WATANZANIA wengi hawajui nini kilisaba-bisha mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda yaliyosababisha mamia ya watu kuuawa mwaka 1994. Naamini kama wakisoma makala haya watajifunza kitu na kuona umuhimu wa mshikamano na amani tulionayo na faida yake. Endelea:


Kuna baadhi ya wasomaji hawajui nini maana ya mauaji ya kimbari. Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948, ibara ya 2, unafafanua kuwa mauaji ya kimbari ni: “Tendo lolote kati ya yale yafuatayo linalofanyika kwa nia ya kuharibu kikamilifu au katika sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, kirangi au cha kidini, kama vile mauaji ya watu wa kikundi hicho; kusababisha athari, kubwa upande wa mwili au wa akili kwa watu wa kikundi hicho…”

Wiki iliyopita tulisema Jeshi la Uganda mwaka huo wa 1994 yalipotokea muaji hayo ya kutisha ya kimbari Rwanda lilikuwa eneo la Mto Kagera ili kuhakikisha kuwa taharuki iliyozuka baada ya maelfu ya miili hii kuonekana haigeuki na kuvuruga amani katika eneo hili.
Lakini pia jeshi lilikuwa hapa ili kubaini miili hii ilikuwa inatoka wapi na kufunika Mto Kagera?

Kadiri ambavyo Jeshi la Uganda lilivyokuwa linafuatilia kwa kurudi nyuma kufuata Mto Kagera ndivyo ambavyo walizidi kubaini kwamba maiti hizo zinaletwa na maji kutoka tawi la Mto Kagera lililopita Kusini mwa Rwanda.

Na kadiri ambavyo walizidi kufuata chanzo cha maiti hizo zinakotoka ndivyo ambavyo walikuwa wanaikaribia Rwanda na maji ya mto rangi yake kuwa nyekundu zaidi kutokana na damu za binadamu.
Wanajeshi wa Uganda ambao walishiriki kwenye ukaguzi huu wa mto huu walikiri kwamba licha ya baadhi yao kupigana mstari wa mbele kwenye vita mbalimbali lakini hakuna yeyote kati yao ambaye aliwahi kushuhudia ukatili mkubwa wa kiasi kile.

Siku hizo Jeshi la Uganda lilifanya kazi ya ziada ya kuokoa mamia ya maiti zilizoonekana kuletwa na maji ya Mto Kagera kutoka nchini Rwanda.
Ajabu ni kwamba miili yote hii ilikuwa ina mfanano fulani. Maiti zote zilikuwa za watu warefu, wembamba, wenye nyuso ndefu na pua za kuchongoka. Haikuhitaji kufikiria sana kufahamu kuwa maiti hizi zilikuwa za watu wa kabila la Watusi (Tutsi).

Miezi kadhaa baadaye ndipo ambapo Jeshi la Uganda na ulimwengu wote walikuja kuelewa kwa nini maiti zilikuwa zinatupwa Mto Kagera. Ni ujumbe gani ambao ulikuwa unajaribu kutumwa.
Kulikuwa na tetesi kwamba Watusi nchini Rwanda walikuwa wanapenda kujisifu kuwa mababu zao wana asili ya nchi ya Ethiopia. Kitendo hiki cha wenzao kuwaua na kuwatupa mtoni, inadaiwa walikuwa wanawaambia kwamba “wanawasafirisha warudi kwao Ethiopia ambako wamekuwa wakijisifu kuwa ndio asili yao.”

Mauaji hayo ya kimbari yanatajwa kuwa yalikuwa ya kikatili sana na hakika yawe fundisho kwa nchi zinazoendekeza ukabila, udini na uhasama wa vyama vya siasa.
Mauaji hayo yalikuwa ni ya kutisha kwani maiti za binadamu zilikuwa zimetapakaa mitaani nchini Rwanda, nyingine zikiliwa na nzi na mbwa.

Ndani ya makumbusho katika nchi hiyo ya Rwanda inaelezwa kuwa asilimia 75 ya watoto nchini kipindi hiko walipatwa na trauma (ugonjwa wa kisaikolojia) na kwa vijana wadogo kushiriki mauaji au kushuhudia mauaji ya kikatili kama hayo wataalam wanasema hilo ni tatizo watakalobaki nalo hao hadi mwisho wa maisha yao.

Waliofika Rwanda wanasema ukifika katika jumba la makumbusho unapokelewa vizuri unaanzia kwenye chumba ambacho kina ‘flat screen’ kubwa, hapo utajifunza historia ya mauaji kupitia runinga.
Ukimaliza kwenye TV unaingia ndani ya makumbusho, utaona kumehifadhiwa vitu vingi, zikiwemo silaha kama mapanga, shoka, mikuki, bunduki nk zilizotumika wakati wa mauaji hayo ya kutisha. .
Ukutani kuna picha mbalimbali za watawala wa kipindi hiko, picha za mauaji, picha za mamia ya maiti vyote vikiwa na maelezo ya kina.

Kuna picha za manusura wa mauaji wakielezea walichoshuhudia. Kifupi kuna taarifa nyingi sana muhimu zikieleza kwa kina na kwa picha. Inahitaji moyo mgumu kutazama na kusoma, inaleta simanzi hata wao Warwanda inawaumiza na kuwatonesha vidonda lakini historia haikwepeki. Huwezi kuikataa historia. Wenzetu wamehifadhi haya kama somo kwa vizazi vijavyo.
Itaendelea wiki ijayo!