Kuna matukio ndani ya dunia hii ni magumu kusahulika kwa vizazi na vizazi. Ni ngumu kwa waingereza kumsahau Diego Maradona na goli lake la mkono robo fainali kombe la dunia mwaka 1986. Yapo mengi sana ya kukumbukwa ambayo yanarithishwa  kwa vizazi na vizazi ili kumbukumbu isipotee.

Ijumaa ya tarehe 25 December 1914 katika maadhimisho ya siku kuu ya Christmas, miezi mitano tu baada ya mtutu wa vita vya kwanza vya dunia kuwaka, dunia ilishuhudia tukio la ajabu ambalo mpaka leo limebaki historia ya pekee katika uga wa soka , diplomasia, kijeshi na masuala ya haki za kibinaadamu.

Vikosi vya majeshi ya Uingereza toka Bataliani namba mbili ya London Rifle Brigade vilikutana na vikosi vya Ujerumani kwenye eneo lisiloshikiliwa na upande wowote kivita ( noman's land ) na kusheherekea siku kuu ya Christmas kwa kuimba nyimbo za Christmas na kucheza mpira pamoja. Mtandao wa CIA Book of facts unaielezea kirefu vita hii.

Tukio hili ambalo kwenye kumbukumbu kidunia linajulikana kama Christmas Truce, halikuwapendeza sana wakuu wa vikosi pande zote kutokana na majeshi hayo kuwa na uhasama mkubwa na kuonekana ni tukio la hatari sana.

Kuanzia milango ya saa kumi na moja alfajiri taarifa mbalimbali kutoka London na Berlin zilianza kutumwa kwa makamanda wao walioko mstari wa mbele kuvunja makubaliano hayo na mtutu wa vita kushika hatamu jambo ambalo halikufanikiwa, wanjeshi na maafisa pande zote waliendelea kushehekea siku kuu ya Noel kwa kucheza soka , kunywa pombe pamoja, kutibu majeruhi wa vita , kurekebisha mahandaki, kuzika marehemu na kufanya ibada.

Tarehe 7 December Papa Benedict XV alitoa wazo kwa wakuu wa majeshi Ulaya siku ya mkesha wa Christmas kuweka silaha zao chini duniani kote ili watu washerekee kwa amani siku kuu hiyo lakini alipingwa vikali. Tukio la vikosi vya Ujerumani na Uingereza kwa maamuzi ya askari na maafisa wadogo mstari wa mbele ( Forward Edge of Battle Area FEBA ), lilimpa faraja sana kiongozi huyo mkuu wa kanisa la Roma duniani wakati huo kuamini kwa sehemu Mungu alisikia maombi yake.

Kabla ya kukutana kwenye noman's land, milango ya saa 6:50 usiku siku ya mkesha wa Christmas , mstari wa mbele mapigo ya mizinga, bunduki na maroketi vilisimama ghafla na upande wa mahandaki ya Ujerumani waingereza walianza kusikia wanajeshi wakiimba nyimbo za Krismasi na kurusha mafataki hewani. Waingereza walijibu. Kitendo hicho kilichukua zaidi ya saa sita mpaka asubuhi ya tarehe 25 December kulipopambazuka wote wakaamua kutoka kwenye mahandani chini ya makubaliano ya kusitisha vita na kusherehekea siku kuu hiyo.

Tukio hili limebaki kama kumbukumbu ya ajabu duniani kwani baada ya sherehe hizo pande mbili ziliendelea na vita vikali.