Dhana ya fasihi simulizi kwa mujibu wa Mlokozi (1996), ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.
Hivyo fasihi simulizi inafungamana na muktadha au mazingira fulani ya kijamii na kutawaliwa na mwingiliano wa mambo
kama vile fanani, hadhira, fani, tukio, mahali pamoja na wakati wa utendaji.
Ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake (Balisidya, 1983).
Fasili hizi zinasisitiza kwamba fasihi simulizi inategemea uwepo wa fanani, hadhira, jukwaa na mada.
Hivyo kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha kisanaa ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa kwa njia ya mdomo au masimulizi.
Nadharia ya fasihi simulizi ni mawazo yanayotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jambo fulani katika fasihi simulizi.
Kwa kufanya hivyo, nadharia hizo zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo kwa mfano utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, uchongaji, jando na unyago umeathiriwa na ujio wa wageni.
Watafiti wa Kimagharibi na wa Kiafrika wameangalia mambo mengi yaliyoikabili fasihi simulizi ya Kiafrika na mawazo yao ni kama yafuatavyo:
MSAMBAO
Waasisi wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na wanaubadilikaji taratibu ambao waliamini kuwa kufanana kwa fani mbili za kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa za kimaendeleo.
Wanamsambao wanaamini kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea, sababu ya msingi ya mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani, jamii hizo ziliwahi kukutana kwa namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana baadhi ya mila na desturi.
Wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa kutoka katika jamii imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo dhaifu.
Hivyo basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi ya Kiafrika ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda sehemu nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano ushairi simulizi wa Kiswahili ulitoka Uarabuni na Uajemi kuja Afrika.
KISOSHOLOJIA
Nadharia hii ina mihimili mitatu ambayo ni ule wa Umahususi, mkazo katika utendaji na dhima ya fasihi simulizi katika jamii. Umahususi, ulijikita zaidi katika jamii peke yake badala ya taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla kama walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi.
Katika Utendaji, Wanasosholojia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji wa kazi mbalimbali za fasihi simulizi.
Kutokana na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya fasihi wana ujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa
husika na jambo hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele cha utendaji.
Katika msisitizo kuhusu dhima ya fasihi simulizi katika jamii, wanaamini kuwa uamilifu wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika.
Kutokana na mawazo ya wananadharia, hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni ndani ya jamii za Kiafrika zenyewe na si vinginevyo.
UTAIFA
Nadharia hii ilizuka kwenye vuguvugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa wanadai kuwa wananadharia wa utandawazi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za Kiafrika.
Kwa kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni na upendeleo wa kibepari kuwa Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya ustaarabu na walistahili kustaarabishwa na Wazungu kupitia mlango wa ukoloni.
Utaifa umeasisiwa na Adeboye, Babalola, Daniel Kunene na Clark. Katika nadharia hii wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa kuondoa kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti hawakuwa tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti. Wanaona ni kosa kubwa kufanya utafiti bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.
Ili kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni lazima kuhusisha wataalamu na wanachuo wa taifa au jamii hiyo kwa sababu wataalamu na wanazuoni hao ndio wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.
HULUTISHI
Nadharia hii iliasisiwa na wanazuoni wa Kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni wamechangia sana katika kukuza taaluma ya fasihi ya Kiafrika. Wananadharia hawa wanaona kuwa fasihi ya kigeni na ya kijadi zimeathiriana na kuingiliana.
Miongoni mwa waasisi na wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Mulokozi, Johnson na Ngugi wa Thiong’o. Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika inaweza kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na wa kijadi.
Hata hivyo, fasihi simulizi ya Kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni lakini ilianza kupata athari mara baada ya ujio wao. Athari na mwingiliano wa fasihi simulizi hauonyeshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwa kuwa fasihi yoyote lazima iathiriwe na iathiri fasihi nyingine.
Hivyo basi kila jamii au taifa huwa na fasihi yake na utamaduni wake ambapo maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza kuathiriana na hivyo kuathiri pia fasihi ya jamii husika