UHAKIKI WA RIWAYA


JINA LA KITABU: Watoto wa Maman’tilie

MWANDISHI: Emmanuel Mbogo

Karibu tena katika makala yetu yanayojikita katika kutoa maarifa ya Kiswahili kwa kidato cha tatu. Leo tutachambua riwaya ya Watoto wa Maman’tilie.

Utangulizi

Watoto wa Maman’tilie ni riwaya iliyotungwa na Emmanuel Mbogo. Riwaya hii inachambua kwa kina maisha ya akina maman’tilie. Hata hivyo maman’tilie ametumika kama ishara tu ili kuwakilisha watu wanaoishi kwa kipato cha chini. Kwa hiyo dhamira kuu katika riwaya hii ni UMASIKINI. Umasikini huu umesababisha watoto wakose elimu, mavazi, wapate maradhi pamoja na kukusa sehemu bora ya kulala. Kutokana na hayo, watoto hujiingiza katika biashara haramu pamoja na wizi mambo yanayowapelekea kifo na kukamatwa na polisi.

MAUDHUI

Katika riwaya hii, msanii ameweza kuonesha shuruba mbalimbali zinazowakumba watu wa kipato cha chini. Kuanzia chakula wanachokula, elimu wanayopata, mavazi yao, huduma za afya na muonekano wao.

Hata hivyo riwaya hii imeonesha njia mbalimbali wazitumiazo masikini ili kukuabiliana na hali zao. Njia hizo ni halali na wakati mwingine si halali. Lakini msanii ameonesha kuwa njia zisizohalali mwisho wake huwa mbaya.

Dhamira

Mwandishi ameonesha mambo mbalimbali yanayoikumba jamii ya watoto wa mamantilie.Mambo hayo yamejenga dhamira mbalimbali kama ifuatavyo.

 • Umasikini

Katika riwaya hii umasikini umeoneshwa kwa kiasi kikubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa riwaya. Watoto wa maman’tilie wanaishi maisha ya dhiki. Maisha yao yanategemea genge la maman’tilie na kilichopatikana kiliishia tumboni tu (uk 4).

Pia, Kurwa na Doto ni watoto masikini waliotegemea dampo la Tabata kama sehemu ya kujipatia ridhiki. Watoto hao ni yatima wasio na msaada. Kutokana na maisha kuwa magumu sana, wanajiingiza katika wizi. Jambo hili linafanya Doto kupoteza maisha walipokuwa kwenye jaribio la wizi.

Vilevile, umasikini unaonekana kwa wafanyakazi wa kiwanda cha urafiki ambao hula chakula kichafu kinachouzwa kwa bei rahisi. Peter aliwauzia wafanyakazi hao wali na nyama alizookota jalalani.

Si hivyo tu bali umasikini unaonekana kwa Musa na Dani. Hawa ni watoto ambao wanajiingiza katika shughuli hatarishi ili wakidhi mahitaji yao ya kila siku. Musa anauza dawa za kulevya wakati Dani ni mwizi wa stendi na dukani. Hata hivyo Dani anauwawa akiwa kwenye jaribio la wizi wakati Musa anakamatwa na polisi akiwa na dawa za kulevya chumbani kwake.

Mwisho msanii ameonesha madhara ya umasikini katika jamii. Madhara hayo ni; kukosa elimu, kukosa lishe bora, huduma za afya, malazi bora, kujiingiza katika ulevi wa kupindukia, kuuza dawa za kulevya, kujiingiza katika wizi na ongezeko la watoto wa mtaani. Mwisho wa yote haya ni vifo na kukamatwa na polisi huku hali za waliobaki zikiendelea kuwa matatani zaidi.

 • Ukosefu wa Elimu

Elimu ni msingi wa maisha katika jamiii yoyote ile. Msanii ameonesha kuwa watoto wa masikini hukosa elimu kwa sababu ya kutokuwa na sare za shule na kushindwa kulipia ada. Peter, Zita, Musa na watoto wengine wa masikini walifukuzwa shule kwa sababu ya kukosa vitu hivyo. Mwalimu Chikoya (mwalimu mkuu) anasema “ Wote ambao hamna sare hakuna shule! Nisizione sura zenu bila ada na sare. Waambieni wazazi wenu hivyo” (Uk.1).

 • Malezi

Suala la malezi limezungumzwa kwa kina katika riwaya hii. Tunaona kuwa malezi bora huwa na matokeo bora na malezi mabaya huwa na matokeo hasi. Mwandishi amewatumia wahusika Doto, Kurwa, Dani na Musa kuwakilisha watoto waliokosa malezi bora hivyo wakajiingiza katika matendo hatarishi. Matendo hayo ni uuzaji wa dawa za kulevya na wizi. Mambo haya yaliwafanya waishie pabaya.

Kwa upande mwingine, Maman’tilie alijaribu kuwalea watoto wake kwa misingi bora. Lakini alishindwa kumudu malezi hayo kwani hakupata ushirikiano na mume wake ambaye ni mlevi wa kupindukia. Suala linalowafanya watoto hao kula chakula cha jalalani na Peter kijiingiza katika uuzaji wa dawa za kulevya na mwisho anakamatwa na polisi.

 • Wizi

Msanii ameonesha suala hili kwa kuwatumia wahusika Dani, Doto na Kurwa. Dani ni mtoto mwenye tabia ya wizi. Kila aingiapo stendi hukwapua mali za wasafiri. Pia, huiba kwa mhindi bangili, mkufu wa dhahabu ama chohote kitachomfaa. Ndiye aliyewashawishi Doto na Kurwa waende kuiba lakini mwisho wake ukawa kifo.

 • Biashara za Dawa za Kulevya

Uuzaji wa dawa za kulevya hufanywa kwa kuwatumia watoto. Msanii anamtumia Musa kudhibitisha hilo. Musa anamshawishi Peter ajiunge na genge la uuzaji wa dawa hizo lakini mwisho wanakamatwa na polisi.

 • Ulevi

Lomolomo ni mhusika anayewakilisha walevi wa kupindukia. Msanii anaonesha kuwa ulevi umesababisha Lomolomo kutokuwa muwajibikaji katika kuitunza familia yake. Hashiriki jambo lolote la kimaendeleo badala yake hunywa pombe tangia asubuhi hadi usiku. 

Hata hivyo msanii anaonesha kuwa ulevi ni mbaya kwani Lomolomo anapoteza maisha baada ya kunywa pombe iliyoisha muda wake wa matumizi.

 • Rushwa

Msanii ameonesha suala la rushwa ni tatizo katika jamii yetu. Maman’tilie na wenzie wanasumbuliwa sana na askari wa jiji wanaotaka rushwa ili wawaruhusu kuuza chakula kwenye eneo la kiwanda cha Urafiki. Jambo hili linafanya wafanya biashara hao kubaki katika hali duni.

 • Mapenzi

Msanii ameonesha kuwa katika jamii kuna mapenzi ya dhati na mapenzi yasiyo ya dhati.

Mapendi ya Dhati

Mamantilie ana mapenzi ya dhati kwani anaipenda familia yake na kuijali. Anahangaika kutafuta kipato ili watoto wake wapate chakula na waweze kurudi shuleni.

Vivyo hivyo, Zenabu ana mapenzi ya dhati kwa jirani zake. Hii inathibithishwa pale anapoitunza familia ya Maman’tilie wakati wote ambao Maman’tilie alipokuwa safarini. Aliweza kumpa Peter chakula na kumtunzia mchele wake. Pamoja na hayo ndiye aliyempeleka Zita hospitali baada ya kuugua.

Mapenzi ya dhati pia yanaonekana kwa Kurwa ambaye anamsaidia Peter ili asipigwe na Doto. Pia, alimgawia mchele alioukusanya jaani.

Peter ana mapenzi ya dhati kwani alimsaidia Kurwa pahala pa kuishi na kuwashawishi wazazi wake wampokee kama mmoja wa familia yao.

Mapenzi yasiyo ya dhati

katika riwaya hii msanii ameonesha wahusika wasio na mapenzi ya dhati kama ifuatavyo;

Mwalimu Chikoya hana mapenzi ya dhati kwa jamii yake. Aliwafukuza wanafunzi ambao hawakuwa na ada wala sare za shule ilhali akijua kuwa wanafunzi hao walikuwa masikini wa kutupwa.

Doto hana mapenzi ya kweli kwa Peter kwani badala ya kumkaribisha kwenye utafutaji wa riziki yeye alimpiga na kumfukuza.

Serikali haina mapenzi ya dhati kwa jamii hasa kwa watu masikini. Hii inadhibitika wazi kwa sababu ilishindwa kuwasaidia masikini hasa katika suala la chakula, elimu, makazi na afya. Wanachi masikini hawana chakula bora kwani wanakula vyakula hatarishi vilivyoisha muda na kutupwa, wanafukuzwa shule kwa kukosa ada na wanaelekea mauti kwa kukosa huduma bora za afya.

 • Nafasi ya Mwanamke katika Jamii

Msanii amemchora mwanamke katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo;

 • Mwanamke amechorwa kama mlezi wa familia. Amemtumia mama Kurwa, Jane pamoja na Maman’tilie kuthibitisha hili.
 • Mwanamke ni mtafutaji wa ridhiki kwa ajili ya familia yake. Maman’tilie ni muuza chakula na pesa anayoipata ni kwa ajili ya familia yake.
 • Mwanamke anahuruma na upendo. Maman’tilie anamhurumia mume wake, pia anamhurumia Kurwa na kumkaribisha awe mwanafamilia. Pia, Zenabu anamhurumia Peter na kumpa chakula. Vivyo hivyo Kurwa anahurumia Peter pale alipopigwa na Doto.
 • Mwanamke ni mvumilivu. Mwanamke anavumilia shida zote alizonazo mumewe.
 • Mwanamke ni jasiri na mstahimilivu. Hapa tunamuona Kurwa jinsi alivyojasiri na alistahimili shida zote alizopata. Aliweza kuyakabiri maisha yake ambayo yalikuwa kama vita. Mwandishi anasema;  

    “Kurwa hakupepesa macho, msichana kweli! lakini shupavu hashindwi na chochote awe msichana awe mvulana, hawezi kuchezea Kurwa” (uk 24).

Ujumbe

Kutokana na dhamira mbalimbali zilizooneshwa, tunapata jumbe zifuatazo.

 1. Tupige vita umasikini kwani ni chanzo cha matatizo mengi katika jamii. Matatizo hayo ni kama vile; ukosefu wa elimu, kukosa huduma bora za afya, kukosa malazi bora na kukosa chakula bora. Pia, umasikini ni chanzo cha uovu kama kama wizi, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
 2. Ulevi ni chanzo cha umasikini. Mzee Lomolomo ni mlevi kupindukia kiasi ambacho hawezi hata kufanya kazi ya kumuingizia kipato. Hii ilimfanya kuwa tegemezi na kuiingizia familia kwenye umasikini.
 3. Mapenzi ya dhati ni nguzo ya familia. Familia ikiwa na mapenzi ya dhati basi familia hiyo inakuwa bora kwani kila mmoja atawajibika. Hii inadhibitishwa na Maman’tilie kwa watoto wake.
 4. Rushwa ni adui wa maendeleo. Wauzaji wa chakula akina maman’tilie wanapata shida sana kwani huombwa rushwa ilhali kipato chao cha chini. Jambo hili linawafanya wasipige hatua ya kimaendeleo.
 5. Uovu sio suluhisho la kutatua matatizo yanayotukabili. Jambo hili linathibitika pale ambapo wahusika Dani, Doto na Musa walipoamua kujiingiza katika wizi na uuzaji wa dawa za kulevya ili kutatua tatizo la umasikini linalowakumba lakini mwisho wao ukawa tatizo zaidi.

Migogoro

Mikinzano iliyojitokeza katika riwaya hii ni kama ifuatayo;

 • Mgogoro kati ya Peter na Doto

Mgogoro huu ulisababishwa na Doto aliyetaka kumfukuza Peter jalalani. Mwisho wakapigana na Peter aliumizwa. Kurwa alisuluhisha mgogoro huu kwa kumtetea Peter na kumkataza Doto aache ugomvi.

 • Mgogoro kati ya Zita na Kurwa

Mgogoro huu ulisababishwa na Zita baada ya kumshambulia Kurwa na kusababisha mapigano. Zita hakumuamini Kurwa na hakuwa tayari kumpokea kama mwanafamilia. Mgogoro huu ulisuluhishwa na Peter aliyemuonya Kurwa kwa kumnasa kibao.

 • Mgogoro kati ya Maman’tilie na Mzee Lomolomo

Mgogoro huu ulisababishwa na tabia ya ulevi ya Lomolomo ambayo ilikuwa ikimkera sana Mamant’tilie. Mwisho ulevi ulisababisha Mzee Lomolomo kupoteza maisha.

 • Mgogoro kati ya Peter, Kurwa, Musa na askari

Mgogoro huu ulitokea baada ya polisi kuvamia chumba cha Musa na kuwakuta Peter, Musa na Kurwa kisha kuwatuhumu kuwa ni wauza dawa za kulevya. Mwisho watoto hawa wanakamatwa na kupelekwa polisi.

Migogoro ya nafsi

Migogoro hii inatokea kama ifuatavyo;

 • Kurwa anaonekana kuwa na mgogoro wa nafsi pale ambapo anawaza juu ya maisha yake ya shida. Hana wazazi wa kumtunza, hana furaha, hana nguo nzuri za kuvaa n.k. Mgogoro huu unatokea pale ambapo Kurwa anawaona watoto wawili wenye furaha wakipita na mama yao huku wakimueleza mahitaji yao.
 • Peter anapata mgogoro wa nafsi pale anapokuwa njia panda kimaamuzi. Hii ni baada ya kushawishiwa na Musa juu ya kujiunga na uuzaji wa dawa za kulevya.

Falsafa ya Mwandishi

Mwandishi anaelekea kuamini kuwa umasikini ni ugonjwa usiotibika. Anaonesha jitihada mbalimbali zilizofanya na Peter, Musa, Doto, Dani, Kurwa pamoja na Maman’tilie ili kujikwamua kimaisha lakini mwisho wao umekuwa maya zaidi.

Mtazamo wa Mwandishi

Mwandishi anamtazamo wa kiyakinifu. Anaonesha matatizo na sababu mbalimbali zinazopelekea umasikini. Pia, ameonesha jitihada mbalimbali za kukabiliana na umasikini ambazo ni kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa.

FANI

Msanii ametumia mbinu mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii. Mbinu hizo ni kama zifuatazo;

Muundo

Mwandishi ametumia muundo changamani lakini kwa kiasi kikubwa mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja (Msago). Anaeleza kuanzia watoto wa maman’tilie walivyofukuzwa shule na hatma yao baada ya shule.

Pia ametumia muundo rejea alipoonesha maisha ya Doto na Kurwa wakiwa wanajitegemea kisha baadaye anaeleza namna walivyozaliwa na kwa nini hawana wazazi.

Riwaya hii ina sura tano zenye sehemu ndogondogo zinazolenga kuunganisha tukio moja na jingine.

Mtindo

 • Mwandishi ametumia nafsi ya tatu kwa kiasi kikubwa.
 • Nafsi ya kwanza na ya pili imetumika palipo na majibizano ya wahusika.
 • Pia ametumia nyimbo mbalimbali kwa mfano,

“Mume wako sikumuita

Kanisimamisha mwenyewe

Kaniona dizaini…… (Uk 16)”

Mandhari

Mwandishi ametumia mandhari halisi yaliyohusisha jiji la Dar es Salaam na viunga vyake. Maeneo kama Manzese, Tabata, Kisutu, Kiwanda cha Urafiki n.k. yametumika.

Mandhari haya yametumika kuwakilisha matatizo yanayoikumba nchi ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.

Wahusika

Mwandishi ametumia wahusika mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwa jamii. Wahusika hao ni kama wafuatao.

Peter

Mtoto wa maman’tilie na Mzee Lomolomo

Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na sare.

Anapenda kusoma lakini hana ada na sare za shule.

Analipa fadhila kwa Kurwa.

Anakamatwa na polisi baada ya kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.

Aligeuza jaa kuwa mahali pa kutafuta riziki.

Anauza genge katika kipindi ambacho mama yake hayupo.

Zita

Mtoto wa Maman’tilie na Mzee Lomolomo.

Anafukuzwa shule kwa kukosa ada na sare.

Anang’atwa na mbwa mwenye kichaa.

Anamsaidia mama yake kuuza genge la chakula.

Anapandwa na kichaa cha mbwa.

Mwisho anafariki kwa kukosa matibabu ya mapema.

Maman’tilie

Mke wa Mzee Lomolomo

Ana maisha ya taabu, hawezi kumudu kulipa ada na kununua sare za shule kwa ajili ya wanae.

Anauza genge la chakula ili aihudumie familia yake.

Ni mvumilivu, kwani anavumilia matendo ya mumewe.

Ana mapenzi ya kweli kwa familia yake.

Mzee Lomolomo

Mume wa Maman’tilie na baba wa Zita na Peter

Ni mvivu kwani hajishughulishi na kazi yoyotee.

Anapenda kunywa pombe (ni mlevi).

Alifukuzwa kazi bandarini.

Ni masikini wa kutupwa

Anakufa baada ya kunywa pombe iliyoisha muda wake.

Doto na Kurwa

Watoto yatima wanaoishi maisha ya taabu.

Wanategemea dampo kwa ajili ya chakula.

Wanajiingiza katika wizi wakishirikiana na Dan.

Doto anakufa baada ya kuuwawa katika jaribio la wizi.

Kurwa anaenda kuishi kwa maman’tilie.

Kurwa anakamatwa na polisi alipokuwa na Musa pamoja na Peter kwa kosa la kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.

Musa

Rafiki yake Peter

Anafukuzwa shule kwa kukosa sare na ada.

Anamshawishi Peter kujiingiza katika uuzaji wa dawa za kulevya.

Anakamatwa na polisi kwa tuhuma za uuzaji wa dawa za kulevya.

Zenabu

Jirani na rafiki wa maman’tilie.

Anafanya kazi ya uuzaji wa pombe.

Ana roho nzuri, anawasaidia watoto wa Maman’tilie.

Anampeleka Zita hospitali alipopatwa na kichaa.

Matumizi ya Lugha

Riwaya hii imetumia lugha ya kawaida inayoeleweka kirahisi. Vipengele vya lugha vilivyotumika ni kama ifuatavyo;

Matumizi ya Lugha ya Kiingereza

Katika riwaya hii msanii ametumia maneno ya lugha ya Kiingereza ili kuonesha uhalisia wa kijamii. Maneno yaliyotumika ni kama ifuatavyo;

 • Faster faster mama”
 • “Misheni”
 • “Blaza”
 • “Nikukonekt”

Tamathali za Semi

Msanii ametumia tamathali za semi mbalimbali kama zifuatazo;

Tashibiha

Tamathali hii hulinganisha vitu viwili kwa kutumia maneno ya mlinganisho. Kwa mfano;

 • “Akamshika mumewe kwa mkono mmoja kama bua”
 • “Mate yenye harufu ya gongo yaliyomtoka kama cheche za moto.”
 • “Akaanguka chini kama mzigo”
 • “…. nywele za kipilipili za Musa, ngumu kama katani.”
 • “Kurwa aliruka nyuma kama chui”
 • “…..akaruka kama paa.”
 • “Mdomo wake ulikaa kama bakuli la pombe.”
 • “Zita alianguka chini kama gunia.”
 • “Moyo ukamzizima kama bonge la barafu.”

Tashihisi

Hii ni tamathali ambayo huvipa vitu au wanyama uwezo wa kutenda kama binadamu.

 • Vikombe vya sahani chafu zilizozagaa pale nje zikamtazama bila huruma.”
 • “….  miguuni raba zilicheka kwa huruma”
 • “Mlango ule wa kuungwa kwa gundi uliitika labeka.”

Matumizi ya Mbinu Nyingine za Kisanaa

Takriri

Hii ni mbinu ya kurudiarudia maneno. Kwa mfano;

– Nakuwacha! Nakuwacha!

– Baba! baba! amka baba!

– Twende! twende!

– Kukurukakara, kukurukakara, kukurukakara.

– Nivione! Nivione! Nivione vya kazi gani?

Tanakali Sauti

 • “Sasa alipiga mlango wa bati teke paa!”
 • “Mbwa alilia bwee!”
 • “… akatema phuuu!”
 • “…akasikia mgongo unalia ka-ka-kaa!”
 • “… Alikohoa, khoo! khoo!”
 • “Paa! Paa! Paa! bastora ililia.”

Ujenzi wa Taswira

Mwandishi amejenga taswira mbalimbali ambazo ni;

Taswira Zinazooneka

 • Mbwa mweusi mwenye mkia mweupe.
 • Vikombe, sahani, sufuria chafu zilizagaa nje.
 • Mabega yake yamechongoka karibu yakutane na masikio.

Taswira za Hisi

 • Tope la mbolea ya binadamu halikuwa mbali na Shimo…”
 • “Sakafu ya udongo uliong’ang’ania ndala za waogaji…”

Jina la Kitabu

Jina la kitabu “Watoto wa Maman’tilie” limesadifu mambo yaliyomo katika riwaya hii kama ifuatavyo;

Dhamira zote zimejikita katika kuonesha maisha halisi ya watoto wa maman’tilie pamoja na mambo yaliyowakabili. Mambo hayo ni kama vile; umasikini, ukosefu wa elimu, uuzaji wa dawa za kulevya, ulevi, vifo na mengine mengi.

Pia, wahusika waliotumika ni watoto wa Maman’tilie ambao wameonesha maisha halisi ya watoto na familia zinazofanana na zao. Maisha yao ni ya tabu yaliyojaa ndoto zisizofanikiwa.

Vivyo hivyo, lugha iliyotumika inarejelea mazingira halisi waliyonayo watoto wa maman’tilie na wengine wenye sifa kama zao.

KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI

 • Kufaulu kwa Mwandishi

Mwandishi amefaulu kifani na kimaudhui kama ifuatavyo:

Kimaudhui

Mwandishi amefaulu sana kimaudhui kwa sababu ameweza kuonesha dhamira mbalimbali zinazoakisi maisha halisi ya wanajamii kwa ujumla. Kupitia hizo ameweka wazi ujumbe na imani yake kuhusu mwenendo wa jamii.

Kifani

 • Mwandishi amefaulu sana kutumia wahusika mbalimbali walioakisi watu halisi katika jamii.
 • Pia, ametumia mandhari halisi ili kumfanya hadhira kuuona uhalisia uliopo katika jamii.
 • Vivyo hivyo, msanii ametumia lugha kiufundi kama vile, tamathali za semi, misemo, mchanganyo lugha n.k ili kuleta ladha na kufikisha ujumbe kwa jamii husika.  

Kutofaulu kwa Mwandishi

 • Mwandishi hakuonesha suluhisho juu ya matatizo yanayowakumba wahusika. Pia, hakuonesha dhahiri mwafaka