• Baadhi ya wadau wa muziki wamesema ni ukosefu wa ubunifu na uwekezaji mdogo katika kazi wanazofanya. 
  • Pia ushirikiano mdogo na wanamuziki wa nje na kushindwa kutumia mizuri majukwaa ya kimataifa ya mauzo kama Youtube. 
  • Wameshauriwa kujiongeza ili kulifikia soko la kimataifa kama wenzao wa kiume. 

Dar es Salaam. Wakati wanamuziki wa kike wa nchi za magharibi mwa Afrika na nje ya bara hilo wakipasua anga la kimataifa kwa kazi za muziki, wenzao wa Tanzania wana kibarua kigumu kuelekea katika anga za kimataifa
Hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ubunifu wa kutengeneza muziki wenye mvuto unaoweza kugusa idadi kubwa ya watu duniani. 
Mathalani, mwanamuziki wa kike wa Nigeria, Yemi Aladei ameweza kujipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na muziki wake kugusa maisha ya watu wengi. 
Chaneli yake ya Youtube ina wafuasi wasiopungua milioni 1.1, Yemi maarufu kama Mama Afrika mwenye miaka 30 ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa zaidi barani Afrika. 
Pia mwanadada huyo ana wafuasi zaidi ya milioni 8.3 katika mtandao wa Instagram, jambo linalomrahisishia muziki wake kuuzika kirahisi katika majukwaa ya kimataifa ikiwemo Youtube. 
Wakati wanamuziki wa kike wa nchi nyingine za Afrika na nje ya bara hilo kama Ariana Grande, Taylor Swift na Rihanna  wanaotoka Marekani wakitikisa dunia, wenzao wa Tanzania bado wanajikongoja hasa katika kutumia majukwaa ya kuuza muziki wao kimataifa. 
Kwa takwimu zilizopo kwenye mtandao wa Youtube, msanii wa kike anayeongoza kwa wafuasi wengi kwenye mtandao huo ni Faustina Charles (Nandy) ambaye ana wafuasi takriban 278,000 huku Vanessa Mdee akifuatia kwa kuwa na wafuasi takriban 163,000 hadi kufikia saa 6:30 mchana wa Septemba 2, 2019.
Wengine wenye wafuasi wengi ni pamoja na Maua Sama (149,480), Ruby (69, 078) na Rosa Ree (55,351).
Muziki ukitumiwa vizuri unaweza kuwa sehemu muhimu ya kuingiza kipato kwa wanamuziki wa kike Tanzania. Picha|Mtandao.
Hata hivyo ukiangalia, hakuna mwanamuziki wa kike wa Tanzania aliyefanikiwa kufikisha japo wafuasi 500,000, licha ukweli kuwa kwenye mtandao wa Instagram wanafanya vizuri lakini mtandao huo hautumiki sana kwa shughuli za kibiashara. 
Ni muhimu kukumbuka kuwa mafanikio ya mwanamuziki hayapimwi kwa kuwa na wafuasi wengi mtandaoni lakini ziko sababu mbalimbali ikiwemo ubora wa muziki anaofanya msanii husika. 
Kwa nini hawatoboi kimataifa?
Blandina Raymond, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCO), anasema wanamuziki wengi wa kike  wanashindana wao kwa wao lakini ushindani wao sio wa maendeleo.
“Wasanii wa kike wengi wana ushindan, hawana ushirikiano kama wanaume,” amesema Raymond ambaye ni mdau wa muziki wa Bongofleva
Kwa mujibu wa Raymond na wadau wengine wa muziki, wanamuziki wa kike hawajiamini na hawana uthubutu hivyo kushindwa kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwafanya kurudia vitu vile vile kama vinavyofanywa na wasanii wengine.

Tofauti na wanamuziki wa kike, wanamuziki wa kiume wa Tanzania wanafanya vizuri na hata kuwafanya washindane kimataifa na kushirikiana na wasanii wengine wa nje. 
Changamoto inayowakumba pia wanamuziki wa kike ni kukosa elimu na mafunzo ya kile wanachokifanya, jambo linalowaweka pembeni katika kuwekeza na kujitangaza kimataifa. 
“Wasanii wengi wa kike wanarudishwa nyuma na elimu, jinsi ya kujitangaza na kuridhika mapema,” amesema Martha Ngwanda ambaye ni mdau wa sanaa ya uchoraji picha. 
Naye, Leyla Siraj ambaye ni mwanamuziki anayeibukia amesema wasanii wengi wa kike wanaogopa kujaribu vitu vipya wakihofia jamii na mashabiki wanao wazunguka watawakatisha tamaa. 
Siraj amesema ipo haja ya wasanii wa kike kujiendeleza na kuwa wabunifu kwenye kazi ambazo wanazifanya ili kuongeza mvuto kufikia ngazi za kimataifa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi waliongea na mtandao huu, wamesema kwa sasa wanamuziki wa kike wameamka na wanafanya vizuri, jambo ambalo limeanza kuwafanya kusikika katika anga za kimataifa akiwemo Vanessa Mdee. 
Ili kuzifikia ngazi za kimataifa, wameshauriwa kuongeza wigo wa ushirikiano na wasanii wa nje huku wakiwekeza zaidi katika kutafuta maarifa mapya ya muziki ili kukuza masoko ya kazi zao.