Namna gani kazi ya meneja wa studio ilivyogeuka tangu kuja vielelezo vya redio na mtandao wa jamii. Hapa tunaangalia uweledi unaohitajiwa.

Jukumu la meneja wa studio (SM – Studio Manager) ni uendeshaji wa kifundi wa vipindi vya redio mubashara au vya kurikodi. Na kuhakikisha  vinasikika kwa daraja bora,  na ikiwa vinaendeshwa kwa sauti na kamera, basi daraja bora ya video piya.  Ingawaje kuendesha deski la sauti  ndio bado ni sehemu kubwa ya meneja wa studio, hata hivyo jukumu hilo limepanuka. Na sasa limekuwa pamoja na kusahilisha utoaji matangazo kwenye majukwaa mengi na kidijitali.  Wasikilizaji wanavutiwa  zaidi na redio yenye picha, na kwa hivyo imebidi vipindi vya redio viwafuate waliko.  Mkabala huu mpya wa redio umebadili  majukumu ya timu nzima ya watoaji vipindi. Na hapa tutaangalia meneja wa studio analazimika kuwa na sifa gani.  
Tumezungumza na mameneja wa BBC World Service ili watujuulishe orodha ya kisasa kabisa ya ujuzi na uweledi unaohitajika.
Matayarisho ndio muhimu
Uliza mapema inavyowezekana maagizo unayotarajiwa kutekeleza. Kila kipindi kina mahitaji yake ya kifundi, kwa hivyo fahamu vilivyo yote yale yatayotokea kwenye kurikodi na kitu gani utahitaji kukiweka tayari kabla ya “booking” kuanza. Ikiwa “booking” yenyewe ni redio ya picha, jukumu lako ni kujua jee kipindi hicho kitarushwa kwa mtiririko (streaming)  kwenye mtandao wa kijamii au kwa video, ili ije kutumiwa kwa matumizi mengine. Ni jukumu lako kuhakikisha kwamba vyombo vyote vinafanya kazi sawasawa kabla ya timu kufika. Kadhalika, hakikisha kwamba eneo lote ni salama, kwamba kila kitu cha hatari kimeondoshwa na wewe na wengine ni salama salmin.  Matangazo na yawe muhimu na magumu kama yatakavyokuwa, usalama siku zote ndio muhimu kabisa.
Hakikisha unajua wapi unakwenda, na wakati gani unatarajiwa kufika. Wakati gani yanaanza mazoezi na jee kipindi ni cha kurikodi au mubashara? Fika pale dakika 5 au 10 kabla ya wengine, ili kucheki (kukagua) vyombo vyako na ipitie orodha ya mtiririko wa kipindi. Na ikiwa kipindi chenyewe ni cha redio ya picha, hapo utahitaji wakati mwingi zaidi wa matayarisho. Inapendekezwa kutumia dakika 20 au 30 kujitayarisha sawa sawa – utahitaji zaidi ikiwa “redio ya picha”.
  • Kama ni mubashara, wakati gani unatakiwa kuanza mubashara na kumaliza mubashara?
  • Watu wangapi wanatarajiwa kuwa ndani ya studio?
  • Jee mtayarishi wa kipindi amekupa utaratibu wa matangazo (running order)?
  • Kuna mambo yoyote mengine ziada ambayo lazima tuyajue kabla ya kazi kuanza? Unahitaji kujadili lolote na mtayarishi wa kipindi?
Mitambo
Ni jukumu lako kuhakikisha vifaa vyote vya kifundi vinafanya kazi sawasawa. Lazima kufanya hayo kabla ya kila matangazo, hata ikiwa ulikuwako studioni punde tu kabla ya hapo. Hujui mabadiliko gani yamefanywa. Cheki sauti zilizorikodiwa na vibwagizo, kama vinasikika sawasawa kama ulivyotaraji. Ripoti mambo yote ya kifundi au ya usalama yanayohitaji kutengenezwa. 
Pitisha kwenye  dawati laini zozote za simu kutoka nje zinazotakiwa. Ikiwa matangazo yenyewe ni mubashara huenda ukataka “main” na “backup”. Ni busara kupakia hayo upesi inavyowezekana, kwa sababu namna mbalimbali ya kiungo cha simu kinaweza kisiwe cha kutegemewa.  Unapounganisha mchangiaji wa nje kwa mara ya mwanzo,  huenda ikawa jambo la busara kujaribu mapema kiungo kabla ya matangazo.
  • Unataraji wachangiaji kutoka nje (Os au Skype au laini ya simu ya ISDN) au utacheza klipu (yaani kitu kisharikodiwa)
  • Jee vilivyorikodiwa na kibwagizo (sting) vinasikika kama inavyotarajiwa?
  • Itakuwepo rikodi ya video au mtiririko kwenye mtandao wa kijamii?
Matangazao ya sauti na picha
Matangazo ya redio na video yanaweza kuvutia sana, hasa kwa wasikilizaji wa kimataifa ambao huenda wakapendelea kuangalia matangazo kwa kupitia Facebook au kwenye mtiririko wa YouTube.  Timu moja ya BBC World Service ilikutwa na mtihani  kwa vile matangazo ya redio shirika hayakusikika kwa sababu ya matatizo ya kisiasa au kiufundi, kwa hivyo njia pekee kwa wasikilizaji ikawa njia ya mtiririko katika mtandao wa kijamii.
Wahusika wa matangazo lazima watayarishe matangazo ya redio kwa picha muda mrefu kabla ya kurikodi, na wakuletee ili upate kujua vipi studio itatumika kutekeleza maagizo yaliopo.
Mtindo wa picha kwenye redio ya video sio kama ule wa TV. Kamera za redio ziko kitambo kwenye studio nyingi. Kadhalika njia ya kuziwasha kamera kwa njia ya otomitiki.
Kawaida mpango huwa hivi: Kamera moja ya mapana kunasa picha nzima ya ndani ya studio, kamera 3 kulenga mtangazaji na wageni wowote wataokuwepo.
Ikiwa kuna mpango wa kupiga filamu/video, mambo ya ufundi ni jukumu lako: hakikisha kwamba kamera zinafanya kazi sawasawa na zinaungana na programu ya komputa ya  kurikodi na kutiririsha (streaming) na kwamba taa zinawaka, ikiwa ziko.
Ni uzuri kukumbuka kwamba katika kipindi cha redio kwa video, redio daima inapewa kipa umbele. Kipindi chako kitakuwa kinaendeshwa kwa uamuzi wa mhariri wa redio, lakini vilevile utahitaji kufikiria  “ki-TV” kuhusu  studio itaonekana vipi katika picha.
  • Jee watangazaji wanajua kamera gani zinawalenga na ziko wapi?
  • Maiki zinaweza kuhamishwa-hamishwa ili mtangazaji aonekane sawasawa (bila ya kuharibu sauti?)
  • Taa zinaweza kun’gara zaidi au kufifia ili kutoa picha nzuri zaidi?
  • Jee nembo ya BBC inaonekana? Matangazo ya BBC lazima yawe na nembo.
Mtayarishaji wa matangazo lazima achangie katika maamuzi hayo, lakini ni vizui kwako kuyajua na kufikiria vipi hayo yataathiri na kufikiria ikiwa hayo yataathiri uendeshaji wa matangazo kiufundi.
Mawasiliano na timu ni kitu cha msingi katika kutekeleza kazi yako uzuri. Daima kutakuwa na jambo kuhusu kipindi, ambapo itakubidi kulicheki na mtayarishaji wa matangazo, na bora kuweka wazi kila kitu tangu mwanzo wa kipindi.
Mtayarishaji matangazo huwa anafikiria mengi wakati wa kipindi chenyewe, kwa hivyo ni muhimu sana kuchagua wakati muafaka kuzusha maswali au matatizo. Lengo lako liwe, dakika tano kabla ya matangazo, wewe na mtayarishi wa kipindi muwe  mmeshafahamiana juu ya kila kitu kitachohitajika kutoka kwako.
Utaweza  kuongea na mtangazaji kwa kupitia ‘headphone’. Kwa vile kila kitu ni mubashara, tahadhari usiwababaishe bila ya dharura.  Kuelezana kwa wazi na ufupi ndio vema kabisa; kwa mfano  sekunde ngapi kabla ya maiki kuwa ‘live’  tena.
  • Angalia orodha ya kipindi chako: jee ungependa kujua zaidi kuhusu sehemu ya kipindi?. Unafahamu wazi mtayarishaji wa kipindi anataraji nini kwako?
  • Wakati gani mtangazaji anataka kuzinduliwa awe tayari?
 Wepesi wa kujirekibisha
Kitu muhimu kabisa wakati matangazo yanaendelea ni kujua kitu gani kinafuata.
Wakati mwengine mpangilio unabadilika kabisa wakati kipindi kiko hewani. Kwa mfano, mhojiwa huenda asitokeze au kuna habari moto zimetokea. Wakati huo unahitaji mtayarishaji wa matangazo kukuarifu kinachofuata ili upate tayarisha dawati. 
Mwiko mkubwa katika redio ni kukaa kimya.  Sekunde chache bila ya sauti zinatosha kuwatia wasiwasi wasikilizaji na hata kuzima redio. Kwa hivyo lazima ujue utafanya nini ukiwa huweza kucheza chochote kile kutoka studioni. Pengine mtangazaji kabanwa na kicheko, au mtu kazidiwa na maradhi studioni. Kazi yako wewe ni kuhakikisha kitu muafaka kinaendelea kusikika hewani.  Ukikosa yote, basi cheza ukanda wa muziki ambao juu yake kuna ombi la msamaha. Jielimishe mipango ilioko kwa nyakati maalumu (mfano kulikimbia jengo kukiwa na dharura; habari maalumu; na tangazo la kifo). Huenda kukawa na vitu maalumu unatarajiwa kuvicheza katika hali mbalimbali.
  • Ikiwa itakubidi kuzima maiki katika studio, utacheza kitu gani? Jee kitu hicho kimo mitamboni?
Wakati
Kwa sehemu kubwa ni kazi ya mtayarishaji matangazo kuangalia jinsi ulivyo katika kipindi. Lakini  ukiona jambo fulani haliendi sawa, chukua hatua; mzindue mtayarishaji wa kipindi. 
Jizoeshe kujumlisha dakika na sekunde. Ujuzi huo utakuwa na thamani wakati unatia hesabu umebakiwa na wakati kiasi gani hadi sehemu ya kipindi inayofuata.
Kuwa makini
Mambo mengi yanaweza kukubabaisha ukiwa studio. Inaweza kuwa kipindi ni kirefu, au umechelewa kulala, au kipindi ni cha lugha ya kigeni, ambayo inakuwa shida kuifuatilia wakati wote. Mbinu chache za kufuata  kuhakikisha uko makini: hakikisha umepumzika vya kutosha, kunywa maji ya kutosha, tembea kila ukipata nafasi. Kitu muhimu ni kuwa makini, machoni na akilini, kwa hivyo ni muhimu kuweka kando simu na chochote cha kukubabaisha wakati umo studioni.   
Mara yako ya mwanzo (uwanagenzi)
Utakuwa na wasiwasi utapodhibiti mitambo mara ya kwanza. Penye shinikizo jaribu kuwa shuwari. Baada ya muda, umakini wa akili wa meneja wa studio kwako utakuwa umbile. Hapo ndipo kazi inakuwa kama sanaa zaidi kuliko  sayansi, na utazidi kuionea raha hasa. Itakuja kutokana na uzoefu, kwa hivyo usivunjike moyo