@mashele

Sura ya 5: Mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi

Utangulizi
Hadi sasa mitindo tuliyoijadili ni ile ambamo mawasiliano yanatekelezwa katika mazingira yaliyo rasmi, yaani yanayowalazimisha wanaowasiliana kufuata taratibu au kanuni maalum za matumizi ya zana za kiisimu. Lakini katika hali ya kawaida ya maisha si muda wote binadamu anakuwa kwenye mazingira yanayomtaka awasiliane kirasmi. Na kwa kweli idadi kubwa ya mawasiliano yanayofanywa na wanadamu hufanywa kwenye mazingira yasiyo rasmi. Sura hii itayaainisha mazingira hayo pamoja na zana za kiisimu zinazotumika katika mawasiliano yasiyo rasmi.
Mawasiliano Yasiyo Rasmi
Mawasiliano yasiyo rasmi ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku mathalani nyumbani (yaani mazungumzo kati ya baba, mama, watoto, watumishi wa nyumbani n.k.), baina ya wasafiri kwenye vyombo vya umma vya usafiri, kama vHe mabasi, magarimoshi, meli n.k., baina ya marafiki mitaani, michezoni, kwenye tafrija au kumbi mbalimbali za starehe, kama vile mabaa, majumba ya dansi; n.k. Hata kwenye mazingira rasmi, kwa mfano vtwandani, vyuoni, maofisini watu wanaweza kutumia mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi ilimradi wawe wanazungumzia mada isiyoambatana moja kwa moja na kazi au taaluma wanayoishughulikia awenye mazingira hayo rasmi. Kwa mfano, waalimu wanaposalimiana na kajuliana hali za nyumbani kwao kwa kawaida hawatumii mtindo wa Mtaaluma, bali wanatumia mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi hata kama mawasiliano hayo yanafanywa kwenye Ofisi ya Waalimu.
Aidha wakati tuandikapo barua za kibinafsi kwa ndugu na marafiki, au kumbukumbu binafsi kwenye vijitabu vya kumbukumbu na maandishi mengineyo ya namna hiyo, huwa tunatumia mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi.
Sifa za Mtindo wa Mawasiliano Yasiyo Rasmi:
Sifa Zisizo za Kiismu
(i) Kutokuwepo kwa hisia ya mazingira Rasmi ya mawasiliano
Sifa kubwa ya mtindo huu ni kule kutokuwepo hisia ya mazingira rasmi ambamo mawasiliano yanatekelezwa baina ya wazungumzaji au waandikianao. Yaani watu wanaowasiliana lazima wajisikie huru na hawabanwibanwi na hali yoyote inayowalazinusha kutumia zana fulani tu za kiisimu. Vilevile washiriki katika mawasiliano lazima wajione kuwa na hali na haki sawa ya kushiriki katika mawasiliano hayo bila mmojawapo kumdhalilisha au kumtukuza mwenzake. Mfano mzuri wa mawasiliano ya namna hii ni mazungumzo au barua kati ya marafiki wawili kuhusu maisha yao ya kawaida ya kila siku.
(ii) Kutotayarisha Awali Mada za Mawasiliano
Mazungumzo na pengine hata maandishi katika mtindo huu kwa kawaida huwa hayatayarishwi rasmi mapema. Tunazungumza jambo lolote linalotujia kichwani bila matayarisho maalum. Yaani mawasiliano katika mtindo huu aghalabu ni ya papo kwa papo.
(iii) Uwezekano wa Kubadilisha Mada Bila Madhara
Kutokana na kutotayarishwa awali kwa mada za mawasiliano mada hizo zinaweza kubadilishwa mara kwa mara bila kuleta vurugu yoyote katika mawasiliano. Kwa nlfano, mtu anapozungumza na rafiki yake kuhusu, mathalani, mikasa iliyompata, basi anaweza mara akaielezea mikasa hiyo, mara akarukia mada ya matatizo yake ya nyumbani, halafu akaendelea tena kusimulia mikasa yake, na pengine akabadili tena mada bila hata yeye kujua, na wakati mwingine anaweza hata akasahaujambo alilokuwa akilizungumzia mwanzoni. Na mabadiliko yote haya ya mada za mawasiliano aghalabu hayawezi kumkera au kumuudhi rafiki yake kwa sababu huu ndio utaratibu wa mazungumzo ya namna hii.
Sifa za Kiisimu:
Msamiati
Msamiati unaotumika zaidi katika mtindo huu una sifa kadha bainifu. Nazo ni:
(i) Matumizi Mapana ya Tamathali za Usemi
Mawasiliano katika mazingira yasiyo rasmi yanatakiwa yawe na mvuto nikubwa ih kuwawezesha wanaowasiliana wasichushwe. Sharti ikumbukwe kuwa mawasiliano ya namna hii hayadhibitiwi na chombo chochote kwa njia mathalani, ya mitihani usaili n.k. Hivyo wanaoshiriki kwenye mazungumzo au maandishi ya mtindo huu wanafanya hivyo kwa hiari yao. Ili kuwashawishi washiriki kwa dhati katika mawasiliano hayo inabidi zitumike zana za kiisimu, hasa msamiati, ambazo zitawavuta wafanye hivyo, Tamathali za usemi, kama vile tasfida, sitiari, mishabaha n.k zimedhihirika kuwa na uwezo mkubwa wa kuipamba na kuitia ladha lugha hivyo zinatumika sana kwenye mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi. Kwa mfano, kati ya sentensi mbili zifuatazo:
1. Yanga ingefungwa magoli mengi kama si kwa uhodari wa Joseph Fungo,
2. Fungo bwana ni nyani kwelikweli, bila yeye lango la Yanga lingekuwa kapu la magoli,
sentensi ya pili, inayotumia mishabaha, ina mvuto mkubwa kwa msikilizaji au msomaji kuliko sentensi ya kwanza ambayo ina taarifa ya kawaida. Sentensi ya pili imemfananisha mlinda mlango Fungo na nyani kwa uhodari wa kudaka mpira. Pia mlango (goli) wa Yanga umelinganishwa na kapu ambalo hubeba chochote kinachotupiwa humo. Katika mawasiliano yasiyo rasmi sentensi ya pili ndiyo itakayotumiwa zaidi kuliko ile ya kwanza.
(ii) Matumizi Mapana ya Simo
Simo au misimu ni maneno yanayotumiwa na makundi maalum ya watu katika jamii yaliyojitenga kwa kufuatana na mambo yanayopendelea, mazoea, kazi au shughuli yao, nafasi yao katika jamii n.k. Kwa kuwa watu wanaoshiriki katika mawasiliano yasiyo rasnu aghalabu huwa na uelewano na ushirikiano wa ndani zaidi baina yao, basi matumm ya simo zinazohusiana na kikundi cha wanaowasiliana huwa ni jambo la kawaida kabisa. Kwa mfano, iwapo wanaowasiliana ni wafanyabiashara, wanafunzi, askari au majangiri, basi simo watakazozitumia zitahusiana na shughuli hizo za biashara, uanafunzi n.k. Moja ya malengo ya kutunua simo ni kutaka mada ya mawasiliano isieleweke na watu wengine. Wanafuozi wa shule wanaposema, kwa mfano, “naamsha ndege” au “nafunga ofisi” kwa maana ya kutaka kutoroka toka masomoni nia yao ni kuwaficha waalimu wasijue (wanafunzi) wanapanga kufanya nini. Matumizi ya simo zifuatazo vilevile yana lengo la kuficha mambo yanayozungumziwa:
kutoa michuzi, mchicha, chauchau, chai, kuzunguka mbuyu
-
kwa maana ya kutoa rushwa.
kumtoa mtu upepo kumkalia, kumwegemea, kumkamua mtu
-
kwa maana ya kutumia hela zake kwa ujanja; au hata kumwibia hizo hela.
Sarufi Maumbo
Mawasiliano katika mtindo huu aghalabu huwa ni diazungumzo ya ana kwa ana kati ya ndugu, marafiki, n.k. Hali hii inafanya mawasiliano ya namna hii yatumie sana nafsi ya kwanza na ya pili ili kuwawezesha washiriki katika mawasiliano wajibizane. Hata waandikianapo barua ndugu na marafiki kwa kawaida hutumia sana nafsi ya kwanza na ya pili. Hivyo matumizi mapana ya nafsi ya kwanza na ya pili ndiyo sifa maahun ya kisarufi maumbo ya mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi.
Fonetiki
Kuna sifa mbili za kifonetiki zinazojitokeza waziwazi kwenye mtindo wa mawasiliano yasiyo rasmi, nazo ni:
(i) Matumizi Mapana ya Vifupisho na Maneno Yaliyokatizwa
Kwa kawaida washiriki katika mawasiliano yasiyo rasmi huwa na usuli unaoeleweka baina yao. Mathalani, marafiki wawili wakikutana kuna uwezekano mkubwa kwamba kila mmoja wao atakuwa anafahamu habari nyingi kuhusu mwenziwe, kwa mfano huyo rafikiye anatokea sehemu gani ya Tanzania, anaishi wapi sasa, ameoa au ameolewa, anafanya kazi wapi, anatumia usafiri wa namoa gani kwenda kazini, n.k. Hivyo kwa kutumia usuli huu unaofahamika baina yao mara nyingi watu kama hawa hupendelea kutumia vifupisho vya maneno au hata kuyakatiza kwa lengo ama la kuchapusha mawasiliano hayo ama kuyakoleza. Kwa mfano katika mawasiliano yasiyo rasmi mara nyingi tunasema:
“Naenda Moro” badala ya “Ninakwenda Morogoro”,
“Nilikuwa Dar” badala ya “Nilikuwa Dar es Salaam”,
“Nafanya kazi SHIHATA” badala ya “Nafaaya kazi Shirika la Habari la Tanzania”,
“Amekwenda Bima” badala ya “Amekwenda Shirika la Bima la Taifa”,
“Sendi” badala ya “siendi”,
“Keshaenda” badala ya “Amekwisha kwenda”, n.k.
(ii) Matumizi ya Lafudhi Huria
Lafudhi ni namna au jinsi ya utamkaji wa maneno. Katika mazungumzo yasiyo rasmi mzungumzaji ana uhuru wa kutumia lafudhi yoyote almradi aeleweke na mwenziwe. Anaweza kuyatamka maneno ya Kiswahili kwa namna inayoathiriwa sana na lahaja za Kiswahili au hata lugha nyinginezo kama vile Khnakonde, Kisukuma, Kichaga, Kihindi n.k. Angalia mfano ufuatao wa Kiswahili cha lafudhi ya Kimakonde:
Nauli chilipi, Mchachani ntakwenda, na chindimba ntacheja
(= Nauli silipi, Msasani nitakwenda na sindimba nitacheza).
Muundo wa Sentensi
Sentensi zinazotumika katika mtindo huu (hasa wakati wa mazungumzo) kwa kawaida huwa ni za mkato. Hii inatokea kwa sababu kwanza, mara nyingi watu wanaoshiriki katika mawasiliano yasiyo rasmi huwa wana usuli unaofanana na pili, mazingira yao ya mawasiliano yanawaruhusu kutumia ishara mbalimbali kama vile kuinua mikono, kukonyeza, kupiga mluzi n.k. kujaliza mawasiliano hayo. Kwa mfano, kama marafiki wawili watapatana kukutana mahali fulani na wakapanga saa ya kukutana, mmojawapo akichelewa na kuulizwa na mwenziwe “Vipi?”, swali hilo litaeleweka kahisa japo ni sentensi ya neno moja tu. Katika mazingira haya “Vipi?” ni sentensi iliyokatizwa. Sentensi kamili, mathalani, ingekuwa “Vipi mbona umechelewa?” au “Vipi ulipata matatizo ya usafiri?” n.k.