STADI ZA UKALIMANI
STADI ZA UKALIMANI
1.0 Utangulizi
Kazi hii imegawanyika katika vipengele mbalimbali kama vile; ukalimani na teknolojia, matumizi ya teknolojia katika ukalimani, stadi za msingi katika ukalimani ambazo ni kunukuu, kusikiliza, kuzungumza na kuzungumza hadharani. Kadhalika stadi za ziada katika ukalimani kama vile, kuficha dosari za msemaji chanzi, kusema jambo lilelile kwa maneno mengine na kupitisha muda. Kimsingi, vipengele hivyo vimefafanua kwa kuoneshwa namna vinavyotumika katika taaluma ya ukalimani, na mwisho tumehitimisha kazi.
2.0 Ukalimani na Teknolojia
Kimsingi, hapa mkalimani hutumia teknolojia ili kukamilisha mchakato wa kukalimani vizuri. Mbillow (2017) anaeleza kuwa, ukalimani na teknolojia unaweza kusemwa kwa namna mbili. Mosi, ni kutumia vifaa au mashine kufanya shughuli ya ukalimani iweze kufanikiwa kirahisi. Mfano, mtu anaweza kukalimani kwa kutumia simu, kisemeo (microphone), visikizi sikio (earphone) au visikizi kichwa (headphone). Pili, ni matumizi ya vifaa hivyo katika juhudi ya kuchukua nafasi ya binadamu. Hapa inamaana kuwa, wanasayansi wanajaribu kuona kama inawezekana msemaji wa lugha chanzi badala ya kumtafuta mkalimani ili kuwezesha mawasiliano kati yake na mtu asiye wa lugha yake, atumie vifaa vya kiteknolojia.
2.1 Matumizi ya Teknolojia katika Ukalimani
Hii ni moja ya kanuni muhimu katika ukalimani. Back na Ted (1998) wanaeleza kuwa, katika kanuni kumi na tano za mkalimani, matumizi ya teknolojia kwa mkalimani ni kanuni namba nane. Kimsingi, kanuni hii pamoja na mambo mengine inamtaka mkalimani popote alipo kujihusisha na teknolojia katika kuhakikisha anakuwa kileoleo, yaani anapata maarifa kwa kujiendeleza yeye mwenyewe katika kujifunza njia bora na za kisasa za ukalimani. Mbillow (2017) anaeleza kuwa, kanuni hii ni kwa mkalimani kufanya juhudi binafsi kuhakikisha anajua kutumia vizuri vifaa vipya vya kiteknolojia.
Mbillow (2017) anaendelea kueleza kuwa, utumizi wa teknolojia katika ukalimani si kitu cha kuhoji ama kuuliza mara mbili hasa kwa maendeleo ambayo dunia ya leo imeyafikia. Mill na Tilden (1967) wakinukuliwa na Beck na Cable (1998) wanadai hakuna namna mkalimani atakwepa kutumia vifaa vya kiteknolojia, bali yampasa mkalimani kuhakikisha anatumia vizuri vifaa hivyo na kwa uangalifu mkubwa. Aidha, vifaa hivi vya kidigitali au vya kiteknolojia vina faida na vinasaidia sana katika fani hii ya ukalimani.
3.0 Umuhimu wa Matumizi ya Teknolojia katika Taaluma ya Ukalimani
Teknolojia katika ukalimani huwa na faida mbalimbali. Kimsingi, teknolojia humrahisishia mkalimani zoezi lake la kukalimani. Hivyo, yampasa mkalimani kuhakikisha anatumia vizuri vifaa hivyo na kwa uangalifu mkubwa.
3.1 Matumizi ya Teknolojia yanatarajiwa kumnufaisha mkalimani hasa katika kujipatia maarifa.
Mpemba (2013) anaeleza kuwa, ukalimani wa awali ulikuwa ni kipaji tu cha mtu ajuaye lugha zaidi ya moja. Mpemba akimnukuu Giambruno (2008) anadai upo ushahidi unaodai kuwapo kwa ukalimani kuanzia miaka ya 3000 KK katika Bara la Afrika. Kwa upande wa Tanzania ukalimani ulianzishwa miaka ya 1955. Ingawa, hata kabla ya hapo ulikuwepo na baadaye ukapigiwa chapuo sana watangulizi wa wakoloni na baadaye wakoloni wenyewe. Miaka ya 2000 wakalimani wamekuwa wakijiongezea ustadi wao wa kuweza kujiendeleza kupitia mafunzo binafsi kwa tarakirishi. Beck na Cable (1998) wanaeleza faida hii kuwa ubora wa ukalimani wa mkalimani utegemea ujuzi na ufahamu mkubwa wa mkalimani alioupata kutokana na kutumia teknolojia kujiendeleza. Sambamba na hilo mkalimani huweza kujisomea na kushirikiana na wenzake ama wataalamu wengine wa sehemu mbalimbali ulimwenguni ili kumsaidia mkalimani kupata taarifa au habari zinazohusu ukalimani. Kwa sasa hali imerahisishwa sana ya upatikanaji wa vitabu, makala na taarifa nyinginezo na kisha kuzihifadhi mtandaoni kwa lengo la kushirikishana habari au ujuzi au stadi hizo na wengine. Mkalimani hubakia na kazi ndogo tu ya kuwa na kifaa kama tarakirishi au simujanja (Smartphone) au vifaa vingine vyenye uwezo wa kushika mtandao na kuandika ama kutafuta chochote atakacho halafu kwa muda mfupi tu hupata kwa wingi.
3.2 Humsaidia Mkalimani kuhudumia watu wengi kwa pamoja na mara moja
Pochhacker (2004) anaeleza kuwa, kabla ya kukua kwa teknolojia ilikuwa ni ngumu kumuunganisha mzungumzaji, mkalimani na wasilikizaji kirahisi. Kupitia teknolojia ya kusafirisha sauti na video sauti sasa jambo hili ni jepesi kabisa. Pochhacker (k.h.j) anaendelea kusema kuwa awali ilikuwa ni vigumu kufanya ukalimani nong’onezi kwa watu zaidi ya wawili, lakini sasa jambo hili linawezekana hata kwa watu maelfu. Kwani sasa kupitia kisemeo, visambaza sauti/video sauti, visikizi sikio, mkalimani anauwezo wa kuwasiliana na yeyote kupitia teknolojia hiyo. Aina hii ni maarufu kwenye mikutano ya kimataifa na inayojumuisha wazungumzaji wa lugha tofauti tofauti.
3.3 Imewezesha kuongezeka kwa aina za Ukalimani na zilizokuwepo kupata kujipambanua sawasawa
Pochhacker (2004) anaeleza kuwa, mageuzi makubwa yametokea miaka ya 1920 katika ukalimani. Anaendelea kueleza kuwa, kabla ya hapo ukalimani uliokuwa unafanyika ni ule fuatizi, kwa sasa baada ya kukua kwa teknolojia kumewezekana kwa njia sambamba. Yaani mkalimani huenda karibia sawa na mzungumzaji wa lugha chanzi na wasikilizaji. Yote haya yanawezekana kwa sababu tu ya urahisi wa mawasiliano maendeleo makubwa yaliyotokea katika kizazi cha simu, yamepelekea hata viziwi au wenye matatizo ya kusikiliza kuweza kuona kupitia simu zao. Dunia ya sasa imekuwa kama kijiji hivyo mkalimani hana budi kutumia teknolojia iliyopo ili kufanya ukalimani kwa urahisi.
4.0 Stadi za Msingi katika Ukalimani
Hizi ni stadi ambazo husaidia kukamilisha zoezi la kukalimani kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa. Stadi hizi mkalimani hulazimika kuwa nazo ili aweze kumudu zoezi la kukalimani. Stadi muhimu katika zoezi la ukalimani ni:
Lugha na Mawasiliano, mfano kuongea, kusikiliza, kuandika na kusoma.
Stadi ya Kunukuu (recording skills).
Stadi ya Kumbukumbu/kukumbuka (memory rehesion skill).
Stadi ya Kuzungumza hadharani (umahiri wa kuongea vizuri mbele ya hadhira).
4.1 Stadi ya Kunukuu
Kimsingi, katika stadi hii kumbukumbu ya mkalimani inatumika kama kitu cha msingi. Aidha, mkalimani si lazima arudie kilekile kilichoongelewa cha msingi azingatie ujumbe kufika kwa hadhira lengwa. Pia, katika stadi hii mkalimani huwa na karatasi, au kijitabu kwa ajili ya kunukuu baadhi ya semo, ujumbe ili imsaidie katika zoezi la kukalimani.
4.2 Stadi ya Kumbukumbu/Kukumbuka
Pochhacker (2004) anaeleza kuwa, mkalimani anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kukumbuka ili aweze kufanikisha zoezi la kukalimani kwa urahisi. Stadi hii humfanya mkalimani aweze kuzungumza maneno aliyoyasema mzungumzaji kwa kutumia lugha nyingine. Kama mkalimani ataweza kumudu Stadi hii vizuri basi shughuli ya kukalimani itafanyika vizuri na ndani ya muda uliopangwa.
4.3 Stadi ya Kuzungumza
Hii ni stadi muhimu kwa mkalimani kwani humwezesha mkalimani kumudu matamshi sahihi ya maneno. Pia, stadi hii humpa mkalimani uwezo wa kujieleza kwa kujiamini. Mkalimani anapozungumza hana budi kuwa na mtiririko wa mawazo ili aweze kumuunganisha msikilizaji na mzungumzaji, ajue mada inayozungumziwa vizuri ili apate uhuru wa kuchagua na kutumia istilahi inayofaa kwa haraka.
4.4 Stadi ya Kuzungumza Hadharani
Nikitina (2011) anaeleza kuwa, stadi hii humtaka mkalimani kuzungumza mbele ya hadhara. Katika stadi hii mkalimani atatakiwa ajue hadhira lengwa, mada inayozungumziwa,pia atumie misamiati ambao utamuunganisha anayezungumza na wasikilizaji, auhishe hisia za mzungumzaji katika kukalimani. Aidha stadi ya kuzungumza hadharani hufanyika katika maeneo makubwa kwani huusisha watu wengi. Hivyo, mkalimani anatakiwa kumudu vizuri stadi hii kwani anatakiwa kuondoa hofu na kujiamini ili aweze kuzungumza vizuri mbele ya hadhara.
5.0 Stadi za Ziada
Hizi ni stadi alizonazo mkalimani ambazo zinamuwezesha kukamilisha mchakato wa kukalimani. Kimsingi mbinu hizi zipo ndani ya uwezo wa mkalimani hivyo hanabudi kuwa uwezo wa kuficha dosari za msemaji chanzi, kupitisha muda, kusema jambo lile lile kwa maneno mengine.
5.1 Kuficha dosari za Msemaji Chanzi
Hii ni stadi ambayo mkalimani anaitumia kwa kurekebisha makosa madogomadogo ambayo msemaji chanzi anayafanya. Kimsingi makosa hayo mkalimani hulazimika kuyaficha kwa kutumia njia mbalimbali. Mathalani, mkalimani hulazimika kuficha dosari ya mnenaji chasili kwa kuchagua visawe ambavyo vinaendana na utamaduni wa lugha lengwa. Mnenaji chasili huweza kutamka neno ambalo katika utamaduni wake ni sahihi lakini katika utamaduni wa lugha lengwa ikiwa sio sahihi. Hivyo mkalimani hulazimika kuficha hiyo dosari kwa kuchagua kisawe ambacho kinaendana na lugha pokezi.
5.2 Kupitisha Muda
Kimsingi, katika stadi hii mkalimani anapaswa kusawazisha tofauti iliyopo kati yake na mnenaji chasili. Mnenaji chasili huweza kuwa na utaratibu wa kuongea polepole hivyo mkalimani kama amekutana na mnenaji chasili wa namna hiyo hulazimika kurekebisha huo utofauti kwani zoezi la kukalimani hufungamana na muda na pia mkalimani hutumia muda mchache kuelewa na kuhawilisha ujumbe kutoka lugha chanzi, mkalimani huweza kutumia pia baadhi ya maneno ambayo huweka usawazo wa muda.
5.3 Kusema jambo lile lile kwa maneno mengine
Ni mbinu inayotumiwa na mkalimani ili kufikisha ujumbe uleule kwa wasikilizaji bila kupotosha maana husika au maana kutoka lugha chanzi (Mpemba 2017). Mkalimani anaweza kutumia mbinu hii ya kusema jambo hilohilo kwa maneno mengine kwa kuzingatia yafuatayo:
Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.
Awe na ujuzi na maarifa ya kutosha juu ya mada husika. Mfano, wewe ni mkalimani wa sheria hupaswi kukalimani masuala ya uchumi kwa hiyo mkalimani akijua mada husika vizuri anaweza kusema jambolile lile kwa maneno mengine.
Mkalimani anaweza kusema jambo lilelile kwa maneno mengine kama atakuwa na kipaji au uwezo wa kumbukumbu wa hali ya juu, kuteua msamiati sahihi kwa haraka na kuunda Istilahi inayotakiwa haraka na kuitumia.
Kama mkalimani akiwa mchapakazi, mdadisi na anayependa kutafuta habari katika vyanzo mbalimbali kama magazeti, vitabu na mitandao ya kijamii anaweza kujua istilahi zaidi na kujua wakalimani wengine wanafanya nini na wanafanya vipi. Hivyo atakuwa na uwezo wa kukalimani mada kwa mawanda mapana.
6.0 Hitimisho
Stadi za msingi za ukalimani na stadi za ziada zote zina umuhimu kwa kuwa humsaidia msikilizaji kuweza kusikiliza, kunukuu, kukumbuka na pia kumwezesha mkalimani kuficha dosari za msemaji chanzi na kusema jambo lilelile kwa maneno mengine. Hivyo basi, katika mchakato wa kukalimani, mkalimani na msemaji chanzi wanatakiwa kuijua mada vizuri ili wasipishane katika kufikisha ujumbe kwa wasikilizaji.
MAREJELEO
Beck, L. & Cable, T.T. (1998). Interpretation for the 21st Century: Fifteen Guiding Principles for Interpreting Nature and Culture. Champaign, IL: Sagamore Publishing.
Mbillow, S. N. (2017). Matumizi ya Teknolojia katika Ukalimani. (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mpemba, T. (2013). “Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho” Kiswahili: Juz. 76, uk. 112-140.
Mpemba, T. (2017). “Kufasiri, Kukalimani na Kurudufu Matini kwa Lugha nyingine: Tulipotoka hadi tulipo Sasa.” Kioo cha Lugha: Juz 13, uk.5-6.
Nikitina, A. (2011). Successful Public Speaking. United State: Bookborn & Ventus Publishing.
Pochhacker, F. (2004). Introducing Interpreting Studies. New York/Canada: Routledge.
Comments
Post a Comment