Moja ya mabasi ya mwendokasi likishushwa kutoka kwenye meli.
Shughuli ya kuyashusha mabasi hayo ikiendelea.
Muonekano halisi baada ya kushushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, Charles Selemani akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea mabasi hayo.
Meli iliyobeba mabasi ya mwendokasi kama inavyoonekana ikiwa bandarini jijini Dar.


KAMPUNI itoayo huduma ya usafirishaji wa abiria kwa mabasi ya mwendo wa haraka jijini Dar,(Udart) imeingiza mabasi mapya 70 na kuyapokea bandarini jijini Dar katika kuhakikisha inaongeza nguvu na kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wateja wake.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuyapokea mabasi hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, Charles Selemani amewashukuru wakazi wa Dar kwa kuendelea kutumia usafiri huo na kwamba wazidi kuwa na imani juu yao ikiwa ni pamoja na kuwa wavumilivu kwa maeneo ambayo hayajafikiwa na usafiri huo kwani siku si nyingi mikakati hiyo itakamilika.

Aidha, Bw. Selemani ametoa ufafanuzi kuwa mabasi hayo yana uwezo wa kubeba abiria 150 hadi 160 ambapo yatasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuajiri idadi kubwa ya vijana wa Kitanzania na hivyo kuchangia uinuaji wa uchumi ndani na nje ya Jiji la Dar.

“Bado kuna watu walikuwa wanatumia magari binafsi kutokana na magari yetu kujaa, lakini ujio wa mabasi haya naamini utawafanya wayaache nyumbani magari yao na kupunguza gharama  kwa ajili ya usafiri binafsi,” alisema Selemani na kuongeza;

“Pia itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji , kwani kutokana na kubeba abiria wengi kupita kiasi yamejikuta yakiaharibika mara kwa mara na badala ya basi kukaa miaka nane, linakaa miaka minne.”
Amesema pamoja na kuongezeka kwa mabasi hayo, utaratibu wa abiria kusimama utaendelea kwa kuwa ndio usafiri wa majiji mengi duniani.