Klabu ya soka ya Azam FC ‘Wanarambaramba’ wameitaja timu ya soka ya Mtibwa Sugar kuwa ni timu ngumu licha ya kushuka kiwango katika baadhi ya mechi za ligi kuu ambazo wamecheza hadi hivi sasa.
Hayo yameelezwa na afisa habari wa Azam Jaffary Idd Maganga, wakati ambapo Azam inatarajiwa kushuka dimbani kuumana na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Robo fainali ya Azam Sports Federations Cup siku ya Machi 31, 2018 katika uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
“Nitarudia kusema kwamba Mtibwa ni timu nzuri na ni timu ya ushindani, na ni timu ambayo msimu huu ilianza vizuri kwenye ligi lakini kushuka kwao kwenye msimamo wa ligi hakutufanyi sisi kubweteka na kuiona kuwa ni timu ya kawaida,” amesema Maganga.
Wachezaji wapo vizuri
Aidha Maganga ameendelea kuweka wazi kuwa kurejea kwa wachezaji wao ambao walikuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa kumewasaidia kwa namna moja ama nyingine kuongeza morali ndani ya kikosi.
“Wachezaji wapo vizuri, wachezaji ambao wanamejeruhi ni wawili tu Waziri Junior na Daniel Amoah, lakini wachezaji wetu ambao walikuwa kwenye timu ya Taifa wamesharipoti kambini wapo na wenzao, kwa hiyo kikosi kimezidi kuimarika maradufu baada ya ujio wao,” Maganga amesema.
Katika hatua nyingine Maganga amesema Mwalimu Aristica Cioaba ameutaja mchezo huo kuwa ni muhimu kwani wanajua mshindi ataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa na kutokana na kutoshiriki msimu huu wamepanga kufanya hivyo kwanza kwa kuchukua taji hilo.
Sare ya 1-1
Mara ya mwisho kwa Azam kucheza na Mtibwa Sugar katika uwanja wao wa nyumbani walitoka sare ya bao 1-1, bao la Azam likifungwa na Enock Atta Agyei wakati la Mtibwa Sugar likifungwa na Kelvin Sabato kwa faulo ya moja kwa moja.