Hadithi; MWANAMALUNDI
Sehemu Ya Tisa

 ILIPOISHIA...
 "Mwanangu mpenzi, Mungu asifiwe ile shoka nilikuwa sikosi kuiangalia. Ilikuwa ikipanda tu bila kushuka. Ilipofika juu sana ilisimama kwa miaka Saba. Hatimaye nilifanikiwa kuiona ikiteremka, nilijawa na furaha isiyo kifani. Tena iliteremka kasi sana kisha ilitulia kwa muda wa siku moja. Kisha ikaanza kushuka pole pole. Leo asubuhi nilifurahi mara baada ya kufika ulipoiweka. Isiende mbele wala kurudi nyuma na punde nawe ukatokea. Pia yale maziwa uliyoyaacha hayakuganda ila yalitaka kuganda miaka miwili iliyopita. " Aliongea Mama huyo.
 Na kweli aliyakuta bado mabichi.

 ENDELEA...
 Huko Nera alimkuta yule yule Mtemi Masanja. Watu walipomuona Igulu walianza kunong'onezana, hata mwisho tetesi zikamfikia Mtemi, ambaye bila kukawia alimfukuza pale Nera. Hivyo yeye pamoja na familia yake walihama na kuelekea Seke katika Wilaya ya Shinyanga karibu na Mjini Shinyanga.
 Huko walimkuta Mtemi Mahizi, ambaye alikuwa mwema sana akawaruhusu kukaa. Kama tulivyosoma hapo Mwanzo Mwanamalundi alikuwa na sifa mbali mbali. Mtemi huyo alipomfahamu hakumfukuza.
 Aliendelea kukaa huko huku akiwa hana wafuasi tena maana hukuwa na hamu ya ngoma wakati huo.
 Ilitokea usiku mmoja Wamasai walikuja kijijini kuiba ng'ombe. Wakaiba mamia ya ng'ombe huku wenyeji wakilia na kupayuka hovyo kwa kuogopa.
Mwanamalundi hakukawia alichukua dawa na kuwafuata kisha akawapita. Akamwaga dawa huku na huko. Wengine walipofuka, wengine wakafa na wengine wakapatwa na ukichaa. Waliosalia walitimua mbio mikono mitupu, huku wakitupa chini mikuki yao. Hapo wenyeji woga ukawaisha wakawafata Wamasai na kuwaua.

 Mnamo mwaka 1934 Mwanamalundi alifariki, katika kijiji cha Ngalitu, huko Seke. Siku hiyo wengine waliwehuka, wengine wakapatwa na ukichaa na wengine kujiua. Waliowehuka walikimbia kutoka Seke, wakipitia Badi, Nera, Bulima, Usumao, Bukumbi hadi Ziwa Viktoria, Mwanza kwa ukichaa walioupata.
 Ajabu ya pili ilitokea mwezi Novemba mwaka ule ule. Lilitokea wingu dogo, saa Nane adhuhuri lililoleta mvua ya rasharasha, Mvua hiyo ilinyesha kwenye kaburi lake tu.
 Ghafla ulizuka moshi mzito sana ambao juu ulijinyonganyonga kama nyoka. Watu wakaanza kusema Igulu anakwenda Mbinguni.
 Baada ya kufa Sita au Mwanajishosha mwanaye alimrithi. Naye akahama Seke na kwenda Shinyanga na mke wake. Huko alikaa kwa miaka mingi. Mkewe alipopata mimba ya kwanza, mtoto akiwa tumboni alisema,
 "Dada nishoshage kunzengo gwa ng'wa guku ulu tuja koi, kugwigasha tubeje noi. ( Baba nipeleke kwenye mji wa babu, huko tukienda tutakaa raha musharehe.)"
 Hivyo Sita na mkewe walihama pale na kurudi Seke, ambako hata sasa wanaishi.

__________MWISHO___________

NB:
Namshukuru Muumba wa Mbingu na Dunia kwani bila yeye tusingekuwa hapa huku tukivuta pumzi ya bure bila kulipia. Pia kwa msaada wa Nyanja. blogsport. co. ke pamoja na mhandishi wa Kitabu cha MWANAMALUNDI ndio walionifanya niimalize vyema.
info.masshele@gmail.com