KILA KIFO NA SIKU YAKE
Kila binadamu atakufa, lakini kila kifo kina siku yake. Nyaisa Simango, katika makala haya  ana tudhihirishia hivyo. Vinginevyo ni vipi mtu anaweza kuelezea alivyo nusurika wakati mamia ya wenzake walio kuwa katika meli moja walishindwa kujiokoa. Ilikuwa sio siku yake.
Ziwa victoria limekuwepo kwa karne na karne, watu wanaoishi kuzunguka ziwa hilo wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali. Kuvumbuliwa kwa Ngalawa, Jahazi, Boti, na meli  kumewezesha kazi za usafirishaji kuwa rahisi.
Bila shaka Simango alipo itwa na mkuu wake wakazi na kuarifiwa kuwa itabidi aende Bukoba  kumpeleka mfungwa kusikiliza rufaa ya kesi yake alifurahi kwani angeweza kuona mandhari nzuri njiani.  Ijapokuwa yeye anatoka katika nmkoa unao pakana na ziwa  bado angefurahia kula samaki.  Nakwavile hakuwahi kufika bukoba, safari ingempa fursa nzuri ya kutalii mjini huko, na pia baada ya kumfikisha mfungwa huko alikotumwa na yeye angepata fursa nzuri ya kwenda kijijini kwake kuwatembelea jamaa.  Inawezekana hayo yote yalimjia  katika fikra zake
Kwahiyo safari yakwenda mwanza haikuwa na mashaka yeyote.
Ugumu wa safari ya kwenda Bukoba ulianza pale alipofika forodhani Mwanza, kwani waliokuwa wanaingoja MV BUKOBA walikuwa wengi kupindukia. Tofauti na safari ya barabara  ambapo ikitokea ajali, na mtu kama hakuumia sana , anaweza kujizoa zoa na  kwenda zake, ajali ya baharini inabidi mtu ajue kuogelea. Nyaisa alikuwa hajui kuogelea
MV BUKOBAilifika bukoba, lakini katika safari ya kurudi haikufika  Mwanza, bali ilizama  na kuteketeza maisha ya mamia ya watu.  Ilikuwa ni moja ya ajali kubwa  kutokea nchini na hata Afrika ya masharikui.
Nyaisa amejaribu kutuelezea hapa ninini kilitokea wakati meli inazama polepole. Lakini sidhani kwamba hata yeye ameweza kuipata taswira kamili ya nini kilikuwa kinatokea katika meli nzima, kwani  yeye binafsi  alikuwa katika hekaheka ya kuokoa maisha yake.
Taifa lilipigwa na butwaa, vilio vilisikika kutokea pande zote za nchi. Na cha kusikitisha zaidi nikule kutokuwepo kwa  uwezo wa haraka wa kuwaokoa  watu walio kuwemo kwenye meli ile. Hata nchi jirani hazikuwa na nyenzo za uokoaji. Afrika ya kusini ilisaidia,  lakini masafa yanayo tenganisha nchi hizi mbili pamoja na kutoweza kuleta vifaa  kwa haraka  ili kuisimamisha mele hii isizame kabisa haikuwezekana, maisha ya wale waliokuwemo ndani ya meli wakaangamia. Tukabaki tukishuhudia maisha ya wananchi wenzetu yakiyoyoma . Sura kamili ya umasikini na udhaifu wan chi ilionekana.
Maafa haya yalikuwa ni pigo kubwa kwa serikali ya awamu ya tatu iliyo ongozwa na raisi Benjamin Mkapa, kwani ilikuwa bado haijatimia hata mwaka mmoja tangu iundwe kwahiyo bado ilikuwa katika fungate. Taifa lili ukabili msiba huu kwa ujasiri mkubwa. Maelfu ya wananchi wa kawaida, viongozi wa kidini,  kijamii na kisiasa , wakuu wan chi, na baba wa taifa wote walimiminika mwanza kuomboleza. Na mazishi ya wale walioweza kupatikana yalifanyika Igoma nje kidogo ya jiji la Mwanza. Kuna wengi ambao Mv bukba ilibidi iwe kaburi lao
Kuna mengi ambayo taifa ilibidi lijifunze kutokana  na tukio hilo kubwa, lakini je tumejifunza chochote?
Sehemu zilizo unda MV BUKOBA, zilitengenezwa Ubelgiji na kuja kuunganishwa mjini mwanza, mnamo mwaka 1978, na meli hiyo kuanza kazi mnamo mwaka 1979. Kiwango cha abiria  ambacho kilitarajiwa kuchuliwa na meli hiyo ni abiria 400 tu na wafanya kazi 36 na tani 200 za mizigo. Hati ya usalama ya kusafiri baharini ( serficate of seaworthiness)  ambayo meli hiyo ilikuwa nayo iliruhusu abiria 400, wafanya kazi 22, na tani 85 za mizigo.
Lakini meli hii ilikuwa na abiria mara mbili zaidi ya hao. Mbali na shehena ya mizigo iliyo kuwemo, hatujui kama meli hiyo ilikuwa ikikaguliwa kila wakati, na kufanyiwa matengenezo kikla inapo bidi. Simango anatueleza wazi kuwa wakati inaondoka Mwanza kwenda Bukoba ilionesha wazi uchakavu wake na kwamba ilikuwa katika hali mbaya. Sasa ilikuwaje meli hiyo ikapata hati ya kusafiria (sertificate of sea worthiness)  linakuja pia suala la uadilifu na uamunifu wa nahodha wa meli hiyo. Ilikuwaje akachukua dhamana  ya kuendesha meli iliyojaa abiria na shehena kubwa ya mizigo kwa kiasi hicho wakati meli ilionesha wazi kuwa sii madhubuti?
Serikali chini ya ibara ya 266 ya sharia ya meli za kibiashara ya mwaka 1967 (merchant shipping Act , 1967) iliunda tume ya watu 13  ikiongozwa na jaji wa mahakama ya rufaa, mh, Robert Kisanga,  kuchunguza sababu ya ajali ya meli ya Mv Bukoba. Tume hiyo ilizinduliwa na waziri wa mawasiliano june 13/1996.
Kwanza alipewa wiki sita kufanya kazi hiyo, na kuongezewa wiki mbili. Ripoti iliyotolewa na tume hiyo  ilikisia kwamba watu waliokufa   kutokana na ajali hiyo walifika 700 na walio nusurika walifika 114, na meli ilitoweka katika macho ya dunia
Ripoti inaonesha kwamba utaratibu wa kununua Mv Bukoba  ulipingana na taratibu za kimataifa kwamba serikali  na shirika la reli nchini  (TRC)  HAVIKUMLAZIMISHA MTENGENEZAJI WA MELI KUITENGENEZA KWA MUJIBU WA MATAKWA YA NCHI
Mtu anaweza akafikiria  kwamba kumbe haya tunayo yaona leo kuhusu machimbo ya madini, TANESCO, IPTL, na kadhalika yalianza zamani?  Bila ya kutaka kuitetea serikali ya awamu ya kwanza  au waziri wa mawasiliano na uchukuzi wa wakati ule   mh Amir Jamal, bora ikumbukwe kwamba,  katikati ya miaka 1970 ndipo jumuiya ya Afrika mashariki ilipovunjika.
Nchi ilikuwa katika wakati mgumu wa kuendeleza huduma zilizokuw azikitolewa na jumuiya wakati ule kama usafiri wa ndege, bahari, reli, nk.  Kilichokuwa katika nchi moja hakikuvuka mpaka.  Ndio maana , labda, baadhi ya mikataba ya wakati ule  ya kununua vitu kama vile  MV BUKOBA, au kukodi ndege ilikuwa haina miguu wala vichwa.
Lakini cha kujiuliza  ni, nini kimefanywa kwa takribani miaka 20  tangu meli ile ilipo nunuliwa mpaka kuja kuzama?  Ripoti inaonesha  kwamba shirika la reli la taifa( TRC)  ilikuwa ikijua fika juu ya hitilafu  zilizo kuwemo katika meli
Lakini badala yake shirika liliingia katika mlolongo mrefu wa barua na watengenezaji wa  meli na hayo hayakuleta tija yeyote  mpaka meli hii ikizama.  Ripoti inaonesha dhahiri kwamba katika shirika la reli la taifa  ambalo ndilo lililokuw alikiendesha MV BUKOBA,  MV victoria na meli nyinginezo,  milkuwa na uzembe, ubadilifu na kulijaa rushwa.
Ripoti ya tume ya jaji kisanga imelaumu wengi  kwa ajali hii, shirika la reli la taifa (TRC)  watengenezaji wa meli ubelgiji, BSC na serikali ya Ubelgiji kwa kuto timiza ahadi ya kutoa misaada katika kugharamia matengenezo ya meli yenyewe.
Taswira aipatayo mtu ni kwamba kulikuwa na hali ya kutojali kwa upande wa uongozi wanchi na kwa upande wa wafanyakazi wa MV BUKOBA na maafisa usalama wa TRC. Kulikuwa na hali ya kutojali kuwakamua  wananchi mpaka tone la mwisho la damu yao kwakuwa kulikuwa na shida ya usafiri.
Kwenye nchi zinazoenzi demokrasia  na utawala bora ajali kubwa mfano wa MV bukoba, viongozi huwajibika, na wanapo sitasita, basi wakuu wao huwawajibisha au wananchi, kwa kelele zao huwataka wawajibike.
Itakubukwa kwamba ilipotokea vifo vya watu wawili walio wekwa rumande na polisi kule Mwanza, waziri wa mambo ya ndani wa wakati huo, mzee Ally Hassan Mwinyi (Ambaye alikuja kuwa raisi wa zanzibari na Tanzania alijiuzulu) pamoja na  waziri aliye husika na usalama  wa taifa na mkuu wa mkoa wote walijiuzulu na raisi Julius Nyerere akawakubalia.
Walipotoroka watuhumiwa wawili wa kesi ya uhaini katika gereza la Ukonga na kukimbilia Kenya, waziri wa mambo ya ndani ya wakati ule  Maj-Gen Said Abdalah na mkuu wa gereza la Ukonga  walijiuzulu na raisi akawakubalia . Kinacho staajabisha umma na ulimwengu kwa ujumla  wakati ilipo tokea ajalia  ya Mv BUKOBA,  sii waziri wa mawasiliano wala uchukuzi  wala mkurugenzi mkuu wa TRC walio ona haja ya kujiuzulu.
Kikubwa zaidi ni kwamba raisi wa nchi ambaye ndiye aliwateua watu hawa  hakuona haja ya kuwawajibisha . Kelele za wananchi  na vyombo vya habari  za kuwataka viongozi hao wawajibike zilipuuzwa. Kujiuzulu kwa waziri hakungekuwa na maana kuwa alihusika moja kwamoja katika ajali ile, bali ni ustaarabu uliojengeka katika nchi nyingi duniani(political responsibility)
Ajali ya Mv Bukoba imeonesha wazi kabisa kuwa  nchi yetu haikujiandaa kwa maafa kwanamna yeyote ile. Ijapokuwa kumekuwepo na sharia na 9, ya mwaka 1990 ya utaratibu  na utoaji wa misaada ya maafa na kuundwa kwa kamati ya maafa ya taifa.
Sera ya maafa inaeleza kwa ufasaha  sana kuwepo kwa kamati ya maafa , kamati ya kitaalamu,  asasi ongozi,  timu ya kukabili maafa,  na kadhalika . lakini kila yatokeapo maafa  vyombo hivyo havionekani wala havisikiki. Sijui kama viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, pemba na tanga vimejiandaaje  na janga lolote linaloweza kutokea
Nyaisa anafaa kushukuriwa kwa  kazi hii nzuri na adhimu kunusurika kwake kutokana na kifo andiko kumetuwezesha leo kujua nini ni kilitokea.
Ikiwa hatujajifunza kutoka na makosa yaliyofanyika na kusababisha ajali hii, basi Tanzania itakuwa ni taifa lisilojifunza na lisilotathimini maisha ya watu wake. Waswahili husema kosa haliwi ni kosa isipokuwa likiwa limerejewa.

Prof Haroub Othman
 Chuo kikuu cha Dar es salaam
               Agost , 2007
My contacts +255766605392