Mpaka sasa mjadala umehusu vipashio vya kifonolojia, hususa fonimu na alofoni. Lakini kila mjua-lugha anatambua kuwa watu hawazungumzi kwa kutumia fonimu moja moja. Hata kama tukiweza kuorodhesha fonimu zote za lugha fulani pamoja na alofoni zao, bado tutakuwa hatujajua mfumo wa fonolojia wa lugha hiyo ulivyo. Katika kutumia fbnimu za lugha ili kuunda maneno, na kufanikisha mawasiliano, kuna kanuni za msingi ambazo kila lugha inazifuata.

Kanuni ya jumla sana, na ambayo tumekwishaigusia katika kurasa zilizotangulia, ni ile ya mfuatano unaoruhusiwa wa fbnimu za lugha fulani; na katika kanuni hii, lugha hutofautiana sana. Katika lugha ya Kiingereza, kwa mfano, vipasuo sighuna /p, t, k/ vinaweza kufuata kikwamizi /s/ lakini vipasuo ghuna /b, d, g/ haviwezi. Hivyo kuna maneno:

28 {spar, star, scar}, lakini hakuna
29 *{sbar, sdar, sgar}

Wazungumzaji wa Kiingereza wanajua wazi kuwa maneno ya (29) hayawezi kuwa maneno ya lugha yao kwa sababu hayaruhusiwi na kanuni za kifonolojia za lugha hiyo.

Mfumo-sauti asilia wa lugha ya Kiswahili hauruhusu mfuatano wa konsonanti mbili katika neno, isipokuwa ikiwa consonanti hizo ni ving’ong’o /m, n,/ ambavyo vinapata usilabi. Ndiyo sababu wanafonolojia wanasema muundo kawaida wa silabi katika Kiswahili ni firabu}, konsonanti + irabu} au {m, n}. Kati ya sauti hizi mbili za ving’ong’o, sauti /m/ inao uhuru zaidi wa kufuatiwa na sauti za makundi mengine kuliko sauti /n/. Kwa mfano, wakati ambapo /m/ inaweza kufuatwa na vipasuo vyote, ghuna na sighuna, /n/ inaweza kufuatwa na kipasuo /t/ peke yake. Sauti nyingine ambazo zinaweza kufuata /n/ ni pamoja na /z, c/. Sauti /m/ inaweza kufuatwa na sauti nyingine zote, na pia yenyewe na /n/.

Muundo huu wa silabi katika Kiswahili umebadilika kutokana na maneno ambayo yameingia katika lugha hii kutoka lugha nyingine, kama tulivyosema katika 3.0. Ingawa mengi ya maneno hayo yamesawazishwa ili yapatane na mfumo-sauti wa Kiswahili, yapo machache ambayo yameachwa na mfuatano wa konsonanti wa lugha yalikotoka. Baadhi ya maneno haya tumeyagusia katika mfano wa (5) wa sehehmu ya 3.0.

Kanuni nyingine ya lugha ya Kiswabili ni ile inayosema kuwa maneno ya lugha hiyo yanaishia na irabu. Konsonanti, hata /m, n/ haziruhusiwi mwishoni mwa neno. Lakini katika maneno machache ambayo asili yake ni lugha nyingine wazungumzaji wengine wanayatamka na konsonanti mwisho. Maneno hayo ni kama:

30 a) {salaam} badala ya {salamu}
b) {mtaalam, utaalam} badala ya {mtaalamu, utaalamu}
c) {Seif} badala {Seifu, Sefu}
d) {Khamis} badala ya {Hamisi}, n.k.

Wazungumzaji ambao hawajui lugba ambapo maneno haya yametoka, mara nyingi watatumia maneno yenye irabu mwisho, kama kanuni za Kiswahili zinavyotaka, ingawa mzungumzaji huyo huyo anaweza pia kutumia maneno yote kwa wakati tofauti. Kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya mzungumzaji achague mojawapo ya matamshi hayo. Sababu hizo ni uwanja unaoshughulikiwa na isimu-jamii.

Kanuni nyingine za kifonolojia ni pamoja na zile ambazo tumekwishazijadili katika sehemu 3.3 kama za alofoni za fonimu tofauti katika lugha mbali mbali.

Mbali na kanuni hizi za jumla, zipo kanuni nyingine ambazo zinatokana na matumizi ya sauti za lugba katika sintakisia ya lugha hiyo, na hasa katika muundo wa maneno (mofolojia). Mara nyingi kanuni hizi huitwa kanuni za kimofonolojia kwa sababu zinahusu minyumbuo inayotokea katika matamshi ya neno kwa kuathiriwa na vipashio vya kisarufi vinavyofuatana.

Mfano mdogo wa kwanza ambao tunaweza kuuangalia ni ule unaobusu ‘tabia’ ya kipashio {ha-} cha ukanushi. Kwa kawaida kipashio hiki kinajitokeza na umbo hilo katika semi zifuatazo:

31 {hatutaimba, hamtaimba, hawataimba} n.k.

Lakini ikiwa kipashio kinachofuata {ha} ni cha nafsi ya pili au ya tatu umoja, semi hizi zinakuwa:

32 a) {hutaimba} na siyo *{hautaimba}
b) {hataimba} na siyo *{haataimba}

Kanuni inayotawala hapa ni ile inayosema ‘dondosha irabu ya kikanushi ikiwa kipashio kinachofuata ni cha nafsi ya pili au ya tatu wnoja’. Hii ni kanuni maalumu inayohusu tu mfuatano wa kipashio cha ukanushi na hivi vipasbio viwili, kwa sababu hakuna kanuni ya jumla inayokataza mfuatano wa irabu mbili, kama maneno mengi ya Kiswahili yanavyodhihirisha. Hata kama kipashio {ha} kitafuatwa na kipatanishi cba kundi lingine la nomino kinachoanza na irabu badiliko hili halitokei:

33 a) {mlango haukufunguka} na siyo *{hukufunguka}
b) {nyumba haitaanguka} na siyo *{hitaanguka}

Kanuni kama hiyo inayohusu kikanushi tunaiita ya udondoshaji, na kanuni kama hizi ni nyingi sana katika Kiswahili.

Mfano mmoja rahisi ni ule unaohusu mabadiliko yanayotokea wakati viambishi ngeli vinapoambikwa kwenye maneno ya kundi la sifa yanayoanza na irabu. Kanuni hii inadhihirika katika orodha mbili zifuatazo:

34 a) mtu mwema
b) watu wema
c) kitu chema
d) vita vyema
e) jambo jema
f) mambo mema

35 a) mtu mzuri
b) watu wazuri
c) kitu kizuri
d) vitu vizuri
e) jambo zuri
f) mambo mazuri, n.k.

Bila shaka unaweza kukamilisha orodha hizo kwa ngeli zilizobaki, lakini kama mfano, tutaishia hapo, ili tuone hasa kunatokea nini. Ni wazi kuwa kuna kanuni za msingi zinazotawala katika maneno ya (34) hapo juu, na pia kwamba ikiwa tutakuwa na neno lingine la sifa linaloanza na irabu, basi kanuni kama hizo zitafuatwa.

Katika (a), kwa vile neno la sifa linaanza na irabu, umbo la kipatanishi linatikiwa kuwa {mu} badala ya {m}, lakini kuna kanuni ya jumla katika mofonolojia ya Kiswahili inayosema kuwa ‘{u-} huwa {w-} kabla ya mzizi unaoanza na irabu’. Tunasema ni ya jumla kwa kuwa inahusu maneno mengi sana kama vile {mwalimu, mwana}, n.k ambayo kimsingi yangekuwa {mualimu, muana}. Katika (b) tunaona kanuni mojawapo ya udondoshaji wa irabu ya kipatanishi na hivyo umbo la kipatanishi linakuwa {w} badala ya {wa}. Katika (c) na (d) kuna kanuni ya ‘ulainishaji’ ambayo inahusu ngeli ya 7 na ya 8 inayosema kuwa ‘kiambishi ngeli {ki} huwa {ch} na {vi} huwa {vy} ikiwa mzizi wa neno unaanza na irabu’ (shuhudia maneno {chumba, chombo, vyumba, vyombo}).

Maneno yanayofuata ya mifano ya hapo juu yanaonyesha jinsi kanuni nyingine za jumla zinavyotumika. Katika (e) kuna kanuni inayohusu kipatanishi cha ngeli ya tano ambapo ‘kipatanishi huwa {ji-} ikiwa mzizi wa neno unaanza na irabu, au una silabi moja tu, mahali pengine huwa {F}’ (kapa) (shuhudia maneno {jicho, jiwe} kwa upande mmoja, na {tunda, chungwa} n.k. kwa upande mwingine). Katika neno {jema} kanuni mbili zimefanya kazi, moja baada ya nyingine, yaani ya uwekaji wa {ji-} na udondoshaji wa irabu ya kipatanishi, kanuni ambayo tumekwishaiona hapo juu. Kanuni hiyo hiyo ya udondoshaji ndiyo inayojitokeza katika (f) na hivyo tunapata umbo {mema} badala ya *{maema}.

Kanuni nyingine muhimu katika sarufi ya Kiswahili ni ile ya ‘uingizaji’ wa kipashio cha ziada katika usemi. Kwa mfano:

35 a) nitakula
b) nitakuja.

Katika mfano huu, tunaona kuwa kuna kipashio {ku} ambacho kimeingizwa katika kifungu tenzi, kipashio ambacho hakipo katika

35 c) nitaimba
d) nitasema

Hivyo tunasema kuwa, kanuni hii inahusu vitenzi vya silabi moja. Na hata hivyo, si kila mahali kanuni hii inatumika, kama mifano ifuatayo inavyodhihirisha:

36 a) hali (na si *hakuli)
b) haji (na si *hakuji)

Tunaweza kulinganisha miundo hiyo na

36 c) haimbi
d) hasemi.

Katika kuandika kanuni hii, ni muhimu kuonyesha kwa uwazi ni wapi kanuni hii inatumika, na wapi haitumiki kwa kuchunguza mazingira yake yote.

Kanuni kama hizo za udondoshaji na uingizaji wa vipashio zinajitokeza katika lugha nyingi, hata zile ambazo hazina uhusiano na Kiswahili. Kwa mfano, katika semi za lugha ya Kifaransa, konsonanti ya mwisho katika neno inadondoshwa ikiwa neno linalofuata linaanza na konsonanti au kilainisho, lakini inabakizwa ikiwa neno linalofuata linaanza na irabu au kiyeyusho:

37

a) Kabla ya konsonanti:

{petit tableau} [peti tablo] (picha ndogo)



{nos tableaux} [no tablo] (picha zetu)


b) Kabla ya kilainisho:

{petit livre} [peti livr] (kitabu kidogo)



{nos livres} [no livr] (vitabu vyetu)


c) Kabla ya irabu:

{petit ami} [petit ami] (rafiki mdogo)



{nos amis} [noz ami] (rafiki zetu)


d) Kabla ya kiyeyusho:

{petit oiseau} [petit wazo] (ndege mdodo)



{nos oiseaux} [noz wazo] (ndege wetu)

Kwa upande mwingine, katika lugha ya Kihispania, kuna kanuni inayoongeza kipashio /e/ mwanzoni mwa neno ambalo linaanza na /s/ ikifuatwa na konsonanti nyingine kama katika maneno:

38 a) escuela (shule)
b) estampa (stempu)
c) Espana (Hispania)
d) espina (uti wa mgongo)
e) escribir (kuandika)

Kipashio hiki cha ziada kinadondoshwa ikiwa maneno haya yanaunganishwa na maneno mengine katika usemi:

38 f) transcribir (kunukuu).

Kanuni ya mwisho tutakayoangalia katika sehemu hii ni ile ya usilimisho. Huu ni mnyumbuo unaohusu kuathiriana kwa sauti zinazofuatana, lakini kwa sharti kwamba sauti hizo ni sehemu za vipashio tofauti vya kisarufi, kama katika kanuni tulizozijadili hapo juu. Mfano mmoja ni ule wa tabia ya kiambishi-ngeli cha ngeli ya 9 katika Kiswahili (na lugba nyingine za Kibantu), ngeli ambayo kwa mazoea huitwa ngeli ya ‘king’ong’o’ au ya /N/. Kanuni inayotawala ‘utamkaji’ wa kiambisbi hiki inategemea mzizi wa nomino unaanza na sauti gani. Ikiwa mzizi wa neno unaanza na kipasuo ghuna /b, d, g/ kiambishi hicho kitapatana na kipasuo hicho katika mahali pa kutamkia, na sauti inayotokea itakuwa ‘kipasuo-ng’ong’o’ kama sauti tulizokwisha zijadili katika 3.4. Ikiwa mzizi unaanza na konsonanti nyingine, kiambisbi ngeli /N/ kitajitokeza kama /F / (kapa). Ndiyo sabbau katika ngeli hii tunapata maneno yafuatayo:

39

a) N + buzi

®

{mbuzi}

(linganisha {kibuzi})


b) N + dizi

®

{ndizi}

(ling. {kidizi})


c) N + goma

®

{ngoma}

(Ling. {kigoma}).

Lakini maneno yafuatayo yanabaki yalivyo:

39

d) N + panzi

®

{panzi}


e) N + tembo

®

{tembo}


f) N + kuni

®

{kuni}


g) N + simba

®

{simba}


h) N + chui

®

{chui}, n.k.

Kanuni ya namna hii pia hujitokeza katika lugha ya Kishambala, lakini katika lugha hii, usilimisho unahusu vipasuo vyote, gbuna na sighuna. Kama utakumbuka, tulisema katika sehemu ya 3.4. kuwa lugha ya Kishambala inazo fonimu sita za vipasuo-ng’ong’o, ambapo Kiswahili inazo tatu tu. Utokeaji wa kanuni hii ya usilimisho katika lugha zote mbili unathibitisha kuwa kanuni za kifonolojia hazitangui mfumo-sauti wa lugha. Katika Kishambala usulimisho wa /N/ na vipasuo katika mazingira yanayofanana na yale ya Kiswahili hujitokeza ifuatavyo:

40

a) N + buzi

®

{mbuzi}

(mbuzi)


b) N + dama

®

{ndama}

(ndama}


c) N +goma

®

{ngoma}

(ngoma}


d) N + pasi

®

{mpasi}

(panzi)


e) N + tembo

®

{ntembo}

(tembo)


f) N + kuni

®

{nkuni}

(kuni)

Lakini maneno yafuatayo yanabaki yalivyo:

40

g) N + shimba

®

{shimba}

(simba)


h) N + sighe

®

{sighe}

(nzige)


i) N + nange

®

{nange}

(kibuyu), n.k.

Kama tulivyokwisha sema, kanuni za aina hii ni nyingi sana katika lugha tofauti, lakini si rahisi kuainisha mazingira yote ambayo yanatawala utokeaji wa kanuni hizi. Katika sura ifuatayo tutazidi kuona umuhimu mkubwa wa kanuni hizi za kifonolojia katika uundaji wa maneno ya lugha mbali mbali.