• Ni mmoja wa wanawake wa kwanza nchini ambaye amechukua kozi ya umahiri kwenye teknolojia hiyo inayokua kwa kasi duniani.
  • Kwa sasa amejikita katika kugawa maarifa kuhakikisha wanawake wenzie na Watanzania wote wanachangamkia fursa za teknolojia hiyo.
  • Amesema blockchain itaondoa upigaji katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kikiwemo kilimo.
Dhana ya kutokufanya kazi nyingine unapoajiriwa inazidi kupungua kwa baadhi ya watu walioona fursa zinazoweza kumsaidia kujiongezea kipato zaidi kupitia teknolojia.
Hii ni kwa sababu matumizi ya teknolojia hayahitaji uwe katika eneo hilo moja kwa moja bali unaweza kufanya vitu vingine kupitia fursa zilizopo mtandaoni.
Sandra Chogo (42), ambaye ameajiriwa kama mkaguzi wa mahesabu, aliona fursa nyingine kwenye masuala ya mfumo wa ‘Blockchain’ na kuamua kuchangamkia fursa hiyo ya teknolojia inayokua kwa kasi zaidi duniani.
Kwa kifupi blockchain ni teknolojia ya mfumo unaomruhusu mtu kutuma au kuhifadhi vitu vyake zikiwemo nyaraka na pesa kwa njia ya mtandao bila kumuhusisha mtu mwingine (third party) au kupitia kwa sehemu nyingine ambayo haihusiki.
Katika teknolojia hiyo ya blockchain ni vigumu mtu yeyote aliyepo kwenye mfumo kufanya uchakachuaji katika masuala ya miamala bila wahusika wote kuthibitisha.
Sandra amekuwa mmoja wa wanawake wa kwanza nchini ambaye amechukua kozi ya umahiri kwenye masuala hayo na sasa anagawa tu maarifa kwa wengine wanaotaka kutumia fursa hiyo vema kujipatia kipato halali.
Sandra Chogo akitoa mhadhara katika moja ya makongamano kuhusu matumizi ya teknolojia ya blockchain. 
Teknolojia hii katika nchi zinazoendelea ni mpya. Mwanamke kama Sandra ambaye siyo mhandisi wa kompyuta kitaaluma alianza lini kujua teknolojia hiyo ambayo inasadikika kuwa ni mapinduzi makubwa ya pili kwenye matumizi ya intaneti?
“Nimejua mambo ya blockchain kwa mara ya kwanza mwaka 2016 na niliamini ni utapeli lakini lakini kadri nilivyokuwa naiona kwenye vyombo kadhaa vya habari nikaanza kuiamini,” anasema Sandra..
Baada ya kujua kuhusu fursa hiyo, alijituma zaidi na mwaka 2018 alijiunga na Chuo Kikuu cha Nicosia cha kwanza duniani kutoa Shahada ya uzamili kwenye pesa za kidijitali (Msc in Digital Currency) ili aweze kubobea zaidi.
Miongoni mwa masuala yaliyomo katika shahada hiyo anayoendelea kuisoma kwa sasa ni teknolojia ya hiyo ya blockchain.

Hata hivyo, Sandra anajivunia kuwa miongoni wa wanawake wa mwanzo kabisa Tanzania kusoma masuala hayo katika kipindi ambacho watu wengi wakiwemo wahadhiri hawaielewi kabisa.
Vilevile imemfungulia fursa ya kuwa mzungumzaji kwenye mikutano mbalimbali ili kuwaelewesha baadhi ya watunga sera na wadau mbalimbali juu ya teknolojia hiyo mpya.
“Nimepata fursa ya kuwaelewesha wabunge wa Afrika Mashariki na viongozi wengine wengi wa Tanzania na nje ya nchi kwa njia ya mtandao,” amesema Sandra.
Hata hivyo, Sandra ambaye ni mama wa watoto watatu, ameweka wazi kuwa anakumbana na  changamoto ya watu wengi  kuchanganya kati ya blockchain na Bitcoin.
Bitcoin ni miongoni mwa sarafu za awali zisizoshikika za kielektroniki ambazo zinatumia teknolojia ya blockchain kufanya miamala.
Kwa Sandra ufahamu mdogo wa masuala hayo katika jamii ni fursa kwake ya kuwafundisha wengine.
Moja wapo ya kazi aliyojipa baada ya kupata mafunzo hayo ni kuwatofautishia watu vitu hivi na amekuwa akifundisha kozi ya matumizi ya teknolojia hii kwa watu binafsi na vyuo vinavyohitaji kujifunza.
Sandra pia hutoa maarifa ya teknolojia hiyo ya blockchain kupitia vipindi mbalimbali vya televisheni na redio. 
“Utakapo ielewa blockchain utaziona fursa wewe mwenyewe mfano mimi kwangu nimeona fursa ya kufundisha,” amesema Sandra anayeeleza kuwa hadi bosi wake ofisini anamuunga mkono katika kuwekeza katika taaluma ya masuala hayo.
Hata hivyo, amesema fursa nyingine zilizopo katika matumizi ya blockchain ni kutengeneza programu zake, kufunguliwa kampuni ya blockchain, kutumika katika huduma za kilimo na sehemu nyinginezo.
Kwenye kilimo blockchain, Sandra amesema itaondoa madalali na hivyo kuongeza kipato kwa mkulima ambacho huwa kinachukuliwa na dalali katika mauzo ya mazao yao.
Pia, wakulima wataweza kupata masoko mengi zaidi na mikopo itakayowaweka pamoja hivyo kufanya washirikiane kwenye zana za kilimo kama matrekta ambayo wanaweza kuchanga fedha na kununua kwa pamoja kupitia mfumo huohuo wa blockchain
Sandra amewataka wanawake wabadilishe mitazamo na kuwaambia kwamba wanaweza na wajaribu kufanya mambo makubwa kwenye teknolojia na hapo wataheshimika zaidi katika jamii inayokuzunguka.
“Wanawake tuchangamkie fursa kabla wanaume hawajaziona haswahaswa ukizingatia mwanamke mwezenu ndiyo nimekuwa ‘sterling’ (kiongozi),” amesema Sandra.
Sandra, mama wa watoto watatu, amekuwa kinara wa kufundisha teknolojia ya blockchain nje na ndani ya nchi. Picha zote| Kwa hisani ya Sandra Chogo.