Alizaliwa mwaka 1863 katika mji wa Besease katika jamii ya Ashanti yenye dhahabu nyingi, Ghana ya sasa, magharibi mwa Afrika. Kaka yake Nana Akwasi Afrane alikuwa ndiye Edweso (kiongozi, au chifu) wa milki ya Ashanti wakati huo. Nana Yaa Asantewaa akiwa bado binti alijishughulisha sana na kilimo. 

Kaka yake (chifu Akwasi) alipokuwa Edweso (kiongozi) alituma askari wake kwenda mapiganoni dhidi ya wakoloni. Baadae aliwekwa kizuizini na wakoloni katika visiwa vya Ushelisheli pamoja na mfalme Prempeh I. Akiwa kizuizini, Nana Akwasi Afrane alimteua dada yake NANA YAA ASANTEWAA kuwa malkia wa milki ya Asante. 
Mwaka 1899 gavana wa wakoloni Waingereza Frederick Hodgson aliitisha mkutano mjini Kumasi ili kulazimisha apewe kiti kilichotengenezwa kwa dhahabu tupu ambacho ni alama takatifu ya Ashanti ambapo askari wa kikoloni walishindwa kukipata kiti hicho, hii ni baada ya kufikiri kwamba ugumu wa kuwatawala Waashanti ungeisha baada ya kupata kiti hicho cha dhahabu. Nana Yaa Asantewaa alimteua mjukuu wake mkubwa kuwa mkuu wa miliki ya Ashanti mara baada ya kufariki kaka yake. 

Alipoona wanaume wa Ashanti wako kimya baada ya hotuba ya gavana wa Uingereza kuwateka baadhi ya viongozi wao, malkia Asantewaa alichukizwa na kimya hicho cha wanaume na kuamua kusimama na kuzitazamanishani za kijeshi kwenye mavazi ya gavana huyo kwa muda mrefu, kisha akzungumza maneno ya kishujaa, na kuwaambia wanaume kuwa wamegeuzwa kuwa wanawake kwa kauli za Waingereza. Ndipo alipoteuliwa awe kiongozi wa kukabiliana na wakoloni.
Nana Yaa Asantewaa alikuwa na kikosi chenye wapiganaji 5,000 kati yao kulikuwepo na waliokuwa na mashaka. Hawakumuamini sana katika kuhimili vishindo vya mapigano. Pia aliwapa morali na kuwaambia maneno ambayo mpaka sasa ni maarufu sana katika historia ya Ghana, alisema hivi;
Sasa ninaona kwamba baadhi yenu wanahofu ya kusonga mbele kupambana kwa ajili ya mfalme wetu. Kama ingelikuwepo siku za ushujaa wa akina Osei Tutu, Okomfo Anokye, na Opuku Ware I, msingekaa kimya tu na kutazama viongozi wetu wanachukuliwa bila kupigwa risasi. Hakuna mzungu ambaye angediriki kuzungumza chochote kwa machifu wetu kama gavana alivyozungumza asubuhi ya leo. Ni kweli kwamba ushujaa wa Ashanti haupo tena? Siwezi kuamini hilo. Ninasema hivi: kama ninyi wanaume wa Ashanti hamtasonga mbele, sisi tutasonga. Nitawaita wanawake wenzangu na tutapambana na wazungu. Tutapambana nao mpaka mtu wa mwisho kati yetu afe kwenye uwanja wa medani”

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mwanamke kupewa mamlaka ya kivita katika milki ya Ashanti.
Mwanzoni mwa mwaka 1900 malkia Nana Yaa Asantewaa aliitisha mgomo katika ngome ya Ashanti mjini Kumasi. Gavana wa wakoloni alituma kikosi cha askari 1,400 kwenda kuwaangamiza walioitisha mgomo wa kutotoa kiti cha dhahabu. Katika mapambano hayo, malkia Nana Yaa Asantewaa na washauri wake wa karibu 15 walitekwa na kupelekewa gerezani visiwa vya Ushelisheli. Ngome hiyo inatunzwa mpaka sasa kwa heshima ya malkia huyo.  
Jeshi la Ashanti likiongozwa na malkia liliikaribia kambi ya Kumasi ya jeshi la Uingereza lakini hwakuwa na silaha za kutosha kukabiliana na jeshi hilo la Uingereza ambalo liliongeza vikosi vyake kutoka Nigeria, na Sierra Leone. Malkia mwenyewe alikuwa akipanga hatua za kuchukua na alishiriki mapiganao.
Malkia Nana Yaa Asantewaa alifariki mwaka 1921 akiwa gerezani huko Ushelisheli. Miaka mitatu baada ya kifo cha malkia Nana Yaa Asantewaa, mjukuu wake Asantehene na washirika waliobaki walirudishwa katika milki yao ya Asante. Akiwa katika milki ya Ashanti, Asantehene alihakikisha kwamba mwili wa malkia wao pamoja na ile ya washirika wengine waliouawa inarudishwa katika milki ya Asante kwa ajili ya mazishi ya heshima za kimila.
Ndoto ya malkia Nana Yaa Asantewaa ilikuwa ni kuweka Ashanti kuwa huru kutoka katika utawala wa wakoloni. Ndoto hiyo ilitimia mnamo tarehe 6 mwezi wa tatu mwaka 1957 ambapo milki ya Ashanti iliachwa huru na kuwa Ghana ya sasa.
Uzoefu wa kuona mwanamke anashiriki shughuli za siasa na kijeshi ulikuwa ni mgeni machoni pa wakoloni karne ya 19 katika Afrika. Wao walizoea shughuli hizo kufanywa na wanaume. Nana Yaa Asantewaa amekuwa ni kielelezo cha thamani kubwa katika historia ya Ghana na Afrika kwa ujumla. Alikuwa na staha ya ndani ambayo ilimsaidia sana kujiamini na kuona yeye ni mtumishi wa Ashanti.
Milki ya Ashanti iliamua kuwapa kipaumbele wanawake jambo ambalo wakoloni walizidi kuwa na mshangao, ni kutokana na jamii ya kijiji cha Akan kuanzisha uongozi maalumu kijijini hapo. Uongozi huo ulikuwa ni kuteua wanawake wa kusikiliza na kutatua masuala mbalimbali ya wanawake katika jamii hiyo. Kiongozi mwanamke aliyeteuliwa alikuwa akiitwa Mpanyinfo au Aberewa
Katika milki ya Ashanti wanawake walikuwa ndio walinzi wa kwenye malango makuu yaani magetini ambapo Nana Yaa Asantewaa kabla ya kuteuliwa kuwa malkia wa milki ya Ashanti alikuwa mlinzi wa lango kuu la himaya ya mfalme. Kiti alichokuwa akikalia kilitengenezwa kwa dhahabu tupu na mpaka sasa ni alama muhimu katika historia ya Ghana. Anakumbukwa hadi leo na picha yake ilionekana kwenye hela ya Ghana Cedi 20, baada ya kupata uhuru.

Malkia Nana Yaa Asantewaa amekuwa kielelezo kinachopendwa sana nchini Ghana kwa juhusi na ushujaa wake wa kuwa kiongozi mwanamke kupambana na wakoloni. Amekuwa akidhaniwa kwamba mzimu wake bado unailinda Ghana, na anaimbwa kwa maneno haya kwa lugha ya Ashanti;
“Koo koo hin koo
Yaa Asantewaa ee!
Obaa basia oko premo ano
Ogyina ampremo ano ee!
Waya be agyaye
Na wabo mmode”
Tafsiri ya maneno katika wimbo huo  ni kama ifuatavyo, kwa Kiswahili;
“Yaa Asantewaa
Mwanamke uliyepambana
Mbele ya mababu
Umefanya mambo makubwa
Umefanya vizuri”
 
 
mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa sanaa lugha na historia pamoja na lugha na TEHAMA