilahi za kitaaluma zinazotumika kwa uwanja husika isimu/fasihi na methodolojia ya utafiti hazitakuwa sanifu na thabiti. Hivyo, makala haya yanafafanua changamoto za kistilahi katika pragramu za M.A. (Kiswahili) na PhD (Kiswahili) katika TATAKI kwa uzoefu wa miaka mitano. Swali linaloibuliwa na makala haya ni je, kutakuwa na usanifu wa program kama usanifishaji wa istilahi haujafanywa na taasisi husika. Mwito wa makala haya kwa watawala wa TATAKI na Chuo Kikuu kwa ujumla wake, ni kwamba, hima usanifishaji wa Istilahi katika Kiswahili hasa katika eneo la methodolojia ufanyike haraka kabla jahazi kuzama. 

1. 0 Utangulizi

 Kuanzia mwaka 2009, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (kuanzia sasa TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilianza kutoa shahada ya M.A. (Kiswahili) na PhD (Kiswahili). Miongoni mwa matunda ya udahili huo ni kuhitimu wanafunzi watatu wa PhD katika mwaka wa masomo 2013/2014. Kulingana na TUKI (2013) na BAKITA (1974), istilahi ni maneno yanayotumika katika taaluma fulani ili kukidhi matakwa ya taaluma hiyo. Katika kuhakikisha kuwa kuna urari wa kazi zinazofanywa na wanafunzi wanaohitimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeweka mwongozo unaopaswa kufuatwa na wanafunzi wote. Kwa upande wa wale wanaojifunza kwa lugha ya Kiingereza kama vile: M.A. (Isimu), M.A. (Elimu) M.A. (Sheria) na M.A. (Uhandisi Umeme) kwa kutaja japo chache tu inaelekea kutokuwa na changamoto kwa sababu zimetumika kwa kipindi kirefu sana. Kwa upande wa uandishi wa tasinifu za M.A. na PhD (Kiswahili), kumejitokeza changamoto mbalimbali za kistilahi kwa Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 107 kuwa hili ni tapo jipya katika chuo hiki. Tangu kuanza kutolewa kwa programu hizi yaani M.A.na PhD Kiswahili hakuna mwongozo wowote wa istilahi uliotolewa na TATAKI ili kuwaongoza watafiti na wanafunzi. Ukosefu wa jambo hili umesababisha kuwapo mkubwa wa kistilahi kutoka kwa mwalimu mmoja na mwingine na hata kwa Watahini wa Nje ambayo hutahini kazi za wanafunzi wa kutoka TATAKI. Hivyo, haja ya kuwa na urari wa matumizi ya istilahi kwa wanafunzi wote ni jambo la welekea, na hili ndilo limemsukuma mwandishi kuandika makala haya. Nikiwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo kabisa kusoma pragramu ya M.A. (Kiswahili) na kuandika tasinifu kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ninaandika makala haya kueleza changamoto za matumizi ya istilahi katika uandishi wa tasinifu. Sababu ya kuandika makala haya ni kwamba, inavyoelekea tangu kuanza kwa Programu za M.A. na PhD (Kiswahili) mwaka hakuna jitihada ya makusudi inayolenga kutatua changamoto ya mkanganyiko wa istilahi. Changamoto zilizokuwepo mwaka 2009/2010 ndiyo hizo hizo zipo hadi hivi leo mwaka 2015/2016. Je, kwa hali hii tutafika? Katika kuonesha hali ilivyo pamoja na kuleta mtiririko wenye mantiki makala yatatalii tasinifu nzima toka sura za awali hadi sura ya mwisho. Maeneo ambayo hayana mkanganyiko sana yataachwa. 2. 0 Maana ya Changamoto Kulingana na (TUKI 2004:41) ni kitu, hali au jambo linalotia ari; hamu ya kufanya kitu; hamasa. Fasili hii inamaana kuwa changamoto ni kazi au hali inayomjaribu mtu uwezo wake wa kutatua mambo. Kutokana na ufafanuzi huu, makala haya yanatalii changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wanaoandika tasinifu za M.A. (Kiswahili) na PhD (Kiswahili) hasa katika kipengele cha istilahi. Licha ya kuwa na ari kwa pande zote mbili; wanafunzi kutaka kukamilisha masomo yao kwa upande mmoja na TATAKI kwa upande mwingine kutaka kuzalisha wataalamu wengi itakikanavyo, ipo kazi kubwa baina yao. TUKI (2004:13) ari inafafanuliwa kuwa ni hamu ya kutaka kukamilisha jambo na kutokubali kushindwa. Ni kusudio la makala haya kuwa pamoja na changamoto hizi tutakazozijadili punde kidogo, si vema kukubali kushindwa na kurudi nyuma. Ni nia ya makala haya kubainisha pengo linalojitokeza na kupendekeza baadhi ya istilahi ambazo zinaweza kuanza kutumiwa na wanafunzi wote katika urari kubalifu. Katika sehemu inayofuata tunajadili maeneo muhimu yaliyoleta sana changamoto katika kazi hizi. KISWAHILI JUZ. 79 108 3. 0 Maeneo yenye Changamoto katika Uandishi Kwa mujibu wa mwongozo wa jumla ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tasinifu imegawanyika katika vipengele mbalimbali ambavyo ni lazima vijitokeze wazi wazi. Miongoni mwa vipengele hivyo ni tamko la utafiti na mbinu za ukusanyaji wa data. Hivyo, katika sehemu hii tunabainisha vipengele mbalimbali vya tasinifu vyenye changamoto katika matumizi ya istilahi kwa shahada ya Umahiri na Uzamivu katika Kiswahili. Kipengele cha kwanza kabisa ni jina la programu. 3. 1 Jina la Programu Katika mchakato wa uandishi wa tasinifu, moja ya maeneo yaliyoleta na yatakayoendelea kuleta changamoto ni katika uandishi wa jina la programu yenyewe. Ingawa programu zote zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huandikwa kama ifuatavyo: M.A. (Linguistics), M.A. (Development Studies), M.A. (Engineering) na M.A. (Geography) kwa kutaja japo chache tu, kile kifupisho kinachorejelea Masters of Arts huwa kipo nje ya mabano wakati eneo la ubobezi (Specialization) likiwa ndani ya mabano. Hali iko tofauti kwa upande wa tasinifu zinazoandikwa kwa lugha ya Kiswahili au tasinifu zilizoandikwa kuhusu lugha ya Kiswahili ambapo hapa huandikwa M.A.Kiswahili. Swali la kujiuliza hapa ni je tasinifu zinazoandikwa au zinazoandikia kuhusu lugha ya Kiswahili ni tofauti na zile zinazoandikiwa kuhusu sheria kwa lugha ya Kiingereza? Hoja ya kuwa kufunga mabano kunamaanisha ndicho kilichosomwa zaidi lakini digirii hiyo inahusu vitu vingine tunadhani haina mashiko kwa sababu; mwanafunzi anayesoma sheria, ualimu, uhandisi na hata maendeleo, haya ndiyo maeneo anayobobea, na yule anayesoma Kiswahili hilo ndilo eneo linalobobewa na mwanafunzi husika. Hivyo ni vema taasisi ikatoa mwongozo bainifu kuhusu suala hili, kwani halijaeleweka vizuri. Ikiwa hoja ni kukwepa kuchanganya Kiingereza (M.A.) na Kiswahili kama baadhi ya hoja zilivyoibuka wakati wa ukusanyaji wa tasinifu hizo katika Kurugenzi ya Shahada za Uzamili, basi napendekeza istilahi ya Mahiri Kiswahili (M.K) badala ya Masters of Arts (M.A.). Aidha, katika shahada ya Udaktari wa Falsafa naya ilikumbana na changamoto hiyo. Baadhi ya watafiti katika ngazi za uandaji wa Pendekezo huandikwa shahada ya Uzamivu (Kiswahili) na waliowengi huandika PhD (Kiswahili). Swali ni je, msimamo wa TATAKI kwa ujumla kuhusu program hizi ni upi? Katika sehemu inayofuata tunajadili kuhusu Matumizi ya ama shahada au digrii. 3. 2 Shahada/Digirii Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha (2010: 360), shahada ni karatasi maalumu ya kuthibitisha kuwa mtu amehitimu na kufaulu masomo yake ya chuo; pia Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 109 digrii. Na dhana ya digrii inafafanuliwa na kamusi hii (uk 68) kuwa ni shahada ya kufaulu masomo ya chuo kikuu. Aidha, TUKI (2004: 364) wanafafanua kuwa shahada ni karatasi maalumu anayopewa mtu baada ya kupata mafunzo fulani katika chuo ili kuthibitisha kwamba amemaliza au amefaulu mitihani yake, pia digrii. Na digrii inafasiliwa kuwa ni shahada anayopewa mtu baada ya kupasi mtihani wa chuo kikuu. Fasili hizi zote mbili katika kamusi zote mbili zinaonesha kuwa dhana ya digrii na tena si digirii na shahada ni dhana ambazo hutumika kwa mtawalia. Hoja yetu hapa ni etimolojia ya neno digrii ni utohozi kutoka katika lugha ya Kiingereza degree. Katika tasinifu za M.A. na PhD (Kiswahili) imependekezwa kutumia digirii tena sio digrii kama kamusi zinavyolitambua badala ya shahada. Maoni yetu hapa kuhusu istilahi ni kwamba hata kama itakuwa digrii au digirii bado kuna hali ya ujinasibishwaji katika Kiingereza. Tunafahamu kuwa utohoaji ni njia mojawapo inayotumika katika kuunda maneno katika lugha za ulimwengu. Pia, tunafahamu kwamba utohoaji husaidia kupata istilahi wakati tunapokosa neno lifaalo kutoka katika lugha husika Mdee (1986). Hata hivyo, katika muktadha huu neno mwafaka katika lugha husika ya Kiswahili lipo ambalo ni shahada. Swali la kujiuliza hapa ni je kwanini tuendelee kujinasibisha na Uingereza wakati kusudio la uanzishwaji wa shahada hizi ni kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania? Je hili nalo linahitaji umataifa? Je ni sababu za ubeberu wa kiisimu ambapo lugha ya Kiswahili ni ya kitwana na lugha ya kiingereza ni watwana? Vyovyote iwavyo haja ya utohozi wa neno hili haikubaliki, kwasababu misingi ya uundaji wa istilahi hudai kuwa istilahi kopwa itumike tu pale ambapo hakuna istilahi ya asili Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008). Katika muktadha wa istilahi ya digrii na shahada haikuwa na haja ya kuendelea kujiegemeza katika istilahi iliyokopwa kutoka katika lugha malaika wakati lugha ya Kiswahili ina istilahi yenye maana sawa kabisa na hilo. 3. 4 Tamko la Utafiti, Tatizo la Utafiti, Rai ya Utafiti, Suala la Utafiti Katika uandishi wa tasinifu au utafiti kwa jumla, kipengele hiki ni kipengele muhimu sana. Kulingana na namna tulivyofundishwa na waalimu wetu wakati tukisoma kozi ya KIS 630: Mbinu za Utafiti. Kulingana na umuhimu wake inatarajiwa kuwe na urari wa namna fulani katika kubainisha kipengele hiki, mathalani tasinifu zote zinazoandikwa kwa lugha ya Kiingereza kipengele hiki huitwa Statement of the Problem tofauti kabisa na tasinifu za Kiswahili. Tutatoa mifano michache ya kazi za wanafunzi ambazo zimekwisha kuwasilishwa katika Kurugenzi ya Masomo ya KISWAHILI JUZ. 79 110 Uzamili zikiwa kila moja imeeleza kwa namna tofauti jambo hilohilo moja. Mfano tasinifu inayo husu Mfuatano wa Mofimu Nyambulishi katika Vitenzi vya Kikinga (Gawasike 2011:11) imetumia Tamko la Utafiti. Tasinifu inayohusu; Uchanganyaji na Ubadilishaji Msimbo katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010: Mifano katika wilaya ya Mufindi (Chalamila 2011:10) imetumia Tatizo la Utafiti. Tasinifu inayohusu; Nafasi ya Maudhui ya Filamu za Kiswahili katika Kuakisi Masuala ya Kijamii (Kileo 2011:4) imeita Tamko la Tatizo la Utafiti. Mifano hii michache inaonesha kuwa sehemu hii licha ya umuhimu wake mkubwa bado hakuna urari mmoja wa kukieleza miongoni mwa wanafunzi. Inaelekea kila mwanafunzi alikuwa anaogelea kadiri anavyoweza, hakukuwa na mwongozo thabiti ulitolewa ili kuwaongoza wanafunzi hawa. Hali hii isipofanyiwa kazi basi itajitokeza pia katika kazi zingine za wanafunzi wanaokuja nyuma baada ya hawa waanzilishi. Aidha, tulijipa kazi yakutalii kwa jirani zetu wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuona katika eneo hilo, wanaandikaje kwani nao si wakongwe sana katika kuandika tasinifu kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Tasinifu za Chuachua (2010) na Ponera (2010) zinaonesha wao wanatumia Tamko la Tatizo la Utafiti, inafanana kama mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Kileo 2011). Vile vile tulitalii kwa jirani zetu wa Kenya (wakongwe) kuona wao katika eneo hilo wanaliwekaje. Hali nako inaonesha kuwa sawa na hapa Tanzania, yaani kila Taasisi ina namna yake ya kuandika jambo hilo hilo kwa namna tofauti, rejea maelezo yetu ya aya tangulizi kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania). Mifano michache kutoka katika Chuo Kikuu cha Kenyatta itasaidia kuona hali hii. Gichuru (2010:4) Tasinifu ya Umahiri; Uchanganuzi wa Nomino Ambatani za Kiswahili: Mtazamo wa Mofolojia Leksia, ameita Suala la Utafiti. Naye Mukuthuria (2004) wa Chuo Kikuu cha Egerton Tasinifu ya Uzamivu; Kuathiriana kwa Kiswahili na Kimeru: Mfano kutokana na Wanafunzi wa Tigani, Kenya, yeye kaita Somo la Utafiti. Ikiwa katika eneo muhimu kabisa kama hili hali iko hivyo, ni maoni ya makala haya kuwa na istilahi moja ambayo itatumika kwa nchi zote, kwani kisiasa nchi za Afrika Mashariki zinaelekea katika shirikisho la Afrika Mashariki. Ikiwa ni vigumu kuwa na istilahi moja kwa nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki basi kuwe na urari wa kiistilahi angalau kwa nchi moja moja, na sio mchafukoge wa kiistilahi kwa kila taasisi hata kwa nchi moja. Aidha, ikiwa lengo la kuanzishwa kwa Kamati ya lugha ya Kiswahili ya Afrika ilikuwa ni kusanifisha lugha ya Kiswahili, yaani kuwa na namna moja ya kutumia lugha hii kwa nchi zote (tatu wakati huo) ni muhimu pia istilahi za uandishi wa tasinifu kwa wanagenzi wa Mahiri na Uzamivu zikasanifiwa kwa nchi zote tano sasa. Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 111 Na hilo ndilo lilikuwa jukumu la kwanza la kamati, kusanifisha maandishi na kuhakikisha kwamba kuna mtindo mmoja unaotumiwa katika nchi zote zinazohusika (Mbaabu 2007: 27). Kimajukumu kamati hii ilikuwa inahakikisha kuwepo kwa msamiati wa aina moja kwa nchi zote mbili. Swali ambalo tunajiuliza ni kwa nini baada ya kipindi kipatacho miaka themanini hivi suala la urari wa msamiati mmoja katika kazi za kitaaluma kama vile tasinifu limeachwa bila kushughulikiwa kama vile halina mwenyewe? Je, usanifishaji uliokuwa unakusudiwa na watawala wa kikoloni wa wakati huo sisi wa sasa tunaona hauna umuhimu? Ni msimamo wa makala haya kuwa ipo haja ya kufanya usanifishaji kwa nchi zote wanachama katika maeneo ambayo kimsingi yanaleta mkanganyiko miongoni mwa wanafunzi. Aidha, kwa Tanzania ni wakati mwafaka kufanya hivyo sasa kwa kuwa ndiyo kwanza programu zao hazipitiwa kwani miaka mitatu ya mapitio ya programu hizo ingali bado. 3. 5 Mipaka ya Utafiti, Upeo wa Utafiti, Mawanda ya Utafiti Ama kwa hakika hili ni eneo jingine ambalo limeleta mkanganyiko na pengine litaendelea kuleta mkanganyiko na tofauti za utumizi miongoni mwa wanafunzi. TUKI, (2004:439), wainafasili dhana ya upeo kuwa ni kiwango cha mwisho cha kuona, kuhisi au kutenda jambo. Mipaka ina fasiliwa kama mahala ambapo ni kikomo cha kitu na kingine kama vile shamba, nchi au kiwanja. Mawanda ni eneo ambalo mtu au akili inaweza kutalii. Aidha, BAKIZA (2010) wanafasili dhana hizi kuwa mpaka ni ukomo wa jambo; mawanda ni eneo ambalo akili ya mtu inaweza kuwa na ufahamu nalo na upeo kikomo cha uwezo wa jicho kuona. Hebu tujadili kwa uchache kidogo fasili hizi. Tukichunguza fasili hizi kama zilivyofasiliwa na Kamusi na tukihusisha na uelewa wetu wa kimalimwengu mambo yafuatayo yanajitokeza. Kwanza mpaka hutumika zaidi katika kutenganisha eneo la kijiografia mfano kiwanja, shamba, nchi, mkoa, wilaya n.k. hivyo utumizi wa dhana hii katika uga wa taaluma kumanisha mwisho wa kujadili, kuchunguza au kutathmini jambo kwa maoni ya makala haya haikubaliki. Aidha, dhana ya upeo kuwa ni uwezo wa jicho kuona (BAKIZA) nayo kwa mujibu wa makala haya nayo inatia shaka kwani katika uga wa taaluma mtafiti au mwanataaluma hafanyi kazi ya kuona tu, bali kazi yake kubwa huwa ni kuchunguza, kuchambua na kuchanganua kwa kutumia akili na maarifa mengine ya kimalimwengu ili kufikia hitimisho kuntu. Katika taaluma kwa maoni yetu utumiaji wa akili na kuhusisha na malimwengu mengine ni jambo la msingi. Kwa walekeo huu TUKI (2004) na BAKIZA (2010) wanaafikiana na kuwa Mawanda ni eneo ambalo mtu au akili (ya KISWAHILI JUZ. 79 112 mtu) inaweza kutalii. Kama tulivyokwisha kudokeza hapo juu, katika kazi za kitaaluma/utafiti mtafiti hutumia akili. Ili aweze kutoa matokeo mazuri na kubalifu lazima ajiwekee mawanda ambayo ndiyo yatakuwa kiunzi chake; yaani mwisho wa uchunguzi, ufafanuzi na usasanyuzi wake. Ama na wale watakao hitaji kumhukumu sharti wamhukumu kwa kuzingatia mawanda aliyojiwekea. Kwahiyo ni maoni ya makala haya kuwa mtafiti huweka mawanda ya kazi yake na sio mipaka (kijiografia) au upeo (kuona tu kitu). 3. 6 Mbinu za Utafiti na Methodolojia ya Utafiti. Mbinu za utafiti au (Methodolojia ya utafiti) ni njia mbalimbali zinazotumiwa ili kutimiza malengo ya utafiti, mathalani jinsi ya kukusanya data, kuzichambua na kuandika matokeo (Pennink & Jan 2010). Katika tasinifu ambazo zimekwisha kuandikwa kwa wanafunzi wa M.A. Kiswahili hili ni eneo ambalo linaonesha mvurugiko mkubwa. Na hali inavyoelekea hata programu ya Uzamivu inayoanzishwa muhula ujao itakuwa na mvurugano mkubwa. Kwa mfano Peterson (2011:14) katika pendekezo la utafiti ameita Mbinu za Utafiti. Naye Samwel (2011:15) katika pendekezo lake la utafiti shahada ya Uzamivu ameita Methodolojia ya Utafiti. Aidha, Mukuthuria (2004:76) katika tasinifu yake ya shahada ya Uzamivu kipengele hiki amekiita Mbinu za Utafiti. Pia Mturo (2011:26) katika tasinifu yake ya Umahiri ametumia Mbinu na njia za Utafiti. Mifano hii michache inaonesha hatari na mvurugano uliopo katika uandishi wa tasinifu za M.A. na PhD kwa Kiswahili. Tatizo sio hapa tu hata kwa majirani zetu wa Kenya. Hivyo ipo haja madhubuti kabisa ya kuwa na urari wa namna angalau moja za uandishi wa tasinifu miongoni mwa wanafunzi. 3. 7 Utumizi wa Vifupisho Ufupishaji ni njia moja wapo itumikayo kuunda maneno katika lugha, kwa mfano: Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA). Hata katika lugha nyingine mathalani Kiingereza mbinu hii pia hutumika. Kwa mfano, United Nations Organization (UNO) na University of Dar es Salaam (UDSM). Tendo hilo la kutumia ufupisho wa maneno huitwa Akronomi (Rubanza 1996:115). Wakati wa uandishi wa tasinifu si za Kiswahili pekee; yaani M.A. Kiswahili na au Ph.D kwa kawaida huwa na vifupisho mbalimbali. Changamoto kubwa ambayo imejitokeza katika kazi za wanafunzi wa M.A. Kiswahili ni uhawilishaji wa neno ambalo lipo katika lugha nyingine na kutengenezea kufupisho chake katika lugha nyingine. Kwa mfano wanafunzi wengi wanaoandika tasinifu zao kwa Kiswahili, rejea zao nyingi zipo katika Kiingereza. Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 113 Ilitarajiwa kuwa mwandishi awe anaandika kifupisho chake kutokana na lugha ambayo imefasiliwa mfano MLUTA ambayo imefinyazwa kutokana na kifipusho cha Mradi wa Lugha za Tanzania; ambayo Kiingereza chake ni LOT Language Of Tanzania (Gawasike 2011) Hali ilivyo kwa baadhi ya wanafunzi sivyo chunguza mifano ifuatayo: Kifupisho Neno katika Kirefu chake NEC Tume ya Taifa ya Uchaguzi REDET Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Demokrasia Tanzania Chanzo: Chalamila (2011: xvi) Ingawa eneo hili halijawa na kazi nyingi za wanagenzi wa mahiri kuchanganya lugha baina lugha moja na vifupisho katika lugha nyingine lakini mwangwi upo, kama mfano wetu huu unavyoonesha. Hatukuweza kupitia tasinifu zote za wanafunzi zaidi ya arobaini waliomaliza mwaka jana. Yumkini uchunguzi ukifanywa katika kipengele hiki unaweza kubaini matatizo mengi zaidi. Hivyo ni maoni ya makala haya kuwa wanagenzi wote wa mahiri na uzamivu wakumbushwe na kusisitiziwa kuwa makini na ufupishaji wao. Hasa ule unao husu lugha mbili tofauti. 4. 0 Mapendekezo na Maoni Ni maoni yetu kuwa jina la programu liwe Mahiri Kiswahili (M.K. Kiswahili) badala ya M. A. (Kiswahili) kama lilivyopendekezwa katika pendekezo la uanzishwaji wa programu yenyewe na kupitishwa na seneti. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tukipa hadhi Kiswahili na kuondoa kabisa mtazamo hasi uliojengeka miongoni mwa Tanzania kuwa Kiswahili hakiwezi kutumika kufundishia katika elimu ya juu. Aidha, mkanganyiko uliojitokeza dakika za mwisho wakati wa uwasilisaji tasinifu katika kurugenzi ya shule ya uzamili ulitokana na mambo mawili ambayo kwa kutumia M.K. (Kiswahili) yataepukwa. Mosi hakukuwa na msimamo mmoja kutoka katika TATAKI juu ya jina lenyewe, hivyo kuruhusu mwanya wa myumbo uliojitokeza. Pili katika pendekezo la programu hakuna ruwaza ya namna moja kwa mfano katika jalada linaloitambulisha programu ni Digrii ya M.A (Kiswahili), lakini ukiingia ndani rejea katika ukurasa wa 2, 3 na 5 programu hiyo hiyo inarejelewa kama MA (Kiswahili). Ni ukweli pia usiopingika kuwa tasinifu zilizokabadhiwa katika shule ya kurugenzi ya masomo ya uzamili zimetofautiana sana. Ili kupata urari wa namna moja basi ni vema jina la programu lenyewe likawekwa sawa kama inavyopendekezwa hapa. KISWAHILI JUZ. 79 114 4. 1. 1 Jina la Programu Katika makala haya tumegusia mara kadhaa katika mjadala wetu kuwa jina la programu iwe ni Shahada ya Mahiri Kiswahili M.K. (Kiswahili). Tumeeleza hapo awali kuwa kuita vyovyote vile ama digirii ya M.A (Kiswahili) au MA (Kiswahili) haielezeki kwa uzuri, kwani M.A au MA zote zinarejelea Kiingereza Masters of Arts. Masters katika Kiswahili ni Mahiri, hivyo tunafikiri kuwa ni mwafaka kabisa kutumia M.K. (Kiswahili) kuliko jina lolote kati ya hayo hapo juu, ambayo yanaelekea kushadidiwa katika mwongozo uliotumika katika kuiandaa hii programu. Aidha, kuondoa mabano au kuweka hakusemi chochote na suala zima la lugha. Shime kwa Wanaleksikografia ikiwa neno Masters halimo katika Kamusi zetu, liingizwe mara moja kabla meli haijaenda Mlama. Fasili yake tumekwisha ifasili katika makala haya. 4. 1. 2 Shahada badala ya Digirii Kama ilivyoelezwa katika § 3. 2 kuwa kwa tasinifu za M.A.Kiswahili na PhD (Isimu) zitumie shahada badala ya digirii. Digirii au digrii etimolojia yake ni kutoka katika lugha ya Kiingereza. Ili hali dhana hii ina kisawe chake kilichozoeleka katika lugha ya Kiswahili shahada tunaona ulazima wa kukopa dhana ya digirii haupo kwa kuwa katika lugha ya Kiswahili tayari kuna istilahi inayojitosheleza. 4. 1. 3 Tamko la Utafiti Aidha tamko la utafiti linapendekezwa kutumika kwani linarejelea maana sawa kabisa na Statement of Problem katika Kiingereza. Istilahi kama tatizo la utafiti, linajenga dhana kuwa utafiti unatafiti au unatoa matokeo yenye kutia shaka. Kwa mujibu wa TUKI (2004) dhana ya rai, kimsingi ni maoni. Utafiti kwa hakika si maoni tu, bali ni uchunguzi na uchambuzi unaofanywa kisayansi kwa kuongozwa na nadharia fulani na kufikia hitimisho. Ama kwa hakika kile kinachoelezwa na mtafiti katika sehemu hii kwa hakika sio tatizo wala maoni tu bali huwa ni haja au sababu inayomfanya mtu kufanya utafiti anaokusudia kufanya. Wakati mwingine huwa ni kuongeza maarifa katika uwanja fulani au kujribu kuziba pengo fulani la kitaaluma ambalo kwalo halikuzibwa. Hivyo tamko la utafiti tunadhani lingefaa zaidi hapa kuliko maneno mengine. 4. 1. 4 Mawanda ya Utafiti Makala pia yanapendekeza matumizi ya istilahi ya mawanda ya utafiti badala ya mipaka ya utafiti na au upeo wa utafiti. Hoja yetu inatokana na mipaka ya utafiti hurejelea eneo la kijiografia mfano mpaka wa kiwanja, shamba, nchi n.k hauhusishi suala lolote la akili za mwanadamu. Ama kuhusu upeo, una husu uwezo wa kuona Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 115 kwa kutumia macho, utafiti hauhusu tu kuona kwa macho. Wakati mwingine utafiti unahusu Uchunguzi wa mambo ambayo huwezi kuyaona kwa macho bali matumizi ya akili na utashi wa mwanadamu ili kufikia hitimisho ya malengo yaliyokusudiwa, ambapo dhana ya mawanda ndipo inapoingia. 4. 1. 5 Mbinu za Utaifi na Methodolojia ya Utafiti Kwa dhana hizi mbili, ni mapendekezo ya makala haya kutumia istilahi ya mbinu za utafiti badala ya methodolojia ya utafiti. Hoja ni kuwa ikiwa methodolojia na mbinu zinatumika kwa maana karibu sawa. Na ikiwa hoja ni kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kutumia kadiri iwezekanavyo msamiati ambao haujiegemezi zaidi katika Kiingereza, basi dhana ya mbinu za utafiti ni faafu zaidi kuliko methodolojia. Methodolojia inatokana na istilahi ya Kiingereza methodology. Tunaomba hapa ieleweke kuwa, hatukipingi Kiingereza kuingiza baadhi ya msamiati wake katika Kiswahili lakini tunadhani ifanyike hivyo mahala ambapo msamiati huo umekosekana katika lugha ya Kiswahili. Tunadhani kuendelea kufanya hivyo na sisi wenyewe wadau wakuu wa lugha ya Kiswahili ni kuwaaminisha watu wenye mtazamo hasi na Kiswahili kuamini kuwa lugha hii si lolote katika taaluma jambo ambalo sio sawa. Aidha, vipengele vingine vinavyoambatana na sura hii sharti vichunguzwe na kupatiwa mwongozo ambao unaweza kusaidia kwa namna fulani kuleta urari wa kazi za wanagenzi wamahiri na wazamivu. 5. 0 Hitimisho Makala haya yalikusudia kubainisha changamoto mbalimbali wanzaokumbana nazo wanagenzi wa Mahiri na wanagenzi wa Uzamivu katika matimizi ya istilahi wakati wa kuandika ripoti zao za utafiti. Mwelekeo uliweka katika kubainisha tatizo la istilahi katika uandishi wa tasinifu, kwa kujiegemeza katika tajiriba ya wanafunzi wa awamu ya kwanza wa M.A.Kiswahili, hata hivyo mifano michache kutoka nje ya TATAKI na pengine nje ya Tanzania ilirejelewa ili kubainisha mkanganyiko. Maeneo yaliyomakinikiwa ni pamoja na: Jina lenyewe, shahada au digirii, tamko au rai ya utafiti, mawanda au upeo, mipaka ya utafiti, methodolojia dhidi ya mbinu za utafiti yenye mkanganyiko yamebainishwa kwa kutumia mifano maridhawa. Vilevile matumizi ya vifupisho kwa kiasi kidogo yamegusiwa, hata hivyo imeoneshwa kuwa katika eneo hili hali si mbaya sana ila kuna mwangiwi fulani (au moshi una vuka). Mapendekezo kadhaa yametolewa na sababu za upendekezi wa matumizi ya istilahi hizo. KISWAHILI JUZ. 79 116 Marejeo BAKIZA, (2010), Kamusi la Kiswahili Fasaha. Oxford, Kenya. Chalamila, A (2011), Uchanganyaji na Ubadilishaji Misimbo katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010: Mifano kutoka katika wilaya ya Mufindi, Tasinifu ya M.A.Kiswahili (haijachapwa), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Chuachua, R (2010), Suala la Itikadi katika Riwaya za Shaaban Robert. Tasinifu ya M.A.Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Gawasike, A (2011), Mfuatano wa Mofimu Nyambulishi katika Vitenzi vya Kikinga, Tasinifu ya M.A.Kiswahili (Haijachapwa) Chuo Kikuu Dar es Salaam. Gichuru, T. M (2010), Uchanganuzi wa Nomino Ambatani za Kiswahili: Mtazamo wa Mofolojia Leksia. Tasinifu ya M.A.Kiswahili (Haijachapwa), Chuo Kikuu cha Kenyatta. Mbaabu, I (2007), Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. TUKI, Dar es Salaam. Mdee, J. S (1986), “Matitizo ya Uundaji Istilahi kama yanavyojitokeza katika Kiswahili” katika MULIKA Na 18, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (uk 52-63). Mukutharia, M (2004), Kuathiriana kwa Kiswahili na Kimeru: Mfano kutokana na Wanafunzi wa Tigania, Kenya, Tasinifu ya Uzamivu (Haijachapwa), Chuo Kikuu cha Egerton. Pennink, B na Jan Jonker, (2010), The Essence of Research Methodology: A Concise Guide to Masters and PhD Student in Management Science. Sprinker Heidelberg Dordrecht, London New York. Peterson, R (2011), Matumizi na Dhima za Lugha katika Mandhari – Lugha ya Jiji la Dar es Salaam, Pendekezo la utafiti liliwasilishwa Juni, 2011 katika TATAKI kwaajili ya shahada ya Uzamivu. Ponera, A. S (2010), Ufutuhi Katika Nathari za Shaaban Robert: Maana yake, Sababu za Kutumiwa na Athari zake kwa Wasomaji. Tasinifu ya M.A.Kiswahili (Haijachapwa), Chuo Kikuu cha Dodoma. Rubanza, Y. I (1996), Mofolojia ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dar es Salaam. Samwel, M (2010), Nafasi ya Ushairi wa Majigambo ya Bongo Flava/Hip hop katika Maendeleo ya Fasihi Simulizi ya Tanzania. Pendekezo la utafiti lililowasilishwa Desemba, 2010 katika TATAKI kwaajili ya shahada ya Uzamivu. Changamoto za Istilahi katika Uandishi wa Tasinifu za Uzamili wa Kiswahili Tanzania 117 Kileo, S. E (2011), Nafasi ya Maudhui ya Filamu za Kiswahili katika Kuaksi Masuala ya Kijamii, Tasinifu ya M.A.Kiswahili (Haijachapwa), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tumbo-Masabo, Z. N. Z, na Herlman,J. M. M (2008), Kiongozi: Uundaji wa Istilahi za Kiswahili. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam. TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu toleo la Pili. Oxford, Kenya.