Chuo-BBC
Angalia habari yoyote kwenye gazeti – kuna kichwa cha habari, mwanzo na habari kamili. Utangulizi wako unatakiwa utimize mambo hayo mawili ya kwanza.
Na Neil Churchman
Katika chochote ukifanyacho, kamwe usiwachanganye au kuwachosha wasikilizaji. Kuna habari ambazo  zinavutia; zingine zinaweza kukanganya na zisizosisimua. Kazi yako ni kufanya watu waketi, wasikilize na watambue. Utangulizi ndio dirisha la duka letu ambalo tunatumia kumvutia msikilizaji kutamani bidhaa tuliyo nayo, ambayo ni habari.
Utakachoweka katika utangulizi
Angalia habari yoyote kwenye gazeti – kuna kichwa cha habari, mwanzo na habari kamili. Utangulizi wako unatakiwa utimize mambo hayo mawili ya kwanza. Kwa mfano:
Kichwa cha habari: “Kudorora kwa uchumi kwaongeza wizi na ujambazi”
Mwanzo wa taarifa: “Kuongezeka kwa visa vya uvunjaji wa nyumba, wizi na wizi wa kutumia visu kwazua wasiwasi kuwa kudorora kwa uchumi kumeanza kuongeza uhalifu”
Hayo ndio maelezo unayotakiwa kuwa nayo kwenye utangulizi wako.
Utangulizi mzuri
Utangulizi mzuri huwavutia wasikilizaji mara moja. Ikiwezekana anza na tukio lenyewe. Kuna mfano mzuri hapa kutoka kwa muhtasari wa Radio 4:
“Wanadiplomasia kutoka nchi za magharibi wameondoka ghafla kutoka kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi mjini Geneva, wakati wa hutuba ya rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad.  Rais huyo aliwaudhi wanadiplomasia hao kwa kuuita utawala wa Israel katili na wenye ubaguzi wa rangi. Kutoka Geneva, Imogen Foulkes.”
Hapa, tunaanza moja kwa moja na tukio. Mstari wa kwanza unasema ni nini, nani na wapi. Mstari wa pili unaeleza kwa nini. Ni mfano mzuri wa kutumia maneno machache. Utangulizi huu unakufanya utake kusikiliza zaidi.
Ongeza mtu
Nukuu nzuri kutoka kwa mhusika mkuu inaweza kufanya utangulizi wa habari uvutie sana. Kwa mfano tungeandika utangulizi kama huu:
“Mbunge wa zamani wa chama cha Labour, Alice Mahon amejiuzulu kutoka kwa chama hicho kutokana na jinsi Gordon Brown anavyoendesha uchumi na kashfa ya barua pepe katika makao ya waziri mkuu, Downing Street. Alisema sifa ya chama imeharibiwa”.
Lakini sisi tuliiandika hivi:
“Mbunge wa zamani kutoka chama cha Labour, Alice Mahon amejiuzulu kutoka kwa chama hicho baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 50 akisema amechoshwa na jinsi chama hicho kinavyoendeshwa . Katika barua kwa chama cha jimbo lake huko Halifax, mbunge huyo alisema amesikitishwa sana na jinsi Gordon Brown anavyoendesha uchumi na kashfa ya taarifa zilizojitokeza kwa barua pepe.”
Mfano wa pili ni mzuri zaidi. Kuna watu wengi zaidi wanaotajwa na lugha iliyo wazi zaidi, kama “kuchoshwa” na “kuudhiwa”. Itamvutia msikilizaji zaidi.
Kushirikiana
Utangulizi mzuri mara nyingi unatokana na wewe kushirikiana na mwanahabari. Unapaswa kuwa na lengo la kutoa taarifa inayotiririka vizuri na si kusema mambo ambayo taarifa ya mwandishi itarudia. Kwa hiyo ni vizuri kuongea – mapema na mara kwa mara iwezekanavo.
Elewa taarifa yako
Mambo muhimu yanaweza kubadilika katika dakika ya mwisho, au matatizo ya kiufundi yanaweza kumzuia mwandishi asitoe habari fulani muhimu katika taarifa hiyo. Kwa hiyo unatakiwa uijue taarifa hiyo vizuri. Soma kwenye tovuti, angalia jinsi idhaa zingine zinavyoishughulikia taarifa hiyo na uwe tayari kuiandika upya katika dakika za mwisho.
Ifanye rahisi
Msikilizaji ana fursa moja tu ya kusikia unachosema kwa hiyo tumia lugha rahisi, ya kuvutia na inayoeleweka. Epuka sentensi yenye sehemu nyingi. Ikiwa sentensi ni ndefu, ikate na ujisomee utangulizi huo, huenda ukapata kuna sehemu umerudia rudia au kuna maneno ya kukanganya ulimi. Ni ishara nzuri kuona watangazaji wakinong’ona si kwamba wamerukwa akili.
Epuka balaa
Kuna mambo mengi yanayoweza kuharibu utangulizi wako-na mengi ni ya kujiletea.  Hakikisha kila wakati unasikiliza ripoti unayoandikia utangulizi, isije ikawa na maneno yale yale utakayotumia au hata sentensi zingine ambazo umetumia, inasikika vibaya sana.
Ripoti inayoanza na sauti tofauti
Kuwa mwangalifu wakati unapoandika utangulizi wa ripoti inayoanza na sauti tofauti. Wakati mtangazaji anasema, ‘ifuatayo ni ripoti ya Justin Webb’ unatazamia kusikia sauti ya binadamu kwanza, si nyangumi, milio ya risasi au vinanda. Utangulizi mzuri basi unapaswa kumtayarisha msikilizaji ajue kwamba atasikia sauti tofauti kabla ya ile ya Justin Webb.
Usiweke mambo mengi
Usiweke mambo mengi katika utangulizi. Japo wakati mwingine zinahitajika, takwimu nyingi zinaweza kuharibu utangulizi, na usitazamie kuwa kila mtu ataelewa ufupisho wa majina unasimamia nini. Kwa mfano si kila mtu anafahamu kuwa UNODC inasimamia United Nations Office for Drugs and Crime. ( Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa ya kulevya na uhalifu).
Andika kwa kipindi mahsusi
Unapaswa kuandika utangulizi unaozingatia idhaa au kipindi. Kila idhaa ina msamiati wake na njia ya kuandika kwa sababu ya wasikilizaji wake. Katika idhaa ya muziki kama Radio 2 hatuwezi kusema ‘mwimbaji Michael Jackson’ kwa sababu tunatazamia kuwa wasikilizaji wanafahamu kuwa Michael Jackson alikuwa mwimbaji. Vivyo katika vipindi vya michezo tunatazamia wasikilizaji kujua Didier Drogba ni nani.
Jifunze kutoka kwa wengine
BBC ina watangazaji wengi wenye uzoefu mkubwa wa kuandika utangulizi. Jifunze kutoka kwao. Unaposikia utangulizi mzuri, uchunguze vizuri uone jinsi ulivyoandikwa na jinsi unavyotumiwa. Iwapo una tashwishi, jiulize jinsi ungeieleza habari hiyo kwa sentensi moja tu, mara nyingi sentensi hiyo itakuwa msingi wa utangulizi bora.