SIFA ZA SHUJAA KATIKA UTENDI: UCHAMBUZI WA SIFA ZA SHUJAA KATIKAUTENZI WA FUMO LIYONGO NA UTENZI WA NYAKIIRU KIBI


                                                 

Mwandishi,
Sarah Mayunga



Iks/UDSM



@mashele/kiswahili

IKISIRI

Makala haya yalikusudia kuchunguza sifa za shujaa katika tendi teule za Kiswahili. Mashujaa ambao tutawaangazia ni kutoka katika kitabu cha Utenzi wa Fumo Liyongo wa Muhammed Kijumwa (1913) na Utenzi wa Nyakiru Kibi wa M. Mulokozi (1997). Madhumuni makuu katika Makala haya;


Mosi, kubainisha sifa za shujaa zilizoainishwa na Mulokozi, pili kuchunguza sifa hizo kama zinazojidhihirisha katika tendi teule na tatu ni kubainisha sifa za shujaa zinazojidhihirisha katika tendi teule tofauti na zilizoainishwa na Mulokozi. Kwa kawaida mashujaa huwa na sifa za kipekee na hutekeleza majukumu ya kimsingi katika jamii zao. Nadharia iliyotumika katika utafiti huu ni Nadharia ya Ruwaza ya Shujaa iliyoasisiwa na Joseph Campbell (1904-1987) na kuhakikiwa na Timothy Lynns (2009).


Nadharia hii ilitumiwa na mtafiti kueleza upeo na mipaka ya utafiti huu na pia ilisaidia kuchanganua data. Aidha utafiti huu ulihusisha ukusanyaji wa data moja kwa moja kutoka Maktabani.


 Mahali pa utafiti palikuwa ni maktaba ya TATAKI yaani Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Inatarajiwa kuwa utafiti huu utakuwa mchango mkubwa katika jamii ya wasomi hasa wanaoshughulikia fasihi ya jadi.


1.0 UTANGULIZI
Watafiti wengi wa Kiafrika kama Okpewho (1979), Mbele (1986), na Mulokozi (1999) walifanya utafiti wa tenzi za Kiafrika. Matokeo ya uchunguzi wao yalibainisha sifa za tendi na kudhihirisha kuwa Afrika kuna tendi kinyume na madai ya Finnegan (1970) na Knappert (1983) ambapo walidai kuwa Afrika hatuna tendi. Baada ya watafiti wa Kiafrika kufanya utafiti juu ya Tendi za Kiafrika na kuhitimisha kuwa Afrika kuna tendi. Hivyo makala haya yatachunguza sifa za shujaa wa kitendi.


Mada ya Makala hii inaitwa uchunguzi wa sifa za shujaa katika tendi teule kwa kuzingatia sifa zilizobainishwa na Mulokozi, pia Makala haya yatachunguza sifa hizo namna zinavyojidhihirisha katika tendi teule, vilevile Makala haya yataangazia sifa nyingine za shujaa zinazojitokeza katika tendi teule ambazo hazikuainishwa na Mulokozi.

 Katika kuchunguza mada hii mtafiti alitumia nadharia ya ruwaza ya shujaa iliyoasisiwa na Joseph Campbell (1904-1987) na kuhakikiwa na Timothy Lynns (2009) ambapo ruwaza hizo za shujaa zilisaidia katika kubaini sifa za shujaa wa kitendi.


2.0 NADHARIA YA RUWAZA YA SHUJAA
Nadharia ya Ruwaza ya Shujaa iliasisiwa na Joseph Campbell (1904-1987) na kuhakikiwa na wanafalsafa wengine wa fasihi na soshiolojia kama vile Rank (1999) na Timothy Lynns (2009). Joseph Campbell anaeleza kuwa ili shujaa katika tendi aweze kuafikia jaala yake, lazima apitie hatua mbalimbali zitakazomwezesha kufikia azma yake.

Campbell alifafanua misingi mitatu ya nadharia hii. Kwanza, kuondoka kwa shujaa. Katika msingi huu shujaa ni sharti aondoke katika taifa lake na aiache jamii yake. Campbell anaeleza kuwa kuondoka huku kwa shujaa huwa na visababishi kadha wa kadha.


Msingi wa pili ni kufundwa na kushindwa kwa shujaa. Katika msingi huu shujaa hupatana na mambo mbalimbali. Shujaa hujitenga na kuishi peke yake pale ambapo baadaye hukumbana na adui ambaye hupigana naye vita vikali,
Msingi wa tau ni kurejea na kurudi nyumbani kwa shujaa.


Baada ya kushindwa na maadui pamoja na mahasidi wake, shujaa huamua kurejea nyumbani ili aweze kuungana na wanajamii wake. Anaporudi nyumbani, shujaa hukumbana na adui mwingine na vita vingine vikali huzuka na wakati mwingi shujaa huibuka mshindi. Shujaa hurejea nyumbani akiwa amebadilika. Ranks alichangia nadharia hii kwa kudai kuwa mhusika mkuu katika tendi huwa kwa wakati mwingi amezaliwa kutoka kwa tabaka la juu.


 Anafafanua zaidi kuwa kuzaliwa kwa mhusika huyu hukumbwa na matatizo anuwai na huwa ni kwa njia ya kimiujiza na anguko lake husababishwa na usaliti wa mtu wa tabaka la chini. Timothy Lynns 2009 alihakiki maoni ya Joseph Campbell na kueleza kuwa licha ya Campbell kufafanua kuwa wahusika wakuu katika tendi ni wanaume tu, kuna kuna idhibati kuwa kuna kazi zingine za kifasihi ambapo wahusika wakuu ni wanawake.


 Hivyo nadharia hii itaufaa utafiti wa Makala hii kwani vipengele vyake vimebeba sifa za shujaa,
MAPITIO YA MAANDIKO NA USULI WA TENDI TEULE
3.01 DHANA YA TENDI
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa utendi ni ushairi wa matendo.


Ni utungo mrefu wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Matukio hayo yanaweza kuwa yakihistoria na visakale. Ufafanuzi huu wa Mulokozi umepiga hatua mbele kwa kueleza utendi kama ushairi wa matendo, aidha fasili hii imesaidia katika kuandaa Makala hii kwa sababu imefanikisha katika uteuzi wa tendi.



Wamitila (2003) anaeleza kuwa utendi ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na kwa mtindo wa hali ya juu, matendo ya mashujaa au shujaa mmoja.

 Anafafanua zaidi kwa kueleza kuwa utendi huwa na sifa nyingi na huweza kuleta pamoja hadithi ya shujaa, visasili, historia, pamoja na ndoto za taifa fulani. Fasili hii inatupatia utata inapoeleza utendi kama shairi refu la kisimulizi. Utata unajitokeza katika kupima urefu wa shairi na kipimo cha kupima urefu huo ni kipi? Pia mpaka wa ushairi mrefu na ushairi mfupi ni upi? Hivyo fasili hii inahitaji maelezo Zaidi.


Kwa ujumla, kutokana na fasili za wataalamu hawa tunaweza kusema utendi ni ushairi unaosimulia tukio fulani na wenye maudhui yanayomhusu shujaa. Hivyo utendi ni lazima uhusu mashujaa wa jamii.


 DHANA YA SHUJAA
Gichamba (2005) anaeleza kuwa shujaa (jagina) ni mtu ambaye humiliki uwezo zaidi kuliko uwezo wa watu wa kawaida na hutumia uwezo huu kiujasiri na huwa tayari kuyahatarisha maisha yake kwa manufaa ya watu wengine. Pia Nayo TUKI (2004), inasema kuwa, shujaa ni mtu mwenye moyo thabiti anayeweza kukabili mambo, hata kama ni hatari.


Kwa ujumla, shujaa ni kiumbe aliye na sifa za kiajabu ambaye hutumia nguvu za kimwili ama sihiri ili aweze kupamabana na maadui zake.
Mutiso (1999) anaainisha majagina (shujaa) katika makundi matatu. Anasema shujaa wa kwanza ni kiumbe wa kweli ambaye amekuzwa na kujikuza mwenyewe hata kuonekana kiumbe wa ajabu. Kiumbe huyu huwa ni mashuhuri na husifika kwa ujasiri, nguvu (hata kama amelemaa ulemavu huu ni onyo kuwa baadaye atakuwa na nguvu za ajabu).


Mabadiliko yote mazuri yatokeayo katika jamii, jamii husika huamini kuwa yameletwa na jagina wao, hata kama shujaa huyo hahusiki kamwe. Anafafanua zaidi kwa kueleza kuwa shujaa huyu hutokana na familia masikini lakini jamii yake huamini ya kwamba ametokana na familia tajiri ya kifalme. Maisha yake huwa ni ya dhiki na ni yaa taabu.

 Yumkini, watu humwabudu baada ya kifo chake.
Shujaa wa pili ni kiumbe wa kihurafa, ambaye ameumbwa na jamii yake. Kiumbe huyu huwa na sifa ambazo si za kawaida na ghalibu awe ni Mungu au yote mawili. Yumkini, iaminike ya kwamba shujaa huyu ndiye mzazi wa jamii husika.


Shujaa wa aina ya tatu ni mhusika mkuu katika utenzi, tamthiliya, riwaya, hadithi, ngano sinema au jambo. Aina hii ya shujaa wa tatu anaweza kuwa kati ya shujaa wa aina ya kwanza au shujaa wa aina ya pili. Pia Mulokozi (2017) anafafanua aina mbili za shujaa wa kitendi kama ifuatavyo;
Mosi shujaa wa utendi wa kijadi wa Kiafrika ambapo shujaa huyu anakuwa na mshikamano na watu pia anafungamana na nguvu za sihiri.


Na shujaa wa pili ni shujaa wa utendi wa Kiafrika-Kiislamu yaani shujaa wa kidini ambaye hutumia nguvu kutoka kwa Allah. Hivyo Makala haya yatachunguza sifa za shujaa wa kijadi wa Kiafrika.


Hivyo katika Makala haya mtafiti aliangazia mashujaa wa kijadi wa kiafrika kama ilivyoelezwa na Mulokozi (keshatajwa).


4.0 USULI WA MWANDISHI WA UTENZI WA FUMO LIYONGO
Kwa mujibu wa Mulokozi (1999) Muhammad Abubakar Kijumwa alikuwa ni mwenyeji wa Lamu nchini Kenya.

 Alikuwa mshairi mashuhuri ambaye mbali na kutunga mashairi na tendi, alikuwa mchongaji wa milango yenye nakishi. Habari za maisha yake hazijulikani vizuri. Alianza kujitokeza katika utunzi miaka ya 1980. Alipoanza kuwasaidia wazungu na watafiti wa Kiswahili waliotaka kufahamu habari za Waswahili. Alifariki mwanzoni mwa miaka ya 1940.


4.1 USULI WA UTENZI WA FUMO LIYONGO
Kwa mujibu wa Mulokozi (1999), utenzi wa Fumo Liyongo uliosimuliwa mwaka wa 1913 na bwana Muhammad Bin Abubakar Bin Omary Al-Bakiy, anayejulikana Zaidi mwa jina la Muhammad Kijuwa. Inaelezwa kuwa hadithi hii aliipata kutokana na mapokezi simulizi ya waswahili wa mwambao mwa Kenya. Shujaa wa utendi huu ni Fumo Liyongo ambapo utendi huu unahusu mgogoro kati ya Fumo Liyongo na kaka yake. Mfalme wa Pate, ambaye katika utendi huu hatajwi jina lake bali katika mapokezi mengine anaitwa Daudi Mringwari. Utendi huu unaanza wakati Liyongo akiwa kijana, aliyekwisha kubalehe, mwenye kusifiwa nchini kote kwa nguvu za ushujaa wake.


Kiini cha mgogoro huu ni kutokana na sifa za Liyongo za kuwa na nguvu nyingi na umaarufu. Jambo ambalo linamfanya mfalme wa Pate awe na hofu ya kupoteza kiti chake cha ufalme. Kutokana na kadhia hizo Liyongo anagundua kuwa mfalme anataka kumuua. Liyongo anaondoka Pate na kwenda nyikani. huko pia Liyongo anakupambana na changamoto mbalimbali kwani mfalme aliendelea kumfatilia na kumtumia baadhi ya watu ili waweze kumuua lakini hawafanikiwi kumuua.

 Mfalme anaamua kumtumia mtoto wa Liyongo na kumshawishi kumua baba yake ili aweze kumpatia fidia ya madaraka na kumuoza binti yake. Hivyo mtoto wa Liyongo anakubali kumua baba yake ili aweze kupokea fidia alizo ahidiwa na mfalme. Mtoto wa Liyongo anamuuliza baba yake juu ya siri ya kifo chake, Liyongo anahisi kuwa mwanaye atakuwa anatumiwa na mfalme lakini Liyongo anatoa siri hiyo kwa mwanaye. Baada ya mtoto wa Liyongo kupata siri juu ya kifo cha baba yake anaamua kumuua baba yake.


5.0 USULI WA MWANDISHI WA UTENZI WA NYAKIRU KIBI
Mtunzi wa Utenzi wa Nyakiru Kibi ni, Mugyabuso M. Mulokozi ni Profesa wa Fasihi katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alizaliwa tarehe 7 juni, 1950. M.M. Mulokozi ameandika na kuhariri vitabu zaidi ya 15 vya kitaaluma, vitabu 10 vya kisanaa (hadithi, tamthiliya na ushairi) na Makala ya kitaaluma zaidi ya 100. Miongoni mwa vitabu alivyoandika ni; Mukwava wa Wahehe (Tamthiliya), Ngome ya Mianzi (Riwaya), Ngoma ya Mianzi (Riwaya), Moto wa Mianzi (Riwaya), Mashairi ya Kisasa (pamoja na K. K. Kahigi) na Kunga za Ushairi wa Diwani Yetu (pamoja na K. K. Kahigi).


5.1 USULI WA UTENZI WA NYAKIRU KIBI
Utenzi wa Nyakiiru Kibi unasimulia historia ya utawala wa Kiziba ambapo mfalme wa kiziba alijulikana kama Mukama. Katika uongozi wa Mukama aliongoza kwa kutumia mabavu, alipoona mwanamke mzuri alimuua mumewe na mke kujinyakuria.


 Mukama alifanikiwa kupata mtoto wa kiume lakini kutokana na hofu juu ya utawala wake aliamua kumfanyia sihiri mtoto wake ili aweze kuota meno ya mbele. Baada ya meno ya mbele mtoto yule alitupwa katika kijiji kingine, kisha aliokolewa na bibi na kupewa jina la Kanyamaishwa. Kanyamaishwa anakuwa katika malezi ya bibi huyo. Kanyamaishwa anajihusisha na uwindaji ambapo anapambana na wanyama porini. Baada ya bibi kufariki Kanyamaishwa alioa na kuanza maisha mapya ya ndoa.


Utenzi huu unasimulia pia kuhusu shujaa Nyakiru Kibi ambaye alipewa jina la Kibi baada ya kua ndipo ushujaa wake ulipoanzia. Nyakiru Kibi alitoka katika familia ya kifalme ambapo baba yake aliwagawia ngoma wanawe ili waanzishe himaya zao. Nyakiru Kibi hakufanikiwa kugaiwa ngoma kwani hakuwepo alikuwa mstuni akiwinda hivyo Nyakiru Kibi aliamua kuiba Kanchwankizi na kutoroka nayo.
Nyakiru Kibi anakutana na Kanyamaishwa na kushirikiana katika masuala ya uwindaji. Shujaa Kanyamaishwa na Nyakiru Kibi pamoja na familia zao wanaanzisha safari ya kwenda Kiziba, nchi waliyokuwa wakiisifu kwa uzuri wa hali ya hewa na udongo. Baada ya kufika Kiziba wanapokelewa vizuri na wanaendelea kuishi vizuri na wananchi huku wakijishughulisha na shughuli yao ya uwindaji. Kanyamaishwa na Nyakiru Kibi wanashirikiana kumuua mfalme wa nchi hiyo na wanafanikiwa pasi na kujua kuwa mfalme yule ndiye baba mzazi wa Kanyamaishwa.


 Baada ya Kanyamaishwa kugundua kuwa kamuua baba yake anaumia sana hali ambayo inamfanya apate maradhi yanayosababisha kifo chake. Baada ya kifo cha Kanyamaishwa wananchi wanahuzunika hata Nyakiru Kibi anahuzunika kwa kupotelewa na rafiki yake. Hivyo Nyakiru Kibi anaendelea kuwa mtawala wa Kiziba.


6.0 SIFA ZA SHUJAA WA UTENDI WA KIJADI WA KIAFRIKA
Mulokozi (2017) anabainisha sifa za shujaa wa jadi ya Kiafrika, ambapo anaeleza kuwa shujaa wa kijadi ana sihiri, shujaa wa kijadi ana mshikamano na kundi, shujaa wa kijadi ana ushakii, shujaa wa kijadi anatoka katika tabaka lolote. Hivyo katika sehemu hii mtafiti amefafanua namna sifa za shujaa wa kitendi zinavyojidhirisha katika tendi teule.
6.01 Shujaa hutoka katika tabaka la juu au la kawaida.


Mulokozi (2017) anaeleza kuwa shujaa hutokea katika tabaka lolote lile, hivyo huweza kutokea katika tabaka la juu au la kawaida. Katika Utenzi wa Fumo Liyongo mwandishi hajaweka bayana kuwa shujaa Liyongo alikuwa akitokea katika tabaka gani. Hivyo baadhi ya wataalamu hudai kuwa Liyongo alitoka katika tabaka la juu na wengine hudai ya kuwa Fumo Liyongo hutoka katika tabaka la chini.

Mtafiti wa Makala haya anaeleza kuwa pengine shujaa Fumo Liyongo alitoka katika tabaka la juu kwa sababu ya binamu yake kuwa ni mfalme. Hivyo yumkini atakuwa alitoka katika tabaka la juu. Pia, katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi, mwandishi anaonesha shujaa Kanyamaishwa kuwa alitokea katika tabaka la juu kwani alizaliwa katika ukoo wa Kifalme, mwandishi anaeleza jinsi malkia alivojifungua mtoto huyo;
                                 75. Likapigwa la mgambo
                                       Likilia lina jambo
                                       Ikuluni kuna mambo
                                       Kajifungua malkia.
                                76. “Malikia mtukufu
                                    Kazaa mwana nadhifu
                                     Mwingine hafui dafu
                                      Kunawiri kazidia.
Vilevile katika utenzi wa Nyakiiru Kibi, shujaa Nyakiru Kibi alitoka katika tabaka bora kwani baba yake alikuwa ndiye mtawala wa Bunyoro. Pia katika Utenzi wa Vita vya Kagera, shujaa Nyerere alitoka katika tabaka la juu kwani alikuwa ni mtoto wa chifu, hivyo ni wazi kuwa alikuwa katika tabaka la juu. Lakini shujaa Idd Amin hakutoka katika tabaka la juu kwani mwandishi anaeleza kuwa Idd amini alilelewa na mama yake aliekuwa akihangaika huku na huku katika kutafuta pesa ili aweze kumhudumia mwanaye. Hivyo kutokana na maelezo haya ni dhahiri kuwa shujaa wa kijadi wa Kiafrika hutoka katika tabaka lolote lile.
6.02 Shujaa ana mshikamano na kundi au makundi ya watu anaowatetea.
Mulokozi (1997) anaeleza kuwa shujaa lazima awe na mshikamano na jamii inayomzunguka. Mathalani, shujaa Fumo Liyongo anawasaidia Wagalla kupata mbegu bora baada ya wagalla wale kutamani kupata mtoto mwenye sifa kama za Fumo Liyongo.                                    
                                          40. Wagalla wakabaini      
                                              Kumwambia Sultwani                                        
                                              “Twamtaka kwa thamani                                    
                                                Kijana kutuweleya.                                            

                                        41. “Twaitaka mbeu yake
                                                 Nasi kwetu tuipate
                                                 Kwa furaha tumuweke
                                                  Apate kutuzaliya
Pia, katika Utenzi wa Nyakiru Kibi, shujaa Kanyamaishwa na shujaa Nyakiru Kibi walikuwa na ushirikiano mzuri na jamii yao. Jamii iliwapenda kutokana na shughuli yao ya uwindaji pia ukarimu wao uliwavutia zaidi wananchi kwani walipotoka mawindoni waligawa nyama kwa raia. Kutokana na ukarimu waliouonesha kwa raia, wananchi walizidi kuwapenda na kuonesha mshikamano kati yao. Mwandishi anaeleza;
                                             674. Waendelea kuuwa
                                                     Wanyama wanaoliwa
                                                     Na nyama yao kugawa
                                                      Kwa wakulima raia.
                                             675. Wauwapo kwa upanga
                                                     Nyama mmoja mjinga
                                                     Hukata na kumchonga
                                                     Watu wakawagawia.
                                            676. Wakasema “Hawa watu
                                                   Ni kama wazazi wetu
                                                   Bahati ya nchi yetu
                                                    Kuwa wameijilia”.
Pia katika Utenzi wa Vita vya kagera, shujaa Idd Amin alikuwa na mshikamano na kundi la watu ambao aliambatana nao katika harakati zote za kivita. Hivyo suala la shujaa kuwa na mshikamano na kundi haliepukiki.
 6.03 Shujaa ana sihiri.
BAKITA (2017) inaeleza kuwa sihiri ni istilahi inayotumika kurejelea hali ya mtu kuwa na imani ya ushirikina na kutenda mambo ya uchawi. Mulokozi (1997) anaeleza kuwa nguvu za mwili au silaha pekee bila sihiri hazitoshi, maana mapambano ya shujaaa na hasimu yake si mapambano ya silaha tu, bali ni mapambano ya sihiri. Na mwenye sihiri ya uganga kuntu zaidi ndiye anayeshinda. Katika utenzi wa Fumo Liyongo, shujaa Fumo Liyongo ana nguvu ya uganga katika kitovu chake na hivyo hawezi kudhurika kwa njia yoyote ila kwa kudungwa sindano ya shaba kitovuni. Mwandishi anasema;
                                        143. Nasikiya wangu baba
                                               Liniuwalo ni haba
                                                Ni msumari wa shaba
                                               Kitovuni nikitiya
                                       144. Jamii silaha piya
                                               Haziniuwi swabiya
                                             Ila nimezokwambiya
                                           Ni njia ya kweli yote piya.
Lakini katika Utenzi wa Nyakiru Kibi, shujaa kanyamaishwa baada ya kuzaliwa sihiri ilitumika katika kumdhuru tofauti na ilivyokuwa kwa Fumo Liyongo mwandishi anaeleza;
                                                   140. Hii dawa ya kunoa
                                                         Meno yapate toboa
                                                          Mafizi na kutokeza
                                                         Kinywani akamtia
                                                  141. “Hii ya kulainisha
                                                           Mafizi kudhalilisha
                                                        Meno yapate pitisha,”
 Hivyo shujaa kanyamaishwa hakuwa na sihiri katika mapambano yake bali alitumia utashi na akili pevu pamoja na nguvu za kimwili katika kupambana na wanayama wakali. Shujaa Nyakiru Kibi hakuwa na sihiri yoyote ambayo ilimsaidia katika harakati za ushujaa wake, bali alitumia nguvu za mwili wake katika kupambana. Pia Bowra (1964) anaona kuwa sihiri ni maudhui na si ushujaa hivyo suala la sihiri kwa shujaa wa kijadi wa kitendi si muhimu. Hata hivyo mtafiti wa Makala haya anaeleza kuwa suala la sihiri kwa shujaa si la lazima kwani shujaa anaouwezo wa kutumia nguvu zake za mwili na akamshinda adui. Mathalani katika Utenzi wa Vita vya Kagera, Idd Amin hakuwa na sihiri yoyote lakini aliweza kupambana halikadhalika Nyerere hakuwa na sihiri yoyote lakini alifanikiwa kupambana.
6.04 Shujaa ana ushakii (ujasiri, nguvu au urijali).
Mulokozi (1999) anaelezea kuwa nguvu za shujaa ni nguvu za kimwili yaani ubabe na mabavu, nguvu za kiume na kidume yaani urijali. Mulokozi anaendelea kueleza kuwa shujaa ana ubabe wa kimwili, ni jasiri na haogopi kitiu. Mathalani shujaa Fumo Liyongo alikuwa ni jasiri asiyeogopa kitu mwandishi anaeleza;
                                7. kimo kawa mtukufu
                                    Mpana sana mrefu
                                   Majimboni yu maarufu
                                  Watu huya kwangaliya
                          13. Ni mwanaume swahihi
                                Kama simba una zihi
                                Usiku na asubuhi
                                 Kutembea ni mamoya
Pia sifa ya shujaa kuwa na ujasiri na ubabe linajidhihiriha pia katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi, kwani shujaa Kanyamaishwa pamoja na shujaa Nyakiru Kibi walikuwa na nguvu za kimwili pamoja na ujasiri wa kuweza kupambana na wanyama wa porini pasi na kuwa na uwoga wa aina yoyote. Mwandishi anaeleza;
                               467. Nyakiru akaanguka
                                        Mkuki alioshika
                                        Vizuri kampachika
                                         Adui penye kifua.
                                468. Na mbwa wakakupuka
                                        Bwabwa bwabwa wakabweka
                                        Chui akababaika
                                         Alia na kuugua!
Hivyo sifa ya shujaa wa kijadi ni kuwa jasiri na mbabe ili aweze kupamabana na mpinzani wake. Vilevile katika Utenzi wa Vita vya Kagera shujaa Idd Amin alikuwa ni jasiri na mbabe ndiyo maana aliweza kupamabana katika vita.
7.0 SIFA ZA SHUJAA WA KITENDI ZINAZOJITOKEZA TOFAUTI NA ZILIZO
                                  BAINISHWA NA MULOKOZI.
Mulokozi (2017) anabainisha sifa za shujaa wa kitendi, lakini miongoni mwa sifa bainifu za kishujaa si zote huonekana katika tendi aghalabu huonekena chache. Mtafiti wa Makala hii alifanikiwa kuchunguza sifa za shujaa katika tendi teule. Mulokozi (2017) anaeleza kuwa makundi mawili aliyobainisha ya sifa za shujaa yanaweza kuwa ni kianzio cha uchambuzi wa mtafiti. Kwa mantiki hiyo mtafiti anaweza tafiti zaidi juu ya sifa za shujaa. Hivyo mtafiti wa Makala haya ametafiti na kufanikiwa kuibua sifa nyingine za kishujaaa wa kitendi tofauti na zilizobainishwa na Mulokozi (2017) ambazo ni;


7.01 Kifo cha shujaa lazima kionekane pigo kwa jamii.
Shujaa anapopatwa na umauti jamii huumia na kuuzunika sana kwa kuondokewa na mtetezi wao. Katika Utenzi wa Fumo Liyongo mwandishi anaeleza kuwa baada ya shujaa Fumo Liyongo kufa jamii inaomboleza kwa kusema;
                          224. Make Liyongo hakika
                                    Matanga aliyaweka
                                     Watu wanasikitika
                             Kwa Liyongo kuifiya
                    225. “Liyongo silaha yetu
                              Kwa wut’e khasimu zetu
                               Alikua ngao yetu”
                              Wut’e wakinena haya
                 226. Mui walisikitika
                         Hakuna wa kutosheka
                         Kwa Liyongo kutoweka
                         Imeanguka paziya.
Pia katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi mwandishi anaeleza kuwa baada ya shujaa Kanyamaishwa kufa shujaa Nyakiru Kibi anapata pigo kubwa anahuzunika kwa kuondokewa na rafikiye. Mwandishi anasema;
                                 877. Nyakiru akamlilia
                                         Akalia, akalia
                                       Akamuombolezea
                                     Mwenzi aliyemfaa.
                         878. Myezi miwili Nyakiru
                                Katu hakuona nuru
                                Kijiji hakukizuru
                                Nyumbani alitulia.
Hivyo shujaa anapatwa na umauti, kifo chake huonekana kuwa ni pigo kubwa kwa jamii.
7.02 Shujaa ana majigambo
Simiyu (2010) anaeleza kuwa majigambo ni maigizo yanayotoa mwanya kwa wahusika kujisifu kwa sababu ya matendo fulani ya kishujaa au mafanikio katika nyanja fulani za maisha. Shujaa wa kitendi wa kijadi wa Kiafrika anahusishwa na majigambo ambapo hujigamba kuhusu matukio aliyokwisha kuyafanya ambayo ni ya kustaabisha. Mathalani katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi, mwandishi anaeleza namna shujaa Kanyamaishwa na shujaa Nyakiru Kibi wanavyojigamba baada ya mashujaa hawa wawili kukutana. Mwandishi anasema;
                                       383. “Ninalo jicho la nyayu
                                               Na nyayo za mbayuwayu
                                               Hali taka mke huyu
                                              Nyama humtafutia.”
                                 386. “Jina langu Nyakiiru
                                         Amiri wa watu huru
                                       Muepesi wa kudhuru
                                      Mgumu wa kudhuriwa.
                         387. kwa hekima nasikika
                                 Kwa ushujaa nawika
                                Bunyoro nilikotoka
                                Wote hunisujudia.
Naye Kanyamaishwa alijigamba baada ya Nyakiiru kujigamba mwandishi anasema;
                                               396. “Ni vema kuyasikia
                                                         Maneno ya ushujaa
                                                       Mimi pia nakwambia
                                                        Si mzembe kwa kuua.
                                           397. “Nimevizoea vita
                                                  Hupiga bila kusita
                                                 Kazi yangu ni kuteta
                                                Mateto ninayoyajua.
Aidha kwa upande wa shujaa Fumo Liyongo hakuwa na majigambo yoyote. Lakini katika Utenzi wa Vita vya Kagera, shujaa Idd Amin dadaa alijigamba kwa kujiita simba.
7.03 Shujaa lazima awe na mpinzani
 Njogu na Chimerah (1999) wanasema kuwa, hakuna shujaa (jagina) yeyote ulimwenguni ambaye hana adui. Kwa kawaida maadui huwa ni muhimu kwa sababu mtu hawezi kuwa shujaa bila kuwa na mpinzani ama adui. Katika utenzi wa Fumo Liyongo, adui mkubwa wa shujaa Fumo Liyongo alikuwa ni binamu yake Fumo Liyongo. Binamu yake alipanga njama za kumwangamiza Liyongo kwani alimwona kama tishio katika utawala wake. Alimtumia mwanaye Liyongo kumsaliti baba yake. Mwandishi anasema;
                                214. Usiketi mui wangu
                                      Wewe adui ya Mngu
                                       Tena vua nguo zangu
Aidha, katika Utenzi wa Nyakiru Kibi shujaa Kanyamaishwa na shujaa Nyakiru Kibi mpinzani wao ni mfalme wa nchi ya Kiziba. Uadui huu uliibuka baada ya mfalme huyo kuongoza nchi kwa mabavu, shujaa Kanyamaishwa na Nyakiru walishirikiana kumuua mfalme wa Kiziba.


8.0 HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
Katika kuhitimisha uchambuzi wa Makala hiii imebainika kuwa mashujaa wa jadi ya Kiafrika hushabihiana kwa baadhi ya sifa na hutofautiana kwa baadhi ya sifa. Hivyo ni vigumu kupata sifa ambazo zitasawiri moja kwa moja mashujaa wa tendi za Kiafrika. Mulokozi (2017) anaeleza kuwa si rahisi kwa mataifa mawili yasiyo kuwa na uhusiano wa karibu kuwa na sifa zinazolanda kwa hali zote. Mtafiti wa makala haya anaeleza kuwa kutokana na tofauti za kijiografia, tofauti za makuzi na tofauti za mila na desturi baadhi ya sifa za shujaa hushabihiana, hivyo sifa fulani ya shujaa wa kijadi wa Kiafrika inaweza patikana kwa mashujaa kadhaa na si kwa mashujaa wote. Mathalani sifa ya shujaa kuwa na sihiri kama ilivyoelezwa na Mulokozi (1997) kuwa ni sifa ya muhimu kwa shujaa jambo ambalo lina utata kwani si mashujaa wote wa tendi za kijadi wanasihiri. Hivyo sifa hizi zinaweza kushabihiana kwa baadhi ya mashujaa.
Mtafiti wa Makala hii anapendekeza kuwa watafiti wajao waweze kutafiti juu ya sifa za shujaa wa kidini.

                                             










                                                    MAREJEREO
BAKITA (2017) Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la Pili, Longhorn publishers limited: Nairobi
Gichamba, J. M (2005) Sifa za Mashujaa na Umuhimu wao kwa Jamii zao: Ulinganishi wa Fumo
                       Liyongo na Shaka Zulu. Chuo Kikuu cha Nairobi. Haijachapishwa.
Njogu, K na Chimera, R (1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi. J. K. F.
Mulokozi, M. M. (1996) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Dar es Salaam. TUKI
Mulokozi, M. M. (1997) Utenzi wa Nyakiiru Kibi: Morogoro. ECOL Publications
Mulokozi, M. M. (1999) Tenzi Tatu za Kale: Dar es Salaam. TUKI
Mulokozi, M. M. (2017) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Dar es Salaam. KAUTTU
Mutiso, K. (1985), Hurafa na Uyakinifu katika Hamziyyah: Tasnifu ya Uzamili. Chuo Kikuu cha
                     Nairobi. Haijachapishwa.
Wamitila, K. W. (2003), Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia: Nairobi-Kenya. Focus Publishers
                       Ltd.
Simiyu, W. (2010), Kitovu cha Fasihi Simulizi: Mwanza. Serengeti Bookshop
TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Nairobi. Oxford University Press.


Comments

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?