Mchungaji azungumza, utata juu ya kifo cha Yussuf Deus aliyekutwa amejinyonga



Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Kijitonyama jijini Dare s Salaam, Eliona Kimaro amesimulia kifo cha utata cha muuza chipsi, Yusuf Deus aliyekutwa amejinyonga katika banda lake la biashara jijini humo juzi.

Video iliyotumwa kwenye mitandao ya jamii jana ilimwonyesha Mchungaji Kimaro akieleza tukio hilo kuwa kabla ya kifo chake, kijana huyo aliyekuwa mwimbaji wa kwaya kanisani hapo aliwahi kutekwa na watu wasiojulikana tangu Desemba 2 hadi 8 mwaka huu.

Mwananchi jana iliwasiliana na uongozi wa Jeshi la Polisi kupata taarifa ya suala hilo, ambapo Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Ramadhan Kingai alielekeza atafutwe Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Mambosasa, hata hivyo, alipopigwa alijibu asingeweza kuzungumza kwa kuwa alikuwa ndani ya eneo la Ikulu kwa shughuli za kikazi.

Mchungaji Kimaro anaeleza kwenye video hiyo kuwa walimtafuta Yussuf baada ya kutekwa na walipomkosa waliripoti Polisi.

“Alikuwa amechukua Sh1.7 milioni kwenda kulipa mayai na bidhaa nyingine. Walikuja watu wakamteka na kumtupia kwenye gari na kuondoka naye.

ADVERTISEMENT

Alisema walimpeleka porini ambako pia hakujui na walikuwa wakibishana ama wamuue na wengine wakipinga.

Hata hivyo, mmoja wa watekaji hao alipinga wazo la kumuua akisema aliyewatuma hajawalipa na kuamua kuchukua zile Sh1.7 milioni walizomkuta nazo kisha wakamrudisha na kumtupa maeneo ya Sayansi baada ya wiki.

Baada ya kuokotwa, kijana huyo alirejea nyumbani na walikutana na alimwelezea mchungaji yaliyomkuta na alimsaidia kuendelea na shughuli zake.

Alisema Desemba 20 alimkabidhi Sh1.5 milioni ili arejee kwenye biashara yake ya chipsi. Lakini baada ya siku kadhaa kijana huyo akakutwa akiwa amejinyonga kwenye banda lake.

“Nilipomuuliza mkewe alisema aliondoka nyumbani saa 4.00 usiku kwenda kununua Luku ya umeme, hakurudi tena,” anasimulia mchungaji huyo.

Hata hivyo, kabla ya tukio la kutekwa, mchungaji Kimaro anaeleza kuwa kijana huyo akiwa kwenye eneo lake la kazi eneo la Kijitonyama, aliwahi kufuatwa na watu wanne, wakamwomba awajulishe mganga anayempa dawa ya kufanikisha biashara yake ya chipsi.

“Kwa mujibu wa maelezo yake, akawaambia mimi sina mganga kila kitu naombewa kanisani, kama ni mganga basi ni mchungaji wangu Kimaro, kama mnataka niwapeleke kanisani. Wakasema “Sisi tuko serious (hatuna masihara), tuonyeshe mganga wako,” mchungaji Kimaro anamnukuu kijana huyo.

Alisema kesho yake wale watu walirudi wakiwa na madai hayo ambayo Yussuf hakuweza kuwatekelezea.

Kaka wa marehemu, Emmanuel Kija alisema hakuwahi kusikia mdogo wake ana ugomvi na mtu yeyote katika maisha yake na hata baada ya tukio la kutekwa alimuuliza mke wa marehemu kama amewahi kusikia chochote na jibu lilikuwa ni hapana.

Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, Yusuf Deus a alizaliwa Februari 14, 1994, ameacha mke na watoto wawili; wa kwanza ni wa kike ana miaka mitatu na wa pili ni wa kiume ana mwaka mmoja

Chanzo: Gazeti la mwananchi.


Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?