Mbinu za ukalimani
Mjadala kuhusu mbinu za ukalimani.
Ukalimani fululizi
Ukalimani fuatizi
Ukalimani nong’onezi
Ukalimani changamani
Ukalimani pokezi
Ukalimani tazamishi
MBINU ZA UKALIMANI
Utangulizi
Insha hii imegawanyika katika sehemu kuu nne ambazo ni; utangulizi, kiini, hitimisho na marejeleo. Sehemu ya utangulizi ni maelezo kuhusiana na mgawanyiko wa insha hii pamoja na fasili ya ukalimani, sehemu ya kiini ni mbinu za ukalimani, sehemu ya hitimisho ni mawazo ya jumla kuhusiana na insha kisha vyanzo mbalimbali vilivyotumika kusheheneza insha hii, vimewekwa katika sehemu ya marejeleo.
Dhana ya Ukalimani
Wanjala (2011:14) anaeleza kuwa ukalimani ni kitendo cha kuhawilisha ujumbe katika mazungumzo kutoka lugha chasili hadi lugha lengwa. Katika fasili hii, jambo la muhimu linalodokezwa ni kwamba, ukalimani unahusu uhawilishaji wa lugha ambayo ipo katika mazungumzo. Hata hivyo, kwa maoni yetu, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia fasili ya ukalimani inapevuka na kuvuka mipaka ya kuonwa kwamba lazima matini chanzi iwe katika mazungumzo bali matini chanzi inaweza kuwa katika maandishi mjongeo, mathalani ukalimani unaofanyika katika luninga. Huu ni ukalimani kwa sababu mkalimani hufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya mazungumzo ilhali akiwa ametoa ujumbe huo katika maandishi yanayojongea kama anavyodai Mpemba (2013:116) kwamba, “kwa kuzingatia madai kuwa kukalimani ni kutafsiri mazungumzo, kunazibagua aina kadhaa za ukalimani kama ule wa kutumia lugha za alama na ule wa soga za mtandaoni”.
Pöchhacker (2004) anaona ukalimani kama aina fulani ya tafsiri ambapo matini lengwa hutolewa mara moja tu katika muda finyu na kwa ajili ya matumizi ya muda wa wakati huohuo. Fasili hii haitofautiani sana na ile ya Kade (1968) anapodai kwamba ukalimani ni aina fulani ya tafsiri ambapo matini chanzi huwasilishwa mara moja pekee na hivyo haiwezi kupitiwa upya, kuchezewa upya au kurudiwa. Pöchhacker (keshatajwa), anaongeza kuwa, matini lengwa hutolewa katika muda finyu huku kukiwa hakuna au kuna fursa ndogo sana ya marudio au masahihisho. Wataalamu hawa wameitanabaisha taaluma ya ukalimani na tafsiri kwa kuiona taaluma ya ukalimani kama matokeo ya taaluma ya tafsiri jambo ambalo si kweli kwani hizi ni taaluma mbili tofauti zinazofanya kazi zinazofanana.
Nolan (2005:2), tofauti na wataalamu wengine juu, anaona ukalimani ni ufikishaji wa uelewa. Pamoja na ubora wa fasili hii, bado ni finyu sana kwani uelewa unaweza kufikishwa kwa namna nyingi ambayo inaweza isiwe ni ukalimani mathalani, kwa njia ya maandishi ama njia nyingine tofauti na ukalimani.
Kwa ujumla, ukalimani ni uhawilishaji wa ujumbe au maudhui yaliyo katika lugha ya mazungumzo na maandishi mjongeo kwenda katika lugha lengwa kwa njia ya mazungumzo ambapo huhusisha alama na ishara, mijongeo ya mwili, mktadha maalumu na matukio kwa haraka zaidi. Ukalimani huinufaisha hadhira lengwa papo kwa papo tofauti na tafsiri ambayo inaweza kuchelewa kumfikia mhusika.
Mbinu za Ukalimani
Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kuhusiana na istilahi za ukalimani, mathalani kwa umahusisi istilahi ‘mbinu’ ‘aina’ na ‘mikabala’. Mkanganyiko huu unatokana na sababu kwamba istilahi hizi zimekuwa zikitumiwa na wataalamu kwa namna tofautitofauti huku wakisigana katika matumizi na maana muafaka ya istilahi hizo. Kutokana na kiini cha mjadala wa insha hii, istilahi ‘aina’ na ‘mbinu’ ndizo zilizojadiliwa kwa ufupi katika kipengele hiki kisha kuhitimisha kwa kupendekeza istilahi ipi itumike wapi na kwa nini.
Wanjala (keshatajwa:35) na Mshindo (2010:30) wanatumia istilahi ‘aina’ kueleza zile walizoziita aina na ukalimani kuwa ni ukalimani andamizi (fuatizi) na ukalimani mtawalia (fululizi/ papo kwa papo/ sambamba/ sawia) pasi na kueleza vigezo walivyotumia kuainisha. Kadhalika, Mwaituka (2012:15), hatofautiani na Wanjala na Msindo kwa kutumia istilahi ‘aina’ kurejelea zile alizoziita aina za ukalimani kuwa ni ukalimani wa papo kwa papo na ukalimani fuatizi. Naye Mpemba (2017:19) katika kujadili nadharia ya ukalimani ya jitihada, ametumia istilahi ‘aina’ kurejelea kile alichokiita aina za ukalimani zinazotokana na nadharia ya jitihada kwamba, ni ukalimani sawia, ukalimani fuatizi na ukalimani tazamizi ambapo pia matini andishi hutumika. Nao, Gemino Specialist Information- GSI (2015:2) wametumia istilahi ‘aina’ (types) kurejelea kile wanachokiita aina za ukalimani, ambazo ni; ukalimani fuatizi, ukalimani fululizi, ukalimani nong’onezi na ukalimani changamani.
Tofauti na wataalamu hapo juu, Merinyo (2014:40) ametumia istilahi ‘mbinu’ kurejelea mbinu za ukalimani ambazo ni; ukalimani sambamba na ukalimani fuatizi. Kadhalika, National Association of Judiciary Interpreters ant Translators-NAJIT (2006) wanatumia istlahi ‘modes’ kurejelea mbinu za ukalimani ambazo ni ukalimani fuatizi, ukalimani fululizi na ukalimani tazamishi (sight interpreting). Nao, Trans Cultures- TC (2007) wanatumia istilahi ‘technique’ kurejelea zile wanazoziita kuwa ni mbinu za ukalimani yaani; ukalimani fululizi, ukalimani fuatizi, ukalimani nong’onezi, ukalimazi na tazamishi.
Aidha, Pöchhacker (keshatajwa) katika kubainisha aina za ukalimani, ametumia vigezo viwili; kigezo cha muktadha na kigezo cha muundo wa lugha. Katika kigezo cha muktadha anabainisha aina sita za ukalimani ambazo ni ukalimani wa kijamii, ukalimani wa mahakamani, ukalimani wa mikutanoni, ukalimani wa tiba, ukalimani wa habari (vyombo vya habari) na ukalimani sindikizi. Pia, katika kigezo cha muundo wa lugha anaainisha aina mbili za ukalimani ambazo ni ukalimani wa lugha ya kusemwa na ukalimani wa alama.
Mitazamo ya wataalamu hawa inakanganya na kutoa fursa ya kuchunguza hasa ipi ni istilahi muafaka kutumika katika mazingira fulani ili kumaanisha jambo fulani. Tunaungana na wataalamu wanaoona kwamba istilahi ‘mbinu’ ni muafaka zaidi hurejelea njia (namna) ya ukalimani unavyofanyika, kama TUKI (1981: 328) wasemavyo kwamba, ‘mbinu’ ni njia (namna) ya utekelezaji wa jambo. Hivyo, mbinu hizo ni ukalimani fululizi, ukalimani fuatizi, ukalimani nong’onezi, ukalimani changamani, ukalimani pokezi na ukalimani tazamishi. Aidha, tunaona kwamba istilahi ‘aina’ itumike kurejelea makundi mbalimbali ya ukalimani, ambayo yanaweza kugawanywa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, mathalani kigezo cha muktadha ambapo tunapata ukalimani wa kijamii, ukalimani wa mahakamani, ukalimani wa mikutanoni, ukalimani wa tiba, ukalimani wa habari (vyombo vya habari) n.k. Pia, katika kigezo cha muundo wa lugha tunapata aina mbili za ukalimani ambazo ni ukalimani wa lugha ya kusemwa na ukalimani wa alama, Pöchhacker (keshatajwa). Ufafanuzi huu utasaidia kuondoa mkanganyiko huu.
Baada ya kujadili kwa ufupi mkanganyiko wa istilahi ulioelezwa sehemu zilizotangulia, sehemu ifuatayo inajadili na kufafanua mbinu mbalimbali ambazo hutumika katika mchakato wa ukalimani. Mbinu hizi hutofautiana kutokana na uhitaji kwa muda husika, mabadiliko ya sayansi na teknolojia na sababu nyingine.
Ukalimani Fululizi/ Papo kwa Papo/ Sambamba/ Mtawalia/ Sawia
Nolan (2005:3) anaeleza kuwa, katika mbinu hii, mara nyingi mkalimani hukaa katika chumba maalamu kisichopitisha sauti kiitwacho kizimba na huzungumza kupitia kipaza sauti ambacho hupeleka mawimbi sauti sehemu husika kwa lugha lengwa. Mkalimani huwa anaupata ujumbe kutoka kwa mzungumzaji kupitia visikizi kisha kuukalimani ujumbe huo wakati huohuo na kusafirishwa hadi kumfikia msikilizaji kwa njia ya visikizi. Kutokana na sababu kwamba ukalimani huu ni wa haraka zaidi, inamuhitaji mkalimani kuwa makini na mwepesi wa kufikiri, kama wasemavyo NAJIT (wameshatajwa) kwamba katika ukalimani fululizi, mkalimani anapaswa kusikiliza kwa umakini kila jambo linalosemwa kisha alikalimani jambo hilo kwa haraka na ufasaha.
Aidha, Merinyo (keshatajwa: 40) anaongeza kuwa katika mbinu hii ya ukalimani, wakalimani kubadilishana walau kila baada ya dakika 20 au 30 ili kupeana nafasi ya kupumzika. Kutokana na maelezo hapo juu, inadhihirisha kwamba ukalimani huu hufanyika katika sehemu za mikutano ambayo hujumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali wanaozungumza lugha tofauti. Pia, hutumika katika Mahakama za kimataifa, kama ilivyokuwa kwa Mahakama ya Nurenberg ambapo katika kesi hiyo zilitumika lugha nne katika mawasiliano yaani; Kijerumani, Kingereza, Kifaransa na Kirusi, Gaiba (1998) na Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Mbinu hii inahusisha pia ukalimani wa lugha ya alama katika luninga.
Ukalimani Fuatizi/ andamizi
Kwa mujibu wa Giles (2009:259), huu ni ukalimani ambao mkalimani husubiri mzungumzaji amalize kuzungumza kisha naye hufuata. Mkalimani hukalimani baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde kadhaa. Pia, Katika mbinu hii mkalimani na mzungumzaji aghalabu huwa pamoja wakiwa wamesamama jukwaani ama kuketi mezani na kutimiza jukumu hilo la ukalimani. Wanjala (keshatajwa: 35) anongeza kwa kusema, “katika ukalimani fuatizi (andamizi), mkalimani ana walau muda wa kuchunguza ujumbe kabla ya kuukalimani na hutegemea sana kile anachokisikiliza kwa mzungumzaji”. Mbinu hii ya ukalimani haina ulazima wa kutumia vifaa vya kielektroniki isipokuwa kwa sehemu zenye watu wengi na hutumika sana katika mazingira ambayo ni nusu rasmi-si rasmi mfano katika mikutano ya kiinjili, mikutano ya kisiasa na mikutano ya kijamii. Aidha, mbinu hii inamruhusu mkalimani wakati mwingine kuandika katika karatasi baadhi ya vitu ili asisahau na huchukua urefu wa kuanzia sekunde 5 hadi dakika 1 kumsikiliza mzungumzaji. Kutokana na maelezo haya, ni wazi kwamba mbinu hii hujumuisha ukalimani wa luninga na ndio ukalimani ambao umeenea sana nchini na duniani kote ikilinganishwa na mbinu nyingine.
Ukalimani Nong’onezi
Nolan (keshatajwa: 4), anaeleza kuwa ukalimani nong’onezi ni mbinu ambapo mkalimani hukaa pembeni mwa mlengwa anayefikishiwa ujumbe na kumkalimania kile anachokuwa akikisikiliza kutoka kwa msemaji. Sauti ya mkalimani huwa ni ndogo na haipaswi kusikika kwa mtu asiye husika. Mara nyingi mbinu hii hutumika katika mikutano ya kibiashara ingawa inaweza kutumika katika mahakama, kituo cha polisi na sehemu nyingine zinazoruhusu ukalimani huu kufanyika. Aidha, Pöchhacker (2004:19) anaongeza kuwa ukalimani nong’onezi hufanyika kwa sauti ndogo na wakati mwingine huweza kufanyika kwa kutumia vifaa vidogo wezeshi mathalani visikizi japo utekelezwaji wake hauathiri watu wengine wasiohusika. Akisheheneza maelezo kuhusu mbinu hii, Nolani (2005:4) anaeleza, sauti ya mkalimani haipaswi kabisa kumwathiri mtu ambaye hausiki isipokuwa yule anayekalimaniwa tu. Hii inaonesha kwamba ukalimani huu hauhitaji mabadilishano kwani kufanya hivyo kunaweza kuathiri mchakato wa ukalimani.
Ukalimani Changamani
Tirosh (2020), anaeleza kwamba hii ni mbinu inayohusisha mbinu za ukalimani zaidi ya moja katika muktadha ulele. Mbinu hii hutumika katika mikutano ambayo huwa na wazungumzaji wa lugha tofauti ambayo pia wajumbe wa mkutano huo hupata nafasi ya kuzungumza katika mikutano hiyo. Mathalani, ikiwa mkutano umefanyika nchini Urusi na mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa ambayo hayazungumzi Kirusi kama vile Waingereza, Wajerumani, Wachina na Waswahili, italazimu wakalimani wa lugha zote hizo wawepo na watakalimani kwa wakati mmoja au kuachiana nafasi ya sekunde kadhaa. Pia, wakati ambapo wajumbe wa mkutano ni wachangiaji na wanazungumza lugha mbalimbali, huwepo mkalimani wa lugha hizo ambaye hukalimani lugha zao katika lugha moja inayoonekana ina matumizi mapana kisha wakalimani wengine hukalimani lugha hiyo ili kuweza kueleweka kwa wajumbe wengine ambao hawaifahamu lugha hiyo ambapo ujumbe huo huwafikia kwa njia ya visikizi. Mbinu hii huhusisha matumizi ya simu iwapo wajumbe watakuwa mbali.
Ukalimani Pokezi
Hii ni mbinu inayotumika wakati ambapo mkalimani mmoja anapokezana na mzungu mwingine ambaye naye anaweza kuwa anakalimani lugha kwa mtu ambaye haelewi lugha ya mzungumzaji wa kwanza. Aghalabu, ukalimani huu hufanyika kwa mkalimani kuhawilisha ujumbe kutoka kwa mzungumzaji wa kwanza kwenda kwa msikilizaji kisha msikilizaji naye huzungumza na ambapo mkalimani wa kwanza hupokewa na mkalimani mwingine ili kuwaunganisha wazungumzaji hao. Aidha, NAJIT (2006) wanasema ukalimani huu hufaa zaidi katika majadiliano kati ya watu wawili wenye usuli tofauti katika lugha, hivyo mkalimani katika mbinu hii huwa ni kama daraja kuwaunganisha wazungumzaji hao kama asemavyo Bharati (2018) kwamba ukalimani huu ni faafu sana katika vikao vya watu wasiozidi watatu na hivyo huunganishwa na mkalimani mmoja. Kadhalika, ukalimani huu unafaa sana pale ambapo watu hukutana mathalani mama anapowakutanisha watoto wake na bibi wao ambaye hajui lugha inayozungumzwa na watoto na watoto wasijue lugha ya bibi yao. Hivyo, mama huwa mkalimani akipokezana na pande zote mbili. Ni dhahiri kuwa mbinu hii kiutendaji inaingiliana na mbinu ya ukalimani fuatizi.
3.6 Ukalimani Tazamishi/ Sindikizi
Kwa mujibu wa Tirosh (2020), hii ni mbinu ambapo mkalimani humsindikiza mteja wake sehemu ambayo kwayo ukalimani hufanyika. Mkalimani hukalimani kila jambo ambalo mteja wake huliona na kutaka kulifahamu. Mbinu hii hutumika zaidi katika shughuli za kitalii, muktadha wa sokoni, matukio ya kitamaduni na sehemu zingine. Mbinu hii inamuhitaji mkalimani kuwa na uelewa mkubwa kuhusiana na vitu mbalimbali ndani na nje ya jamii yake. Hata hivyo, mbinu hii inatofautiana na mbinu nyingine kwa kiasi kikubwa kwani haihitaji maandalizi ya ukumbi ama jukwaa bali mkalimani na mteja wake huenda katika eneo husika na kutekeleza shughuli hiyo ya ukalimani.
Hitimisho
Katika insha hii zimejadiliwa mbinu mbalimbali za ukalimani kwa kutalii mawazo ya wataalamu mbalimbali. Mbinu hizo ni kama vile; ukalimani fululizi, ukalimani fuatizi, ukalimani changamani, ukalimani nong’onezi, ukalimani tazamishi na ukalimani pokezi. Mbali na kujadili mbinu mbalimbali za ukalimani, insha hii imebeba fasili ya ukalimani na ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi sahihi ya istilahi mbalimbali za ukalimani, mathalani ‘aina’ na ‘mbinu’
MAREJELEO
Bharati, B. (2018). 5 “Different Types of Interpretation Techniques”. Kutoka
https://blog.bhashabharatiarts.com/5-different-types-of-interpretation-techniques/ ,
ilisomwa tarehe 19, Disemba 2020
Gaiba (1998). The Orgin of Simulitaneous Interpretation, “The Nuremberg Trial”. University of
Ottawa, Canada.
Gile, D. (2009) Basic Concepts and Models for Interpreter and Translator Training: Revised
Edition, Amsterdam and Philadelphia: John Benjamins Publishing Company.
GSI (2015). Interpreting. Berlin. GEMINO Publishers
Kade, O. (1968). Translation and Signed Language: Highlighting the Visual-Gestural Modality.
Saint Katarina. Brazil
Mshindo, H. B. (2010). Kutafsiri na Tafsiri. Dar es Salaam. OUP
Merinyo, F. F. (2014). Tafsiri na Ukalimani. Antigon Florence Publishers. Rombo.
Mpemba, T. (2013). “Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho”, Kiswahili,
76:112-140.
Mwaituka, D. P. (2012). “Matatizo ya Kiutendaji katika Ukalimani wa Mikutano” Dar es
Salaam: Tasnifu ya shahada ya Umahiri, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(haijachapishwa)
NAJIT (2006). “Translation and Interpretation” kutoka,
https://thetranslationcompany.com/translation-directory/translation-associations/najit- national-association-of-judiciary-interpreters-and-translators/,
ilisomwa tarehe 20, Disemba 2020
Nolan, J. (2005:3). Interpretation Techniques and Exercises. Multilingual Matters Ltd. Toronto.
Pöchhacker, F. (2004). Introducing Interpreting Studies. New York: Routledge.
Tirosh, O. (2020). “What are the Different types of Interpretation” kutoka
www.tomedes.com/translator-hub/types-of-interpretation,
imesomwa tarehe 20, Disemba 2020.
Trans Culture- TC (2007). “Interpretation Techniques” kutoka,
www.transcultures.com/interpretation-techniques/,
ilisomwa tarehe 19, Disemba 2020.
TUKI (1981). Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Oxford University Press. Dar es Salaam
Wanjala, F. S. (2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri kwa Shule, Vyuo na Ndaki. Mwanza:
Serengeti Educational Publishers (T) Ltd.
Comments
Post a Comment