JUMLA ya wanufaika 122,000 wanatarajia kupata fedha zitakazotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambayo imefungua dirisha la maombi kwa njia ya mtandao.


Kati ya wanafunzi hao, wapya ni 40,000 na wanaoendelea na masomo vyuoni ni zaidi ya wanufaika 80,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Abdul-Razaq Badru, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi kuanza kupokea maombi ya mikopo jana.

Dk. Badru alisema katika wanafunzi wapya, wanawake ni 14,000 sawa na asilimia 35 na wanaume ni 26,000 sawa na asilimia 65.

Alisema kwa mwaka huu idadi ya wanufaika wa mikopo imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana ambako walikuwa 33,000.

Alisema katika bajeti ya fedha za mikopo kwa mwaka 2018/19 jumla ya Sh. bilioni 427 zimetengwa ili kufanikisha suala hilo.

Pia alisema mwaka huu wametanua wigo wa utoaji mikopo ambapo baadhi ya wanafunzi wanaosoma kozi za diploma watanufaika nayo.

"Kuna fani chache zinauhitaji mkubwa ambazo ni ualimu wa masomo ya sayansi na hesabati na sayansi ya afya ya binadamu ambao mwaka huu watapata mikopo," alisema.

Pia alisema watatoa kipaumbele kwa waombaji mikopo watakaodahiliwa katika kozi zinazohitajika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi wa aina zote, kozi ya sayansi ya kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi na nishati.

Dk. Badru alisema wahitaji ambao ni yatima wenye nakala za vyeti vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhibiti (Rita), watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma.

"Wengine watakaopewa kipaumbele ni wenye ulemavu uliothibitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya. Waombaji mikopo ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya stashahada au sekondari na wana barua za uthibitisho kutoka taasisi zilizowafadhili," alisema.

Aidha, Dk. Badru aliwaeleza wanufaika kuwa mikopo siyo zawadi kwa sababu watakapotakiwa kuirejesha wanapaswa kutekeleza bila shuruti.

Kadhalika, alisisitiza kuwa wazazi wenye uwezo wa kuwasomesha watoto wao wafanye hivyo, ili mikopo iwanufaishe wasioweza kujilipia.

MIFUMO RAFIKI
Dk. Badru alisema bodi hiyo kwa kushirikiana na kitengo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC) wanaendelea na maboresho makubwa, ili kuifanya mifumo ya utoaji na urejeshaji mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wateja.

Alisema kwa mara ya kwanza Bodi imetoa mwongozo wake wa uombaji mikopo kwa lugha ya Kiswahili pamoja na kitabu chenye maswali na majibu 21 kuhusu sifa na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo.

"Kitabu na mwongozo vinapatikana katika tovuti yetu ya bodi na vitasambazwa kwa wadau kuanzia wiki ijayo ambapo maofisa wa bodi watatembelea shule na waombaji nchini kote," alisema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso), George Mnali, alisema wapo tayari kufanya maandamano ya kuhakikisha wanufaika wa mikopo wanairejesha, ili iwanufaishe wengine na sio kuandamana kwa mambo mengine.Pia aliomba wanafunzi waliokosa mikopo mwaka jana waangaliwe mwaka huu.

Kaimu Mkuu wa Shirika la Posta, Hassan Mwangonde alisema vituo 180 vilivyopo nchini vitatoa huduma kwa wanafunzi wanaoomba mikopo hiyo na watapata majibu kwa muda mfupi.

Meneja Usajili kutoka Rita, Patricia Mkulya ambaye alimwakilisha Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, alisema wanatarajia kuhakiki vyeti vya wanafunzi wapatao 60,000 kwa mwaka wa masomo wa 2018/19 na baada ya maombi kupokelewa watapewa taarifa kupitia akaunti zao.

Alisema ada ya uhakiki wa kila cheti ni Sh. 3,000 ambayo inatakiwa ilipwe benki za CRDB au NMB.