SEHEMU YA TATU YA USASA USASAMBU

      
Kwa Mukhtasari
Kwa kiasi fulani suala la utandawazi limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili.
UTANGULIZI

SUALA la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya ovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike.

Inaendelea sehemu ya Tatu



Mama Mwanaharusi: Kwa nini?
Mama Mwanaharusi: (Anatania) Naona pazia limekushinda kushona.
Mama MwaNaharusi: Heee heeeee, umeona hili tu! Kabla sijakujibu lolote soma yale maneno kwenye fremu ya dirisha.
Mama Mwanawima: (Anasoma kwa sauti ya chini) Mgeni wangu karibu lakini uyaonayo na uyasikiayo yaache humu humu (Wote wanacheka.)
Mama Mwanaharusi: Aaaah ila mambo mengi shoga yangu, hapa kuna nguo nyingi za watu zinanisubiri.
Mama Mwanawima:  Mwanamke kazi na kujituma. Kuzaliwa masikini sio kosa, kosa ni kufa masikini.
Mama Wwanaharusi: Kweli ila hizi kazi zina changamoto, watu wengine wana visa utadhani ni waganga wa kienyeji
Mama Mwanawima: Changamoto gani tena? Kama hela si unapata?
Mama Mwanaharusi:   Hakuna kitu kinaniudhi kama mtu kuniletea nguo ambayo haijafuliwa, yaani unakuta nguo
imevunda, inanuka jasho kama mzoga lakini mtu hajali anataka umshonee.
Mama Mwanaharusi: Ubinadamu kazi shoga yangu, jamani nimekuja kumuulizia mwanangu hajarudi nyumbani mpaka saa hizi.  Sio kawaida yake! (Anaangalia saa yake.)
Mwanaharusi: Mimi leo sikuwa nao, hata nyumbani nimerudi mwenyewe ila skuli nilimuona yupo na Mwanakombo.
Mama Mwanaharusi: Mwanakombo huyu huyu au?
Mwanaharusi: Ndio huyu na Mwanahawa…
Mama Mwanawima: Mimi sitaki kabisa mazoea na ile familia.
Mama Mwanaharusi: Jambo la kushukuru ni kuwa tumeshajua aliko hivyo ni vyema ukamwangalie huko.
Mama Mwanawima: Haya jamani mimi ngoja niende huko kwa Mwanahawa.
(Anatoka mbio mbio kuelekea nyumbani. Kwa upande mwingine  Mwanawima naye anakazana kurudi kwa mama yake anamuona kwa mbali akiagana na wanamume, anajibanza uchochoroni na kumuacha atangulie nyumbani… mama Mwanawima hasira zimempanda, anasononeka na kujilaumu kumsomesha mwanaye.)
Mama Mwanawima: (Anaongea mwenyewe) Afadhali hela zangu ningenunua vitenge kuliko kuhangaika namsomesha halafu anafanya ujinga.
(Anamuacha mwanaye atangulie kisha naye anamfuata nyuma nyuma anafika na kumkuta Mwanawima akiwa amelala.)

Mama Mwanawima: Wewe Mwanawima! Mwanawima niambie ulikuwa wapi?
Mwanawima:Nilikuwa skuli mama, nimerudi muda mrefu tu sijakukuta.
Mama Mwanawima:Mwendawazimu mkubwa wewe, usinifanye sina akili!
Mwanawima: (Kimya anainamisha kichwa chini.)
Mama Mwanawima: Hii ni aibu mwanangu, wale vijana uliokuwa nao ni kina nani?
Mwanawima: (Kimya anaona aibu hata kuinua kichwa chake.)

Mama Mwanawima: Usidhani kuna kijana anayekupenda pale, wote hohe hahe tu.
Mwanawima: Nisamehe mama…
Mama Mwanawima: Baba yako si unamjua vizuri lakini! Lazima nimwambie akunyooshe, siwezi kuvumilia huu uchafu.
Mwanawima: Hapana mama, naomba usimwambie baba.
(Analia na kuomba msamaha.)
Mama Mwanawima: Katika siku ambazo umeniudhi leo umeniudhi sana, nakuonea huruma jinsi baba yako atakavyokupiga.
Mwanawima: Nisamehe mama sirudii tena.
Mama Mwanawima: (Hasira zinaongezeka, anavua kiatu chake na kumpiga nacho kwa hasira) Haya rudia tena sasa.
(Mwanakombo naye anafika nyumbani kwao akiwa kachoka hoi, anaingia ndani kwao anakuta wazazi wake wanaangalia runinga, anawasalimia.)

Mwanakombo:  Shikamoo (Baba na mama wanaitikia) Marahabaa.
Mwanahawa: Ulikuwa wapi mpaka muda huu… Unajiona
umekua eee!
Mwanakombo: Hapana leo tulichelewa kutoka, mwalimu alisema tubaki.
Mwanahawa: Wewe jifanye umeota mapembe tu…
Mwinyikheri: Aaaah, muache apumzike kwanza.
Mwanahawa: Mimi hapo ndio nakosana na wewe mume wangu, huyu mtoto akiharibikiwa aibu itakuwa kwetu sote.
Mwinyikheri: Mtoto haombewi mabaya, futa hiyo kauli yako…
Mwanahawa: Haya, mimi yangu macho…
(Mwanaharusi anarudi kutoka skuli.  Akiwa njiani, Mwanawima anamwachia simu aongee na Dulla kisha wanatawanyika kila mmoja kwao. Mwanaharusi pamoja na uvumilivu wa kutotumia simu alishawishiwa akaanza kuongea na Dulla kwa shingo upande. Anafika nyumbani mbio mbio, anaingia ndani haraka haraka na kutoka nje huku mifuko ya sketi yake ikiwa imevimba kama tumbo la chura, mama yake anamuangalia kwa makini…)
Mama Mwanaharusi: Mwanaharusi hebu njoo. (Anamuita na kuendelea na shughuli zake za kushona nguo).
Mwanaharusi: Abee mama…
Mama Mwanaharusi: Unataka uende wapi? Siku hizi sikuelewi mwanangu, vyombo havijaoshwa, ndani pachafu lakini hufikirii hata kidogo au nivioshe mimi?
Mwanaharusi: Hapana mama naenda mara moja hapo kwa Mwanawima, sichelewi kurudi
Mama Mwanaharusi: Hebu rudi hapa, unazurura ovyo kama mbwa koko. Njoo, njooo…
Mwanaharusi: Mamaaaa, narudi muda si mrefu.
Mama Mwanaharusi: Nini! Njoo hapa, hicho kilichovimba mfukoni ni nini?
Mwanaharusi: Huu mzigo wa Mwanawima ndio nampelekea.
Mama Mwanaharusi: Mimi nimekuuliza ni nini sijakuuliza wa nani?
Mwanaharusi: Ni simu mama, sio yangu ni ya Mwanawima.
Mama Mwanaharusi: Haya ilete, ilete haraka. Masuala ya simu nilishakukataza siku nyingi ila ukajiona wewe ndio una akili sana, sasa utaniambia ulikoipata.
Mwanaharusi: Sio yangu mama…
Mama Mwanaharusi: Wewe mtoto kwa nini unataka kunifedhehesha!
Kweli unamiliki simu ya gharama hivi kuliko hata ya wazazi wako! Unafanya kazi gani wewe?
(Mwanaharusi macho yamemtoka na hofu inamuingia. Anajua siri zake zimefichuka, anaweweseka na kuzidi kulia apewe simu… Matumizi ya simu yalikuwa yakupokezana. Leo kwa Mwanaharusi kesho kwa Mwanawima. Imekuwa kawaida yao kuperuzi mitandaoni na kuangalia picha chafu za ngono, wamejaza namba za simu za wanaume mbalimbali wanaowafanya muda wote wawe wanajishughulisha na simu tu, leo ndege mjanja amenaswa na tundu bovu… anaongozana na mama yake mpaka kwa mama Mwanawima huku akiwa amemshika mwanaye kwa mkono wa kulia na simu mkono wa kushoto… anafika na kuanza kufoka kwa hasira.

Mama Mwanaharusi: Muite huyo Mwanawima muite haraka aseme sababu za kukupa hii simu, mnajifunza mambo yaliyo nje ya uwezo wenu…
Mwanaharusi: (Analia) Nisamehe, nisamehe mama sirudii tenaa Mama.
(Kelele zinaongezeka maradufu, Mwanawima na mama yake wanatoka mbio kushuhudia nje kuna nini na kukuta ni mama Mwanaharusi amemfinyanga mwanaye, anampiga kweli kweli.

Mama Mwanawima: Jamani nini tena? Muache kwanza utamuumiza
(Anasogea na kuwaamua).
Mama Mwanaharusi: Mwanao anamfundisha mwanangu ufuska, naomba akome kuongozana na mwanangu kuanzia leo, sitaki, nasema sitaki. (Anatoa simu na kumuonesha mama Mwanawima picha na video chafu zote zilizopo kwenye simu.)
Mama Mwanawima: Mmh jamani! Haya ni makubwa, mbona sijawahi kumuona na simu jamani? Mwanawima simu umeitoa wapi?
Mwanawima: Mama mimi sijui hiyo simu ni ya nani! Ananisingizia tu, mwambieni aseme ukweli alikoitoa hiyo simu.
Mama Mwanawima: Kimya wewe! Msitufanye sisi hatuna akili. Kila mtu anasema sio yake, kwa hiyo haina mwenyewe sio?
Mama Mwanaharusi: Hao lao moja… Hii n aibu gani! (Anazidi kumpiga mwanawe)
Mama Mwanawima: (Anamfuata na kumsogeza pembeni) Shoga yangu subiri kwanza, kupiga tu hakutatui tatizo. Hebu tuyazungumze wenyewe kabla baba zao hawajarudi
maana tusizidi kupalia moto.
Mama Mwanaharusi: Hapa tutazungumza nini! Kama maji ndio hivyo yameshamwagika.
.Mama Mwanawima: Hapana tulia kwanza (Anamsogeza tena pembeni ili watoto wao wasisikie) Hawa watoto wa siku hizi sio kama wa zama zetu, mambo yamebadilika sana, tena sana.
Mama Mwanawima: Wanatia kichefuchefu, maisha magumu bado wanaongeza matatizo!
Mama Mwanawima: Kila kona ukipita unaona watoto wa kike wanayoyafanya.Wanavaa nguo za ovyo, wanamiliki simu na vitu vya thamani kuliko hata wazazi wao.
Mama Mwanaharusi: Yaani wanaanza uhuni wakiwa bado wadogo kabisa. Siku hizi maradhi ni mengi, wataangamia.
Mama Mwanawima: Mimi nakumbuka enzi zetu mwanamume akikutaka atafanya kazi sana kukupata, ila watoto wa siku hizi mwanamume akishapata namba yake ya simu tu, ujue biashara imekwisha.
Mama Mwanahharusi: Wanaume nao wamegundua udhaifu wao. Kurahisisha mambo yao wanawadanganya kuhusu usasa. Huyu mwanangu baba yake akisikia mambo haya atamuua.
Mama Mwanawima: Wala usimwambie baba yake, mtafutie muda mzuri useme naye. Naamini ataelewa na atanyooka tu. Huyu wa kwangu niachie nikapambane naye.
Mama Mwanaharusi: Ni kweli jirani… Kweli kila zama na kitabu chake! Mimi nakumbuka hatukuwa na hii michezo. Tulijiheshimu  tukaheshimika.
Mama Mwanawima: Ndio utandawazi wanaoutaka huo. Kila kona wanahubiri utandawazi. Eti usasa!
Mama Mwanaharusi: Watoto wetu nao wamezidi kupenda vitu vya
thamani,wamesahau kuwa mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba… (Anaaga kisha wote wanatawanyika… Giza linaingia, nyumbani kwa akina Mwanaharusi, Mwanaharusi anaonekana akiwa anamsaidia mama yake kuingiza cherehani na mizigo mingine huku kila mmoja akiwa kimya. Wanamaliza kuingiza vitu vyote ndani, mama Mwanaharusi anaamua kuvunja ukimya.)
Mama Mwanaharusi: Mwanaharusi hebu njoo kwanza tuongee kabla baba yako hajarudi.
Mwanaharusi: Sawa mama, (Hofu imetanda.)
Mama Mwanaharusi: Mwanaharusi mwanangu, wewe sio mtoto tena,
mdada mkubwa kama wewe kuchapwa viboko huwa haipendezi.
Mwanaharuusi: Ni kweli mama, nisamehe nimekosa, sirudii tena.
Mama Mwanaharuusi:Mwanangu, siku zote kumbuka mtoto hawezi kuwazidi wazazi wake. Usasa umewafanya kudhani kuwa mna maarifa kuwazidi watu wazima.  Uliona wapi sikio likazidi kichwa?
Mwanaharusi:(Kimya.)
Mama Mwanaharuusi: Kosa ulilolifanya baba yako akilisikia utachungulia kaburi, naomba usirudie tena.
Mwanaharusi: Sawa mama, nimekuelewa nisamehe (Anajibu kwa hofu.)
Mama Mwanaharusi: Mwaka jana ulikuwa na matokeo mazuri tu lakini angalia mwaka huu ulivyoporomoka, unaona inapendeza eeeeeee!
Mwanaharusi: Hapana mama.
Mama Mwanaharuusi: Soma, soma mwanangu! Achana na uchafu huo.

Popular posts from this blog

HIZI HAPA SMS TAMU ZA KUMTAKIA USIKU MWEMA MPENZI WAKO

SMS na MESEJI 900+ za mapenzi

MIAKA 22 SASA TANGU KUZAMA KWA MELI KUBWA YA MV BUKOBA, TANZANI TUMEJIFUNZA NINI?