Na Masshele Emanuel

SIMBA imefanikiwa kushinda mechi nne mfululizo kwa idadi kubwa ya mabao ambayo yanaifanya kuwa timu hatari zaidi katika kipindi hiki unapozungumzia Ligi Kuu Bara.

Katika mechi nne, Simba imekusanya pointi 12, maana yake imeshinda bila ya kupotea hata moja, jambo ambalo linaonyesha mwendo wao ni mzuri zaidi.

Lakini utaona katika mechi zote nne, Simba imeshinda mabao 2-0 katika mechi mbili na 4-0 katika mechi mbili. Hawajaruhusu hata bao moja kutinga katika nyavu zao.

Katika ligi kama ya sasa ambayo ugumu wake unajulikana, timu kucheza mechi nne na kufunga mabao 12, si jambo dogo. Lakini timu kucheza mechi nne bila ya kuruhusu hata bao moja, maana yake ni kiwango bora kabisa cha utendaji kwa maana ya ulinzi na ushambulizi.

Mechi tatu za mwanzo, Simba iliifunga Ndanda FC kwa mabao 2-0 ikiwa ugenini, ikaitwanga Singida United 4-0 jijini Dar es Salaam na kusafiri kwenda Bukoba ambako waliivurumisha Kagera Sugar 2-0. Hapa kikosi kilikuwa chini ya Mrundi, Masoud Djuma.

Mechi ya nne, Mfaransa, Pierre Lechantre akawa ameanza kazi rasmi na akaanza na ushindi wa 4-0 dhidi ya Majimaji ambayo haikuwa imepoteza dhidi ya vigogo wengine watatu ambao ni Yanga, Azam FC na Singida United ambao wote walipata sare dhidi yake.

Mwendo wa Simba, unaonyesha utendaji bora wa muunganiko wa timu kuanzia ulinzi, kiungo katika uunganishaji wa ushambulizi na ulinzi lakini kazi bora kabisa ya washambuliaji.

Walinzi hawajafungwa au kuruhusu watu “kuchafua gazeti” lakini washambulizi wamefunga mabao mengi na unaona mshambuliaji mmoja kama John Bocco amefunga mabao matano na kutengeneza mawili katika mechi nne zilizopita.

Lakini Emmanuel Okwi aliyerejea kikosini, amefunga mabao manne na kutengeneza pia. Huku kukiwa na wengine kama Said Ndemla, Shiza Kichuya wakiwa katika mwendo mzuri.

Simba iko katika nafasi ya kuamua ubingwa mapema au kuchagua ijipe ugumu mwishoni kutokana na namna ubora wa kikosi chake ulivyo sasa.

Kwa asilimia 80, uchezaji umebadilika ukilinganisha na ule wakati Kocha Joseph Omog hasa katika ushambulizi. Kasi na pasi za haraka, mashambulizi ya kushitukiza na inaonekana wachezaji wanataka kucheza.

Kikubwa ambacho wachezaji walikosea mara nyingi hata wakati wa Omog ni kutozitumia nafasi kwa zaidi ya asilimia 100. Simba walitengeneza nafasi hadi sita na wasitumie hata moja au wangetumia moja tu.

Lakini sasa, wanaweza kutengeneza nne wakafunga mbili. Wakitengeneza sita wanafunga nne na hii inawafanya kuwa na kikosi kinachoweza kuamua ubingwa mapema sana.

Utajifunza kwamba, katika mechi nne, mbili wamecheza ugenini yaani katika viwanja nje ya Dar es Salaam, kila moja wameshinda mabao 2-0. Waliporejea Dar es Salaam, wameshinda mabao 4-0 kila mechi.

Utagundua Simba inapocheza kwenye Uwanja wa Taifa inaweza “kujiachia” zaidi kiuchezaji na kutafuta nafasi nyingi zaidi za kufunga.


Mechi tano zinafuatia, Simba watakuwa na kazi moja tu, kuhakikisha wawe walivyo, wakiweza basi kutakuwa hakuna mtu wa kuwazuia kuchukua ubingwa.

Kwa sasa wako kileleni wakiwa na pointi 35, zikiwa ni tofauti ya pointi tano na Azam FC katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 30. Lakini katika mechi sita zijazo za Simba, moja watacheza na Azam FC kama itakuwa imepangiwa tarehe.

Kama Simba itacheza na kushinda mechi hiyo au jumla ya mechi sita zijazo, hakika hakutakuwa tena na mwenye uwezo wa kuizuia kubeba ubingwa.

Mechi inayofuatia ya Simba itakuwa ni mzunguko wa pili rasmi. Maana yake itakuwa ina mechi 15 za mzunguko wa pili. Kushinda tano mfululizo, itakuwa ni rahisi wao kucheza hesabu zijazo na kama itashinda na kuifunga Azam FC maana yake itatengeneza pengo la pointi nane dhidi ya timu ya pili.

Inaweza ikawa rahisi kukumbuka kwamba Simba iliwahi kufikisha idadi hiyo lakini ikafikiwa na Yanga lakini somo hilo la kufikiwa linaweza kuwa chachu ya Simba kukataa kukosea tena.


Hayo yanaweza kuwa ya nje lakini kasi ya Simba katika ufungaji tena kuwa na watu takriban sita wanaofunga, inaipa Simba uhakika wa kufanya vema zaidi tena maradufu.

Lakini wachezaji, viongozi na benchi la ufundi wanaweza kuwa waamuzi sahihi wa mwendo huo, uendelee au wanaacha ukauke. Kwa kuwa kuna kipindi wanaweza kupata sare au hata kupoteza.

Hapo linaweza kuwa chaguo lao waendelee kama mwanzo au wayumbe na wapotee. Lakini kama watatulia na kuhakikisha mwendo walionao haushuki, hakika hakutakuwa na wa kuwazuia tena.

 MATOKEO MECHI 4 ZILIZOPITA:
Ndanda FC 0  Vs  2 Simba
Simba 4 Vs 0  Singida
Kagera 0 Vs 2  Simba
Simba 4 Vs 0  Majimaji

MECHI ZA SIMBA
Ruvu Shooting Vs Simba
Simba Vs Azam
Mwadui FC Vs Simba
Simba VS Mbao FC
Simba Vs Stand United

Mtibwa Sugar Vs Simba

Gmail, massheleemanuel@gmail.com
Phone +255766605392