MWANAMALUNDI
Mtu maarufu katika kabila la wasukuma

KUZALIWA.
Mwanamalundi alikuwa msukuma. Alizaliwa katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mnamo mwaka 1892. Wazazi wake hawakuwahi kuzaa. Baba yake alikuwa Bugomola na mama yake aliitwa Ngolo.
Baba yake alipoona hapati mtoto aliondoka kwenda kwa mganga kuaguliwa. Alipofika aliambiwa;
"Mtoto utapata lakini atakapoanza kutembea wewe sharti utaiaga Dunia. Mtoto huyo atakuwa wa kiume na atakuwa na fahari kubwa sana."
Bugomola kusikia atapata mwana, tena wa kiume ambaye atapata heshima na kusifiwa nchini pote, furaha aliyokuwa nayo ilikuwa haielezeki.
Alipofika nyumbani alimueleza mkewe kinagaubaga alivyoambiwa na mganga huku akichekacheka kama aliyepatwa na kichaa. Siku hiyo alikuwa hatulii. Mara akae hapa mara akae pale.
Wakati mwingine alikuwa akitembea huku na huko pale kijijini. Watu walimuona walishangaa kumuona vile, maana siku zote alikuwa ni mpole na mtulivu. Ingawa alikuwa akikumbuka maneno ya mganga kuwa mtoto akianza kutembea sharti yeye atakufa. Lakini kwake aliona ilikuwa sawa tu. Maana tangu utoto wake hajapata mtoto na amezeeka kabisa. Kwake siku aliiona Juma, Juma aliina Mwezi na Mwezi aliona Mwaka. Hali kadhalika Mwaka aliuona Miaka.
Lakini hata hivyo muda ulipotimia Ngolo mke wake alipata mimba na baada ya miezi kadhaa akajifungua. Mtoto huyo walimpatia jina la Igulu maana yake 'Mbingu'. Igulu alipokuwa mtoto alikuwa mpole sana na mwenye adabu. Igulu alipoanza kutembea baba yake aliaga Dunia.
Igulu alikuwa mwoga sana kwa watu. Ilikuwa mtu akipiga hodi yeye hujificha chumbani au huzunguka nje ya nyumba hadi mtu huyo aondoke ndipo arudi. Alipokuwa na kufikia makamo ndipo alipoanza kucheza ngoma. Hivyo alipofikia umri wa miaka ishirini aliondoka nyumbani pamoja na vijana wenzake wawili wa pale kijijini kwenda kwa bibi kizee aliyekuwa maarufu sana ili kupata dawa ya 'Samba'. Samba ni dawa ya kisukuma yenye kumfanya mtu apendwe na kuvutia watu. Walipofika waliambiwa wasubiri kwa siku chache.
Itaendelea...
Kesho
Jumamosi