WAKATI serikali ikitangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi 123,285 wa elimu ya juu mwaka ujao wa masomo, Bunge limesema kigezo namba moja cha kuzingatiwa wakati wa utoaji wa mikopo hiyo kinapaswa kuwa ufaulu. 

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akiwasilisha bungeni mjini hapa jana makadirio ya wizara yake kwa mwaka 2018/19, alisema wanatarajia kutoa mikopo ya jumla ya Sh. bilioni 427 (sawa na fungu la mwaka huu) kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 40,544 na wanafunzi wanaoendelea na masomo 82,741. 

Prof. Ndalichako alisema mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu itatolewa kwa wenye vigezo vya kupata mikopo na ruzuku hizo. 

Hata hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo, Hussein Bashe, akiwasilisha bungeni jana maoni ya kamati hiyo kuhusu bajeti ya wizara hiyo, alisema kamati yao inaona kigezo cha ufaulu kinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika utoaji wa mikopo hiyo. 

“Kamati inashauri serikali kuanzia sasa ukiacha vigezo vingine, kigezo cha ufaulu kipewe kipaumbele cha kwanza kwa maana mtu aliyefaulu vizuri (best student) ndiye apewe kipaumbele cha kwanza kabla ya kuangalia vigezo vingine,” alisema. 

Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema kamati yao inapongeza jitihada zinazofanywana Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. 

Hata hivyo, alisema kamati inafahamu changamoto zilizopo katika utoaji mikopo ikiwamo baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo kwa sababu mbalimbali. 

Alisema kamati pia inashauri serikali kuipa HESLB fungu lake (separate vote) na ijulikane ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na si ya miradi ya maendeleo kama ilivyo sasa inayofanya bajeti ya miradi ya maendeleo ya wizara ionekane kubwa ilhali asilimia 48 ni fedha za bodi hiyo. 

Awali, akizungumzia kuhusu shughuli za HESLB mwaka ujao wa fedha, Prof. Ndalichako alisema serikali itatekeleza mpango wa kuunganisha na kuifanya mifumo ya upangaji, ulipaji na urejeshaji mikopo kujiendesha. 

"Serikali itaendelea na utekelezaji wa mkakati wa ukusanyaji wa mikopo iliyoiva na kukusanya Sh. bilioni 157.7 kwa mwaka,” alisema. 

"Pia itaendelea kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kurejesha mikopo kutoka kwa wanufaika pamoja na kuujulisha umma kuhusiana na mwongozo wa utoaji mikopo kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, sifa za mwombaji na tarehe ya kupokea maombi ya mikopo.” 

TOZO SHULE BINAFSIBashe pia alisema kamati yao inaishauri serikali kuangalia upya kodi na tozo kwa shule binafsi ikiwa ni pamoja na kuweka uwiano wa kuchangia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kati ya shule za umma na shule binafsi kuwa ni asilimia 0.5 ya pato la mfanyakazi. 

“Pia kuondoa urasimu katika upatikanaji wa misamaha ya kodi na tozo, ili kuwezesha sekta binafsi kupata msukumo zaidi wa kuwekeza na hivyo kuendelea kuzalisha wataalamu wengi na wazuri zaidi,” alisema Bashe. 

Aliongeza kuwa kamati yao imebaini watoto wa kike wanaosoma katika vyuo vya vyuo vya sayansi nchini ni wachache ikilinganishwa na watoto wa kiume. 

Alisema katika ziara yao ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwenye Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, ulibaini mwaka huu wa masomo wanafunzi wa kike wanaosoma stashahada chuoni hapo ni 344 kati ya wanafunzi 1,759 na wanaochukua shahada ya kwanza ni 365 kati ya 2,459, hivyo jumla ya wanafunzi wa kike chuoni hapo ni 709, sawa na asilimia 17. 

“Kamati inaona ipo haja kama nchi kuweka mkakati utakaotilia mkazo na kuwezesha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi katika ngazi ya chini,” alisema. 

WENYE ULEMAVU: Bashe pia alisema kamati yao inaishauri serikali kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wenye ulemavu, ili kuacha kuwaficha kutokana na imani potofu na ihakikishe miundombinu ya shule inakuwa rafiki kwa watoto hao kama vile madarasa, vyoo na njia za kupita.

#NIPASHE