Serikali yatangaza ajira za walimu
Dodoma. Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo amesema Serikali inatarajia kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 4,549 ili kupunguza changamoto ya waalimu iliyopo nchini.
Waziri Jafo ameyasema hayo jijini hapa leo Alhamisi Februari 28, 2019 wakati akizindua Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania bara (Tapsha) na kusema katika kipindi cha mwaka huu na mwaka jana wanastaafu waalimu wengi wa Upe hivyo nafasi hizo zinatakiwa kuzibwa haraka iwezekanavyo.
“Nafahamu kuna upungufu wa walimu, hivyo ofisi yangu niliwaagiza wataalamu wafanye tathmini nikijua wazi tulikuwa na waalimu wengi wa Upe walioingia maalumu ambao kwa sasa walimu hao ndio wanatoka katika kazi.”
“Wengine walistaafu mwaka jana na mwaka huu tuna idadi kubwa ya walimu wa Upe wanaostaafu, hivyo nikamuomba mheshimiwa Rais (John) Magufuli na yeye akaridhia walimu zaidi ya 4,549 waajiriwe ili kuongeza nguvu katika sekta ya elimu,” amesema Jafo.
Amesema kati ya hao watakaoajiriwa idadi kubwa itakuwa kwa walimu wa shule za msingi.
kwa mujibu wa tangazo lililowekwa kwenye ukurasa wa mtandao wa Tamisemi waombaji wanatakiwa kutuma barua za maombi hadi machi 15, 2019
Comments
Post a Comment