Hadithi; MWANAMALUNDI
Sehemu Ya Pili
Msimuliaji; A. H. Shaban
Simu; +255 742 016 407
ILIPOISHIA...
Alipokuwa na kufikia makamo ndipo alipoanza kucheza ngoma. Hivyo alipofikia umri wa miaka ishirini aliondoka nyumbani pamoja na vijana wenzake wawili wa pale kijijini kwenda kwa bibi kizee aliyekuwa maarufu sana ili kupata dawa ya 'Samba'. Samba ni dawa ya kisukuma yenye kumfanya mtu apendwe na kuvutia watu. Walipofika waliambiwa wasubiri kwa siku chache.
ENDELEA...
°MIKIKIMIKIKI.
Baada ya siku tatu bibi kizee aliwachukua na kuwapeleka mwituni. Walipofika walianza kutafuta na kuwayawaya huku na huko. Kisha walifika kwenye mti mkubwa na mrefu.
Kizee aliwaambia wamngoje kidogo akaokote kuni maana dawa ameikosa kwa hiyo watakuja kuitafuta siku nyingine. Igulu na wenzake waliachwa chini ya mti ule wakiwa hawana la kufanya.
Ghafla kifaru alitokea akiwajia mbio na kila mmoja alikimbia kuokoa maisha yake. Igulu akawa katika mkikimkiki wa mbio kutaka kuyaokoa maisha yake, pia kwa bahati mbaya au nzuri wenzake wote wakamtelekeza nae akapata mti akaushika na kuukwea. Kifaru alimfuata mpaka pale mtini na kumngojea pale kwa chini. Alimsubiri mpaka akachoka na kuanza kuuparua ule mti kwa pembe zake kali. Kisha akakojoa na kwenda zake.
Kumbe yule hakuwa kifaru hasa bali alikuwa ni yule bibi kizee aliyejigeuza tu. Alitaka kuwajaribu ili ajue na hasa mwenye roho nzito atakaye rithi dawa zake.
Baada ya dakika kadhaa bibi kizee alirudi akiwa amejikusanyia kuni huku akizungumza peke yake,
"Baja hali Abahnu a balaha?". Akiwa na maana "Wamekwenda wapi hawa watu hawa waliokuwa hapa. Igulu alipomtambua alijibu,
"Bibi niko huku. Njoo haraka twende kuna kifaru mkali sana humu, ndio kwanza ameondoka. Haya magamba yamepapatuka wakati akiuparuza huu mti kwa hasira wenzangu wote wamewahi kukimbia.".
Bibi kizee baada ya kuona hivyo aliyaokota yale magamba akisema,
"Twende mwanangu hata haya yanatosha kwa dawa yako."
Alipomaliza kuyaokota waliongozana hadi nyambani kwa bibi kizee. Walipofika nyumbani, Bibi kizee alianza kumweleza Igulu kuwa yule kifaru alikuwa ni yeye na kumweleza kusudi la kunigeuza katika hali ile. Kisha alimpa ile dawa pamoja na masharti. Baadhi ya masharti hayo yalikuwa;
Ni marufuku kumparuza mtu na akifanya hivyo basi mtu huyo atakufa. Ilikuwa marufuku kumuelekezea kidole mtu au kitu na kama akifanya hivyo basi mtu huyo au kitu hicho kitakauka.
Igulu alipoipata dawa ile alimshukuru sana kizee yule, kisha akaaga na kuondoka. Alipofika nyumbani mama yake alimkaribisha kwa heshima huku akipiga vigelegele kwa shangwe.
Itaendelea... Kesho jumapili