“BWANA, wewe umekuwa makao yetu katika vizazi vyote. Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele. Huwarudisha watu mavumbini, ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.’’ Kwa maana kwako miaka elfu ni kama siku moja iliyokwisha pita, au kama kesha la usiku.

Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo, nao ni kama majani machanga ya asubuhi, ingawa asubuhi yanachipua, ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka. Tumeangamizwa kwa hasira yako na tumetishwa kwa ghadhabu yako. Umeyaweka maovu yetu mbele yako, dhambi zetu za sirini katika nuru ya uwepo wako.

Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako, tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza. Siku zetu za kuishi ni miaka sabini, ikiwa tuna nguvu ni miaka themanini, lakini yote ni ya shida na taabu, nayo yapita haraka, nasi twatoweka. Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako? Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako, Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa hekima” #Zaburi 90:1-12

Bwana Yesu atukuzwe mwana wa Mungu.

Ninamshukuru Mungu mkuu na Mungu mwaminifu kwa upendo wake juu yetu siku njema ya leo ambayo Bwana ametupa neema ya pumzi ya uhai. Ahimidiwe Mungu anayezidi kututia nguvu na kutustahimilisha katika kumtumikia Yeye. Ijumaa ya leo wewe ambaye utapata neema ya kuungana pamoja nasi kwenye maombi, basi pamoja na maombi yako binafsi uliyo nayo nakusihi sana hebu usiache kumwomba Bwana atupe neema ya akili atufundishe jinsi ya kuzihesabu siku zetu.

Wengi wetu hatujui namna ya kuzitumia siku zetu ambazo Bwana ametupa neema ya kuziishi. Na ndiyo maana wengi wetu tumejisahau kabisa. Hatuna maono mazuri ya kumtumikia huyu Mungu mkuu. Huwa tunadhana kana kwamba tunao muda wa kutosha wa kumtumikia Mungu. Ila ukweli ni kwamba muda tulio nao ni mdogo mno. Kama Mtunga Zaburi anavyosema siku za maisha yetu zinakimbia mno na tena ni za shida na taabu, nazo zapita haraka, nasi twatoweka. Kama siku zetu zinapita haraka na kutoweka kwa haraka maana yake ni muhimu kuitumia vizuri kila siku unayopewa neema ya kuiishi.

Kwa wastani kama wewe huwa unalala masaa 7 kwa usiku mmoja, kwa miaka 35 ina maana umelala miaka 10. Maana yake katika umri wa miaka 35 miaka yako 10 umekuwa usingizini. Miaka 25 iliyobaki fikiri majukumu ambayo umekuwa nayo kila siku ni kwa wastani gani umepata nafasi ya Mungu. Na bahati mbaya wengine hawajataka kujitoa kumwamini Yesu na kumtumikia. Fikiri jambo hilo.

Tunapotambua kwamba muda wetu wa kumtumikia Mungu ni mfupi mno basi tunahitaji neema ya Mungu tupewe akili ya kujua kuzihesabu siku zetu ili tuweze kumtumikia Mungu aliye hai. Ukweli ni kwamba hakuna kitu kingine hapa duniani cha kufanya zaidi ya kumtumikia Mungu.

“Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati”#Wakolosai 4:5. Tunahitaji neema ya kujua kuukomboa wakati tulionao mpendwa wangu. Vijana hii ni nafasi nzuri ya kumtumikia Mungu. Usidhani bado una nafasi ya kutosha ya kuishi duniani na uendelee kufanya anasa za dunia ukidhani una muda wa kutosha wa kutubu. Mtunga Zaburi anaonyesha dhahiri hatuna mkataba na Mungu maana siku zetu zinatoweka kwa haraka.

Ni maombi yangu Roho Mtakatifu akusaidie hata wewe uliyeokoka kujua namna ya kuzitumia siku ulizopewa na Bwana. Wengi wetu hatujui namna ya kuzitumia siku hizi kwa ajili ya kuujenga ufalme wa Mungu. Tunaenenda pasipo maono ya kumtumikia Mungu. Wengi tunaenenda pasipo kuwa na mipango na maono ya kumtumikia MUngu.

Wakati wowote Mungu anahitaji roho zetu maana ni mali yake. Hatuna mkataba na Mungu wa kuishi milele. Wakati wowote Bwana anahitaji roho zetu. Hivyo ni muhimu tukajua namna ya kuzihesabu siku zetu. Sio muda wa kucheza cheza kwenye wokovu lakini ni muda mzuri wa kuomba neema ya Kristo ya kumtumikia kwa uzuri na utakatifu.
Mwenye masikio ya kusikilia na asikie.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mwana wa Mungu na ikiwa umebarikiwa basi share ujumbe huu kwa mwingine naye abarikiwe

“YASIYOWEZEKANA KWA WANADAMU, YAWEZEKANA KWA MUNGU” #LUKA 18:27

Kwa maombezi, unataka kupokea uponyaji au kufunguliwa kwenye kifungo chochote kile, ushauri au unatamani ujitoe kikamilifu kumtumikia MUNGU na UNATAKA KUMPOKEA BWANA YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO NA AKUSAMEHE DHAMBI ABADILISHE MAISHA YAKO NA TABIA MBAYA ZILIZOKUSHINDA basi wasiliana nasi kwa msaada wa Roho Mtakatifu tukusaidie +255 758 443 873. Ukipiga simu isipopokelewa tafadhali acha sms.