fasihi simulizi na utamaduni wa jamii zinavyohusiana
ELEZA UHUSIANO KATI YA FASIHI SIMULIZI NA UTAMADUNI WA JAMII.
Fasihi
simulizi ni sanaa
inayotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana katika kufikisha ujumbe
uliokusudiwa kwa hadhira husika. Hii ni sanaa ambayo ujumbe wake upo katika
mfumo mzima wa pande mbili za mawasiliano kuwepo pamoja ana kwa ana hii
ikimaanisha fanani yaani mtu anayerithisha (msimuliaji) na Hadhira yaani mtu
anayerithishwa (msimuliwaji). Kwa njia hii fasihi simulizi hushirikisha au
huwafikia watu wengi na mawazo ambayo jamii iliyakubali, imeyakubali,
inaendelea kuyakubali yatokeapo na inayapitisha na au kuyakabidhi kwa
kuendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine kwa njia ya mdomo.
Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake.Hiyo inajumlisha ujuzi, imani, sanaa, maadili , sheria, desturi n.k. ambavyo
mtu anajipatia kama mwanajamii.
Kama sifa maalumu ya binadamu, inayomtofautisha na wanyama, utamaduni ni suala la msingi katika anthropolojia, ukihusisha yale yote yanayopokezwa
katika jamii fulani, kama vile lugha inayounganisha watu wanaohusika nao ,fasihi, mafungamano, ndoa,michezo,ibada,
sayansi na teknolojia.
Utamaduni ulioendelea
unaitwa pia "ustaarabu". Kila utamaduni unabadilikabadilika
mfululizo: ndani ya watu husika, baadhi wanachangia na
kuunga mkono
mabadiliko, wakati wengine wanayakataa. Ujuzi mpya na teknolojia, pamoja na
mahitaji ya uchumi, ni kati ya
mambo yanayosukuma zaidi kubadili kiasi fulani utamaduni.
Hakuna
jamii isiyokuwa na fasihi simulizi , kwa
sababu iliibuka pale jamii zilipoanza
kutumia lugha kama chombo cha mawasiliano. Kwa muda mrefu,
fasihi kwa ujumla imechukuliwa kwamba jukumu
lake ni kuburudisha na kustarehesha. Majukumu
haya mawili yanatokana na maumbile ya
sanaa hii. Fasihi simulizi
imetumiwa kuamsha hisia za burudani
na kustarehesha kwa matumizi ya simulizi,
nyimbo, ngano, vitendawili na maigizo. Lakini
tutazamapo fasihi simulizi yoyote ile, tunaona
kwamba haikosi kufundisha jambo, au
kimakusudi ama kisadfa.
Fasihi
simulizi ni sanaa
inayotuchorea taswira ya uhalisi wa
maisha ya binadamu, hivyo inawasilisha
hali, maingiliano, mivutano na mikinzano
miongoni mwa binadamu na mazingira yake. Msikilizaji
wa kazi ya fasihi huingiliana na
tajriba za hali inayowasilishwa na wahusika
wa kazi hiyo kama walivyosawiriwa.
Vilevile,
hukata kauli kuhusu ukweli; uhalisi; na
ubora wa yale anayokumbana nayo. Waandishi
wengi hujaribu kusimulia maisha katika
mapana na marefu yake na kwa lugha
teule, ili kugusa hisia za msomaji au
msikilizaji.
Fasili nyingi za fasihi
zimeegemea kuileza katika uhusiano wa fasihi simulizi na jamii. Fasili hizi
zimeonyesha kwamba fasihi simulizi
ni taasisi ya jamii na
uhusiano wake na jamii hauwezi kupuuzwa. Mmoja wa wanaounga mkono dhana hii ni
Escarpit, R (1974:4) anayesema kwamba: Fasihi
hasa simulizi lazima ichukuliwe kama iliyo na uhusiano usiotatanika na maisha
ya kijamii.
Kutokana na maelezo haya tunaweza kuona wazi kuwa fasihi
simulizi katika swala zima la jamii ni kwamba imekuwa kielelezo mwafaka cha
kuona kwamba jamii inakuwa na kuchongeka ifaavyo. Ni ukweli usiopingika kuwa
fasihi simulizi ni kioo cha jamii.Hija hii inapigiwa upato tunaposhuhudia namna
tamaduni, mila, miiko na hali halisi ya maisha katika jamii zetu inavyopitishwa
kutokakizazi kimoja hadi kingine.
Hili linajitokeza katika tanzu mbalimbali za fasihi simulizi
zikiwemo methali, nahau,misemo, mafumbo na kadhalika. kwa mfano methali zipo
zile zenye chuku ambazo hutumiwa sio tu kupamba lugha ambayo ni sehemu ya utamaduni wa jamii bali pia hutumiwa
kuonyesha utabaka wa wanajamii pamoja na shughuli ambazo wana-jamii
wanazozifanya.
Kulingana na Wamitila K.W (2000) anaeleza kuwa chuku ni
udanganyifu au maneno yasiyo ya
kweli. Msemo 'kupiga chuku’
unaelezewa kuwa hali ya kuongezea,
kuzidisha au kuitia chumvi habari
fulani. Katika chuku, huwa kuna
ukweli fulani unaotakiwa kuwasilishwa
ila umejificha ndani kwa ndani kwa kutiliwa
chumvi mno. Mathalani, watu wahudhuriapo
mkutano fulani , hali hiyo inaweza kupigwa
chuku kwa kusemwa hivi: 'Watu walijaa
hivi kwamba hapakuwa na nafasi ya
kutema mate au nzi kupita.’
Ukweli katika kauli
hii ni kuwa mkutano unaozungumziwa
ulihudhuriwa na watu wengi lakini
haiwezekani wingi huo kuikosesha hadhira
nafasi ya kutema mate au nzi nafasi
ya kupita. Chuku imetumiwa hapa kushadidia wingi
wa wahudhuriaji.
Utakuta kwamba methali zilizo na chuku na
vitanza ndimi kwa upande wake zimetumiwa sana katika jamii. Vitanza ndimi ni mbinu
ambayo hujitokeza sana katika mashairi
na methali za jadi. Jamii nyingi
za Kiafrika zilikuwa na mazoea ya kuchezea
maneno katika hali ya kujiburudisha.
Tukitazama kwenye
methali zilizona chuku na vitanza ndimi, tunapata kuwa haliya maisha hasa
utabaka hujitokeza wazi kabisa.Chuku na vitanza ndimi
vilitumiwa katika methali zilizoonyesha na
zinazoonyesha utabaka
miongoni mwa wanajamii mbalimbali, zilizozisuta
tabia fulani kama vile kiburi na
tadi, zilizoonyesha na zinazoonyesha ushirika
katika kazi miongoni mwa nyingine.
Mbinu
hizi zilizifanya methali hizo kuwa na
urefu usiokuwa wa kawaida japo zimeendelezwa kwa
kifupi katika kamusi za methali . Mfano : Kuku
wa mkata hatagi na akitaga
haangui na akiangua vifaranga huchukuliwa
na mwewe. Watu wengine huisema methali
hii hivi: Kuku wa mkata, kata na
akita haangui na akiangua, vifaranga huchukuliwa
na mwewe.
Vitanza ndimi(ambavyo ni sehemu ya
mojawapowa vipera vya fasihi simulizi) katika
methali hii ni mkata, kata, akita ,
taga angua na vifaranga. Jamii nyingi za Kiafrika
ziliuchukulia umaskini kama hali ya
majaliwa. Ulimnyima mwanajamii uwezo wa
kushiriki katika shughuli za kiuchumi
katika jamii yake. Ilisadikika kuwa
maskini asingeweza kufanikiwa kwa vyovyote
vile na katika lolote alilokusudia
kulifanya licha ya kutia juhudi.
Kutokuwa na uwezo wa
mtu maskini kumepigwa chuku sana
katika methali hii. Hali hii pengine
ndiyo inayotudokezea kwa nini pengo kati
ya walalahoi na walalaheri
liliendelea kupanuka kila uchao katika
jamii kwa ile kasumba iliyoyatawala
mawazo ya Mwafrika kuwa umaskini wake
ulikuwa kudura kutoka kwa Maulana.
Chuku katika methali
hii inatekeleza dhima ya
kutudhihirishia kuwa ni muhali sana
kwa mtu maskini kuweza kufanikiwa
maishani kwa sababu ya hali
tofauti zinazomzunguka kama vile uwezo wake
mdogo, ukosefu wa raslimali muhimu ,
kudhulumiwa na mwenye nguvu ambaye
hapa analinganishwa na mwewe na
kasumba yake mwenyewe.
Kupitia kwenye mifano hii, ni wazi kuwa jamii husika
inaweza kupitisha na kirithisha amali zake mbalimbali kwenye kizazi kipya.
Urathi huu ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha kuwa
jamii inazidi kuwa na mwelekeo ufaao wa kimaisha.
Vile vile fasihi simulizi tangu awali hadi sasa imekuwa
mbinu bora zaidi ya kuwafundisha wanajamii.Tukitazama hapo awali, tanzu
mbalimbali za fasihi simulizi zilikuwa zikitolewa kulingana na muktadha wa
tukio husika. Kwa mfano nyimbo ziliimbwa kulingana na matukio husika. Baadhi ya
matukio yaliyoangaziwa katika Nyimbo ni
kama zile Nyimbo za tohara(nyiso) katika
jamii ya Wabukusu.
Nyimbo hizi zilifunzwa na wakongwe hasa nyakanga au kungwi katika swala zima la kuwaandaa vijana wa
kiume katika mpango mzima wa kuwadariji kutoka utotoni hadi ukubwani. Zilikuwa
na maudhui ya kuwafanya kuwa na ujasiri wa kukutana na kisu cha ngariba pamoja
na Kuwapa kitambulisho cha kuwa wana-jamii waliokamilika. Wale walioonekana
kuwa waoga vile vile waliimbiwa zaoza kuwakejeli kadamnasi ya jamii. Kwa
kufanya hivyo jamii husika iliweza kuwarithisha wanajamii tamaduni na mila zao
katika shughuli kama hizo.
Fasihi simulizi vile vile imekuwa katika mstari katika
kuielekeza jamii huku ikiimarisha wajibu
wa wanajamii mbalimbali.Kupitia tanzu mbalimbali za fasihi simulizi, jamii imewezakuelewa wajibu wao kikamilifu.
Hililimewekawaziwajibu wakila mmoja katika jamii awe mtoto wa kike,kiume, mzazi
wa kiemeau kike n.k.
Vijana Wavulana walipewa mafunzo bora ya kuwawezesha
kuwa mstari wa mbele katika Kuhakikisha kuwa majukumu yote ya kiume yanatiliwa
mkazo kabisa. Hii ilikuwa pamoja na kuilinda jamii kutokana na mashambilizi ya
kila aina,
Fasihi simulizi vile vile ni hazina kubwa ya kuhifadhi
historia ya jamii.Hii inajitokeza katika masimulizi ya majagina kama Fumo
Lyongo, Luanda Magere na kadhalika. Kupitia kwa masimulizi haya jamii
inajitambua vyema kule ilikotoka, namna ilivyokuwa na kule inakodhamiria kuenda katika siku zake za halafu.
Methali
ni miongoni mwa kauli teule zinazotumiwa katika mawasiliano ya jamii. Kila
jamii huwa na methali zake. Kwa sababu, methali zimefundika hekima na hutumiwa
katika kuelimisha, kubainisha na kuhifadhi falsafa ya watu katika muktadha wa
utamaduni. Vile vile, methali zinapotumiwa huufanya ujumbe unaowasilishwa kuwa
bayana, kueleweka na kuweza kufafanuliwa kwa kuzingatia uhalisi wa maisha. Kwa
kuzingatia hayo, ujumbe katika methali hupata ufasiri usiokuwa na utata.
Kimsingi
methali ni zao la utamaduni na hazijafungika katika ufinyu wa mawasiliano ya
jamii (Parker, 1972). Kwa hivyo, methali huweza kupatanishwa na takribani kila
kipengele katika maisha ya watu. Kutokana na umaarufu wake katika mawasiliano
ya watu, zimekuwa zikirithishwa na kutumiwa kimapokeo kutoka kizazi kimoja hadi
kingine. Kadhalika, methali hujibainisha zaidi katika tamathali za usemi ambapo
huwa ni kauli za kimafumbo zitumikazo katika kufafanua maswala ya uadilishaji
na uielekezaji wa wanajamii kuhusu maisha.
Ni
katika muktadha huu ambapo hadhira huhitaji kupiga bongo ili kuweza kuupata
uzami wa ujumbe unaowasilishwa. Kulingana na Wamitila (2000) na Wafula (1994),
methali ni kauli zilizokubalika katika utamaduni wajamii. Isitoshe, methali ni
kauli ambazo zimejengeka katika miundo mahususi inayotambuliwa na kukumbukwa
kwa urahisi. Kwa hivyo, hutumiwa kwa malengo ya kuwaelekeza, kuwasuta,
kuwakejeli na kuwashauri watu.
Endapo
maswala yanayoshughulikiwa yanagusia hisi; ujumbe huo huwasilishwa kiistiari,
kitashihisi, kitashibihi, kijazanda na kitaswira ili kuepukana na kutonesha
hisi za wale wanaohusika.
Kimapokeo,
methali zimekuwa zikitumika katika mawasiliano ya kila siku kutokana na
tajiriba inayotokana na utamaduni na uhalisi wa maisha. Kwa hivyo, ni kauli
zinazoweza kutumiwa katika mawasiliano ili kupatanisha ujumbe unaoibuliwa na
yale yaliyopo katika jamii. Tangu jadi, tamaduni za kilimwengu zimekuwa
zikitilia mkazo maswala ya umoja na utangamano.
Hayo
ni baadhi ya mambo ya msingi ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele siyo tu katika
jamii hizo za awali bali pia katika jamii za sasa. Wanajamii wamekuwa wakiunda
kauli mbalimbali katika uwasilishaji wa swala hilo. Isitoshe, methali
zinapotumika kwa mwafaka huusisitiza zaidi ujumbe unaowasilishwa. Kadhalika,
methali hutumika katika kutekeleza mambo mawili: kubainisha na kuwaelekeza
watu.
Matarajio
ni kwamba, watu waweze kuzingatia busara inayoibuliwa na zaidi kuchukua hatua
inazostahili ili kujenga mahusiano ya ushirika, upendo na amani kama
ilivyodhinishwa katika utamaduni wao. Katika muktadha migogoro na migaragazo ya
kijamii, kisiasa na kiuchumi ambayo imekuwa ikishuhudiwa kila kuchao katika
jamii imejengewa muktadha wa kurejelea katika methali zilizopo.
Methali vile vile hutumiwa katika sala zima
la kudhihirisha amali za kijamii . Mfano ni methali isemayo , 'Kinyozi hajinyoi
na akijinyoa hajitakati na
akijitakata hujikata’. Kihunzi katika
methali hii kimeegemezwa katika
maneno kujitakata na kujikata. Methali
yenyewe inatilia chumvi hali ya
kinyozi mzoefu wa kuwanyoa wengine
kukosa uwezo wa kujinyoa.
Pale ambapo kinyozi
mwenyewe atajibidiisha kujinyoa huenda
asifikie usafi unaohitajika na iwapo usafi
huo utafikiwa, basi kinyozi huyo
atajikata. Dhima ya chuku katika
methali yenyewe ni kutudhihirishia
kwamba hapana mtu hata mmoja ambaye
anaweza kujidai kuwa mjuzi wa kila
jambo kwani uwezo wa binadamu una
kikomo.
Lengo kuu la matumizi ya chuku
na vitanza ndimi katika methali za
Kiswahili lilikuwa ni kuburudisha ,
kufurahisha na kuteka nadhari ya hadhira
ili iweze kupata ujumbe uliojitokeza
katika methali zenyewe. Mbinu hizo aidha
'ziliutohoa’ na kuuficha ukali ambao
iwapo ungesemwa bayana, ungeibua
hisia kali.
Kwa yakini na si yamkini fasihi simulizi ni taasisi ya kijamii, inayotumia lugha kama
mtambo wake. Isitoshe, fasihi simulizi huwakilisha maisha. Maisha kwa upana wake
huhusu uhalisi wa kijamii, hata ingawa ulimwengu halisi na hata ulimwengu wa
ndani wa mtu binafsi ni mambo yanayoweza kuzingatiwa katika fasihi. Mbali na
hayo twafahamu kwamba iwapo fasihi simulizi hulenga watu fulani, basi bila
shaka hiyo fasihi yahusu jamii fulani lau sivyo hapana haja kutungia watu kazi
isiyowahusu ndewe wala sikio.
Jambo jingine la kutaja hapa
ni kwamba mtunzi mwenyewe wakazi ya fasihi simulizi ima yawe mafumbo, ngano,
nyimbo n,k ni mwanajamii kwa ambavyo ana nafasi na tabaka fulani katika jamii
yake; yeye hutambuliwa na jamii kama mmoja wao. Hawezi kuepuka nafasi hiyo yake
katika jamii wala hawezi kukwepa athari ya jumuiya katika utunzi wake kwani
kama mtoto mchanga yeye anafundishwa maadili na itikadi za jamii yake ili kuweza
kuenea katika jamii hiyo. Na kama ambavyo tumetaja tayari, mtunzi hulenga
hadhira fulani hata iwe ndogo vipi.
Mara nyingi fasihi hutokana
na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za kijamii. Taasisi za kiuchumi,
kisiasa, na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na utoaji wa fasihi na
kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyengine, hudhihiri ukweli huu. Maendeleo
na mabadiliko ya jamii yametokea kuwa maendeleo na mabadiliko ya fasihi hivi
kwamba hatuwezi kutenganisha fasihi na jamii inamoibukia. Uhusiano huu unatokea
kwa sababu pindi maisha ya jamii yabadilikapo, mielekeo, tamaduni na hata
maadhili ya jamii hubadilika pia. Aidha, mabadiliko ya fasihi toka simulizi
hadi andishi ni zao la mabadiliko katika maisha ya jamii ambapo taaluma ya
kusoma na kuandika ilitokea. Kwa hivyo fasihi inalo jukumu kuu katika jamii
ambalo sio la kibinafsi, bali ni la kijamii. Katika kuiunga mkono kauli hii,
Wellek na Werren (1949:95) wanasema kwamba: Uhusiano kati ya fasihi ima iwe
Andishi au simulizi na jamii hujadiliwa
kwa kuanza na kauli aliyoitoa De Bonald kwamba `fasihi ni kielelezo cha
jamii'.
Kwa hivyo ni muhimu
kuichukulia fasihi kama zao la jamii ambalo pia huathiri na kuathiriwa na
jamii. Hata katika nyingi za tahakiki za fasihi ambazo twaweza kuziita za
kijamii (kama za Ki-marx) pamesisitizwa kauli kwamba mtunzi anapaswa kuendeleza
maisha ya wakati wake kwa ujumla wake; kwamba anapaswa kuwa kiwakilishi cha
wakati wake na jamii yake. Kwa maoni ya waitifaki wa tahakiki hizi,
`uwakilishi' huelekea kumaanisha kuwa mtunzi anapaswa kutambua na kuona hali
halisi za maisha katika jamii yake na kuzizingatia katika utunzi wake. Maoni ya
Hegel na Taine katika Wellek na Warren (1949:95) ni mfano unaochangia zaidi
kauli hii wanaposema:
Katika uhakiki wa Kihegel na hata ule wa Taine, utukufu
wa kijamii na wa kihistoria huenda sambamba na utukufu wa kisanaa. Msanii huendeleza
ukweli, na
huo ukweli ni wa kijamii na kihistoria. Tunaloweza
kuongeza ni kwamba pana tatizo linalokumba juhudi yoyote ya kujaribu kutenganisha fasihi na jamii kwani
fasihi huathiriwa na mandhari ya kijamii
pamoja na mabadiliko na maendeleo yake. Isitoshe, mtunzi ni mwanajamii
anayetumia lugha ya jamii kutunga kazi yake ili kuwafifikia wanajamii husika.
Ukweli huu wanaogusia waandishi hawa utategemea mtizamo, matarajio, na tajiriba
za anayehusika kwani hali mbali mbali
katika jamii hutoa maana mbali mbali kwa watu mbali
mbali hata kama ni wa
jamii moja. Hivyo basi ukweli hubainika tu
kimuktadha.
Wale wanaosisitiza kigezo
cha fasihi na jamii katika kuieleza fasihi, wametoa kauli kwamba pana aina
mbali mbali za fasihi ambazo zinachukuana na jamii mbalimbali. Dhana kama vile
fasihi ya kirusi, fasihi ya kiafrika, fasihi ya kiingereza n.k. ni baadhi ya
mifano ya kazi za fasihi zinazohusishwa na jamii fulani. Fasihi kama hizi
hulenga jamii fulani pana zenye kaida na maadili yanayopatana katika muundo wa
kijumla kwani katika jamii hizo huwa kuna vijamii vidogo vidogo. Kwa mfano
katika fasihi ya Kiafrika pana fasihi ya jamii ya nchi mbali mbali ambazo
zimeibuka kihistoria kwa jinsi maalum ambao ni tofauti na ya nchi nyengineyo.
Na katika nchi hizo pana
vijamii vingine vidogo vidogo vinavyobainishwa na lugha, mazingira, na itikadi.
Hivyo kutaja kwamba pana fasihi ya kirusi ni kutoa kauli ya kijumla tu. Vile
vile pana fasihi zinazochukuana na mifumo mbali mbali ya maendeleo ya kijamii
kama vile fasihi ya kibwanyenye, fasihi ya kisosholisti, fasihi ya
kikapitolisti n.k.
Ama kwa hakika mojawapo ya
majukumu ya fasihi ni kule kuihifadhi historia ya jamii husika. Yaani kwa
kuitazama kazi ya fasihi twaweza kupata picha maalum ya historia ya jamii
husika. Kwa mfano katika fasihi ya kiswahili twaweza kupata vipindi maalum vya
kihistoria, Mashetani (Ebrahim Hussein) ni mfano wa Kipindi
cha Ukoloni-Mamboleo, na utenzi wa Al-Inkishafi (Sayyid
Nassir) ni kielelezo cha historia ya Mji wa Pate. Hivyo basi twaona kwamba
kauli kuwa fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii ni dhana yenye mashiko
sana.
Hata hivyo hatulengi kusema
kwamba kazi ya fasihi ni hitoria kwa kule kuhitajika kutoa picha halisi ya
maisha ya wakati husika, kwani japo mada ni matukio halisi ya kihistoria, namna
ya kusawiri mada hizo na matini maalum (kati ya mengi) yaliyozingatiwa, ndiyo
yaibainisha kama kazi ya fasihi. Maoni yaliyotolewa hapa ni mwongozo wa
kuitazama fasihi katika vigezo ambavyo bila shaka huathiri fasihi.
Iwapo tutakubali kwamba kazi
ya fasihi simulizi si amali ya mtu
binafsi, basi tutakuwa tayari tumeonyesha kwamba fasihi na jamii ni vitu
visivyotengana. Na hata pakitokea kwamba maisha ya mtu binafsi yametumiwa kama
nguzo ya kutunga kazi ya fasihi, hatuwezi kusahau kwamba tajiriba zake
zimepaliliwa na maisha yake kama mwanajamii, awe anachukua au kukiuka maadili
na matarajio ya jamii hiyo.
Hitimisho.
Kutokana
na ufafanuzi huu, tunaweza kusema kuwa fasihi simulizi ina uhusiano mkubwa na
utamaduni. Maana kati ya vipengele vya utamaduni kimoja ni lugha. Lugha kama
sehemu ya utamaduni ina tabia ya kuwapambanua watu. Japo siku hizi kuna jitihada ya watu kujifunza
lugha mbali mbali, lakini lugha ya kujifunza haiwi yako, na mara nyingi wenyeji
wa lugha hiyo uliyojifunza huweza kujua kuwa wewe si mmoja wao.
Kwa kuwa lugha ni kipengele kimojawapo cha
utamaduni, na kwa kuwa fasihi hutumia lugha, basi fasihi na ni sehemu ya
utamaduni. Na iwapo utamaduni ni utashi na uhai wa taifa, ni mti wa mgongo wa
taifa, basi hapana budi fasihi nayo kuwa sehemu ya uhai na utashi wa jamii
hiyo.Fasihi (na maelezo haya yaweza
kuingia katika fasihi kwa jumla, fasihi maandishi na fasihi simulizi) si sehemu
tu ya utamaduni, bali ni chombo cha utamaduni pia. Ndiyo chombo cha kukuzia,
kuhifadhia, kuendelezea na kuelezea huo utamaduni. Ni chombo cha pekee kati ya
taaluma mbali mbali za utamaduni. Hutokea hivyo kwa kuwa taaluma hii huhusika
na jinsi lugha inavyosema na jambo linalosemwa. Kwa hivyo hutoa tafsiri mbali
mbali ambazo pengine taaluma zingine hushindwa kuzitoa.
Marejeleo
o Kirumbi, P. S. 1975. Misingi ya Fasihi
Simulizi. Nairobi: Shungwaya Publishers.
o Matteru, M. D. 1983. Fasihi Simulizi na
Uandishi wa Kiswahili, katika Fasihi: Makala za Semina ya Kimataifa ya
Waandishi wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI. Uk. 26 – 37.
o Mlacha, S. A. K. 1995. Fasihi Simulizi na
Usuli wa Historia ya Pemba. Katika: Lugha, Utamaduni na Fasihi Simulizi ya
Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI/ITAA. Uk. 16-26.
o Msokile, M. 1992. Kunga za Fasihi na Lugha.
Kibaha: EPD.
o Wamitila K. W. 2003. Kamusi ya Fasihi:
Istilahi na Nadharia. Nairobi, Kenya: Focus Publications. Wamitila, K. W. 2003.
Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Fasihi. Nairobi, Kenya: Focus Publications.
o Gazeti la Mtanzania la tarehe 13.06.03.
o Kimani N. 2006. Fasihi Simulizi na Nadharia
ya Fasihi ya Kiafrika, katika Fasihi ya Kiswahili. Nairobi: Twaweza
Communications. Uk. 1 – 10.
o Senkoro, Fikeni (2004b). “The role of
language in education and poverty alleviation: Tool for access and empowerment”
in Justian Galabawa and 20 Anders Narman Education Poverty and Inequality
(eds), DSM: KAD Associates. (pp 46-58).
o Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi
Simulizi: Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.
o Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi
Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
o Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi,
Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd.Nairobi.
o TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
(Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi
wa Kiswahili (TUKI).
Comments
Post a Comment