Mbinu zitakazowasaidia wahitimu wa vyuo vikuu ‘kutoboa’ soko la ajira
- Wanahimizwa kutatmnini soko linataka nini kwa wakati huu.
- Kutengeneza mtandao na kujitolea katika shughuli mbalimbali kunaweza kuwatoa kimaisha.
- Serikali, wadau wakumbushwa kuimarisha programu za maendeleo ya nguvukazi kwa vijana.
Dar es Salaam. Ni ndoto ya kila muhitimu wa elimu ya juu, kuajiriwa au kujiajiri ili kutumia taaluma na kipaji chake kuwa sehemu ya kuchangia maendeleo ya jamii na kupata kipato cha kuboresha maisha yake.
Lakini ndoto hizo huyeyuka baada ya wahitimu kuingia mtaani na kujikuta waliyotarajia kuyapata hayapo, jambo linalowaweka katika utata wa kuzikabili changamoto za ajira na kujenga mustakabali mzuri wa maisha ya baadaye.
Hata hivyo, vijana waliopo vyuoni na wale ambao wamehitimu miaka ya hivi karibuni, bado wana nafasi kubwa ya kufanikiwa katika ajira za kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.
Yapo mambo mengi yanayoweza kuwasaidia vijana hasa waliopo vyuoni kufanikiwa mara baada ya kutoka vyuoni. Usisubiri umalize masomo, ndiyo uanze kutafuta hatma ya maisha yako.
Anza ukiwa shuleni, ukitoka iwe rahisi kufanikiwa katika soko la ajira hasa kwa wale wenye mawazo ya kuajiriwa ili kutumia taaluma zao.
Uchambuzi uliofanywa na mtandao Huu, kuhusu soko la ajira la sasa ambalo kwa kiasi kikubwa linaathiriwa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, linawataka vijana kuwa majasiri, wasaka fursa na walio na ujuzi wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.
Tenga muda wa kujifunza na kupata taarifa ya kinachoendelea katika sekta ya ajira. Tambua soko linahitaji nini kwa wakati ukilinganisha na ulichonacho.

Je kuna teknolojia imeingia sokoni ambayo ni muhimu kujifunza ambayo unaamini inaweza kuongeza thamani katika taaluma yako? Kadiri unavyojifunza zaidi, unapata fursa ya kuhuisha akili yako na kuwa mbunifu katika soko la ajira.
Jenga mtandao
Hata kabla hujamaliza masomo yako, anza kujenga mtandao wa marafiki na watu wengi unaofikiri muhimu kukusaidia katika taaluma yako. Dunia imebadilika, watu wanafanya kazi wakati mwingine kwa kujuana na kuaminiana.
Mtandao (network) itakusadia kupata mawazo mapya na kukutanisha na watu wenye uwezo na ujuzi tofauti ambao unaweza kuwa fursa kwako kupata ajira baada ya masomo.
Mtaalamu wa masuala ya ajira wa kampuni inayowaunganisha watu na fursa za ajira ya Monster Worldwide, Inc, Linda Wiener anasema mtandao ni sehemu muhimu ya utafutaji wa ajira lakini inahitaji mipango inayoeleweka ya kutengeneza mawasiliano na mahusiano mazuri na watu wanaohusika na shughuli mbalimbali ambazo zinaendana na taaluma yako.
“Kwa kila mawasiliano, tambua hatua zinazofuata na mfumo wa ufuatiliaji wa kuaminika. Mkusanyiko wa kadi za mawasiliano utafanya kazi; kwa kutumia daftari au programu ya kompyuta. Jambo la muhimu ni kuhakikisha mawasiliano yako yanadumu,” anasema Wiener.
Mawasiliano na mahusiano unaweza kuyajenga na marafiki mnao au mlisoma nao, klabu za wanafunzi, waajiriwa wa taasisi mbalimbali, majirani na watu unaokutana nao kwa mara ya kwanza katika mikusanyiko mbalimbali.
Pia shiriki majukwaa mbalimbali yanayohusisha shughuli za kijamii au taaluma. Yote hii itatanua wigo wako wa kupata fursa za ajira.
Jitolee katika shughuli mbalimbali
Kujitolea katika shughuli mbalimbali za kijamii (volunteering) wakati ukiwa masomoni ni njia nyingine ya kujiandaa kuingia katika soko la ajira.
Zipo programu mbalimbali zinazoendeshwa na taasisi na mashirika mbalimbali kama Umoja wa Mataifa (United Nations Volunteers) ambazo zinatoa fursa kwa vijana waliopo shuleni kufanya kazi za kijamii bila kulipwa.
Katika kazi hizo utajifunza vitu vingi ikiwemo jinsi ya kuishi na watu mahali pa kazi, uongozi, kutatua changamoto na uvumilivu. Pia, inaweza kuwa fursa ya kuajiriwa katika taasisi hizo baada ya kumaliza masomo hasa katika mashirika ya kimataifa.
Kwa vijana ambao ndiyo wanamaliza masomo wanaweza kuingia katika programu za ujuzi kazini (Interniship programs) ambazo unaomba katika kampuni ili ufanye kazi kwa muda mfupi kwa ujira mdogo.
Kupitia programu hizi utapata ujuzi na uzoefu wa kufanya kazi, hata ukipata kazi mpya ni rahisi kuajiriwa kwa sababu una uwezo wa kutekeleza majukumu kikamilifu.
Jijenge kitaaluma
Fahamu wazi kuwa lengo la elimu ya chuo ni kukuandaa kwa ajili ya kuingia kazini au kijiajiri. Kama ndiyo hivyo, anza kufanya mambo yako kwa kuzingatia taaluma unayosomea.
Mtaalam wa wasifu na taaluma kutoka kampuni ya CareerAddict ya Ireland, Joanna Zambas anasema jitahidi kujiheshimu, jenga umakini na mtazamo chanya kwa kila jambo unalofanya huku ikizingatia muda na miadi unayopanga na watu.
Kijizoesha tabia hizi wakati ukiwa chuoni, kutakusaidia hata unapoingia kwenye soko la ajira kufanya vizuri zaidi. Jifunze kwa watu wanaofanya kazi katika taaluma unayosomea namna wanavyoendesha mambo yao.

Programu za maendeleo ya nguvukazi
Hata wakati vijana waliopo chuoni wakijiandaa kuingia katika soko ajira, Serikali na wadau wa elimu nao wana sehemu ya kuwaandaa kupata ujuzi na maarifa zaidi ya yale wanayopata darasani ili kuwawezesha kuhimili changamoto za ajira.
Programu za ujuzi na kuendeleza nguvukazi zinazoendeshwa na taasisi mbalimbali zikiwemo za Launch Pad na Digital Opportunity Trust (DOT) zinaweza kuwasaidia vijana kutambua vipaji na uwezo walionao wa kuibua suluhisho la teknolojia la changamoto zilizopo kwenye jamii.
“Wengi wetu tunapuuza uwezo wetu wa ubunifu; tunatoa sifa kwa wasanii bora lakini tunapuuza mazingira ambayo tumetumia akili zetu na rasilimali zetu kwa ubunifu kushughulikia hali za maisha,” anasema Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Launch Pad, Henry Kulaya
Programu kama hizi zinaruhusu vijana kuunganisha ujuzi wa kiufundi na stadi za maisha zinazowasaidia kuwa na uelewa masuala mbalimbali ya fedha na uongozi.
Chama cha Waajiri Afrika Mashariki (EAEO) kinaeleza kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 60,000 wanahitimu vyuo vikuu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) huku nusu ya wahitimu hao wakiwa hawana vigezo vya kuajiriwa.
Wadau wa elimu wamesema kuna haja ya kupitia upya mitaala ya elimu tangu ngazi ya shule za msingi ili iendane na mabadiliko yanayotokea katika soko la ajira kwa sasa ambalo linahitaji vijana wenye ujuzi na maarifa ya kutosha kutimiza majukumu wanayokabidhiwa katika jamii.
Mhadhili kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO), Richard Ngaiza amesema mitaala hiyo ni muhimu ikalenga kuwajengea uwezo wa kivitendo wanafunzi na kuwafunza kuzingatia maadili ya kazi ili kuongeza ushindani katika soko la ajira.
Kijana, mustakabali wa maisha yako uko mikononi mwako. Tafuta kila fursa iliyo mbele yako. Soko la ajira ni ushindani na wenye nguvu ndiyo wanaoshinda na kufanikiwa.
Comments
Post a Comment